Dar es Salaam. Serikali imetoa onyo kali kwa wanaochafua mazingira wakiwemo wazalishaji wa mifuko ya plastiki iliyopigwa marufuku, wanaotupa taka ovyo, kumwaga maji machafu baharini na kusababisha kelele mitaani, ikitangaza hatua za kisheria kuimarisha udhibiti.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Hamad Masauni, amesema changamoto hizo zinaendelea kulichafua Jiji la Dar es Salaam na majiji mengine, hivyo Serikali inakusudia kufanya mabadiliko ya sheria ili kuliwezesha Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuchukua hatua kali bila upendeleo.
Akizungumza leo Machi 30, 2026 katika Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Taka Sifuri jijini Dar es Salaam, Masauni amesema lengo ni kuhakikisha mazingira yanakuwa safi na salama.
Amesema mabadiliko hayo yataipa NEMC mamlaka zaidi ya kuwachukulia hatua wahusika wote, iwe ni taasisi za umma au binafsi, huku ikiwezeshwa kwa rasilimali watu na vitendea kazi.
Aidha, ameonya vitendo vinavyoendelea kukera ikiwemo umwagaji wa maji machafu baharini, kelele kwenye maeneo ya starehe na utupaji wa taka kwenye mitaro vinavyoathiri afya na ustawi wa wananchi.
Kwa mujibu wa takwimu, zaidi ya tani milioni saba za taka huzalishwa nchini kila mwaka, lakini ni asilimia 45 hadi 50 pekee hukusanywa ipasavyo, huku zaidi ya nusu ikibaki kwenye mazingira.
Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk Immaculate Semesi, amesema Serikali inaendelea kuimarisha mifumo ya ukusanyaji na urejelezi wa taka, akisisitiza umuhimu wa kuona taka kama rasilimali badala ya uchafu.
