Serikali yaingilia kati mgogoro wakulima, wafugaji Korogwe

Korogwe. Mvutano kati ya wakulima na wafugaji katika vijiji vya Magungacheki na Mkokola wilayani Korogwe umeingia katika hatua inayohitaji uingiliaji wa haraka wa mamlaka husika, kufuatia mgongano wa matumizi ya ardhi kati ya pande hizo mbili.

Hata hivyo, Serikali imeanza kuchukua hatua za kushughulikia mgogoro huo kwa kupeleka timu ya wataalamu kufanya tathmini ya kina.

Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti wafugaji hao akiwamo Fadhili Bakari, amesema Serikali inapaswa kuingilia kati mvutano huo haraka kwa kuwa mifugo yao inakosa njia za kupitisha mifugo yao kwenda kwenye malisho na maeneo ya kunyweshea maji.

Mmoja wa Wafugaji, Marmo Gumbe akizungumzia adha ya ng’ombe wake kukosa maji ya kunywa kifuatia njia kulimwa na kupandwa mpunga katika Kijiji cha Magungacheki wilaya ya Korogwe mkoani Tanga. 

“Ng’ombe wanakosa njia za kupita kwenda malishoni na kwenye maji, hali hii inatuumiza sisi wafugaji kwa sababu mifugo hii ndiyo tegemeo letu la maisha,” amesema Bakari.

Naye Yohana Paulo amesema wakulima wamelima mashamba yao mpaka kwenye maeneo wanayopitisha mifugo inapojaribu kutoka kwenye mazizi hukutana moja kwa moja na mashamba ya wakulima, hali inayoongeza migogoro ya kila siku.

“Hapa ukimtoa ng’ombe kidogo tu anaingia shambani, hivyo hali imekuwa ngumu kwa pande zote,” amesema.

Kwa upande wake, Shabani Lab kutoka kijiji cha Mkokola ameiomba Serikali kuingilia kati ili kuweka mipaka iliyo wazi ya matumizi ya ardhi ili kuepusha migogoro inayoendelea.

Mfugaji Hamis Gare amesema wameishi katika eneo hilo kwa muda mrefu lakini sasa wanahisi kushinikizwa kuondoka bila kupatiwa maeneo mbadala ya kuendeshea shughuli zao.

Naye Marmo Gumbe, mfugaji anayemiliki zaidi ya ng’ombe 400, amesema alihamia eneo hilo mwaka 2011 kwa ruhusa ya kijiji na kuwepo kwa utambuzi wa eneo lililotengwa kwa wafugaji.

Wafugaji wakizungumza na Mwenyekiti wa Wafugaji Mkoa wa Tanga, Ibrahim Molam wakati alopotembelea Kijiji cha Magungacheki katika wilaya ya Korogwe, Kijiji chenye mgogoro kati ya wakulima na wafugaji.   

“Kulikuwa na alama zinazoonyesha hili ni eneo la wafugaji, ndiyo maana tukaja hapa,” amesema.

Hata hivyo, Mwananchi imezungumza na Ofisa Ardhi wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe, Serena Kimari ambaye amesema tayari timu ya wataalamu imefika katika eneo la mgogoro kwa lengo la kukusanya taarifa kwa ajili ya hatua zaidi.

Lakini amesema changamoto kubwa iliyobainika awali ni ile ya wakati wa msimu wa kilimo, wakulima hujiongezea maeneo ya mashamba kuelekea maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya wafugaji kupitisha mifugo yao kuelekea malishoni.

“Tumekusanya nyaraka na taarifa zote kwa ajili ya kuziwasilisha kwenye Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya kwa maamuzi,” amesema Kimario.

Akizungumzia hilo, Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, William Mwakilema amesema Serikali imeanza kuchukua hatua za kushughulikia mgogoro huo kwa kupeleka timu ya wataalamu kufanya tathmini ya kina.

Amesema lengo ni kupata suluhisho litakalohakikisha haki inapatikana kwa pande zote mbili bila kuathiri maisha ya wakulima na wafugaji.

“Hatuwezi kuacha hali hii iendelee hivi, ndiyo maana nimeelekeza timu ya wataalamu ije na mapendekezo ya haraka,” amesema Mwakilema.

Kwa upande wa uongozi wa kijiji cha Magungacheki, unakiri kuwepo kwa mabadiliko ya matumizi ya ardhi yaliyochangia kuzuka kwa mgogoro kati ya wakulima na wafugaji.

Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Hamis Bila amesema awali eneo la Mazizini lilitengwa kwa ajili ya wafugaji, lakini baadaye mahitaji ya kilimo yaliongezeka na kusababisha sehemu ya eneo hilo kutumika kwa shughuli za kilimo.

Amesema kutokana na ongezeko la wakulima, kijiji kililazimika kuruhusu matumizi ya kilimo katika baadhi ya maeneo yaliyokuwa yakitumiwa na wafugaji.

Hata hivyo, amesema hadi sasa hakuna mpango rasmi wa kuwahamisha wafugaji, jambo linaloendelea kuongeza mvutano kwa kuwa pande zote mbili zinaendelea kutumia eneo moja kwa wakati mmoja.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Mkoa wa Tanga, Ibrahim Molam ameiomba serikali kuchukua hatua za haraka ili kurejesha utaratibu wa matumizi bora ya ardhi na kulinda haki za pande zote mbili, kwa lengo la kumaliza migogoro inayoendelea.

Mwenyekiti wa Wafugaji Mkoa wa Tanga, Ibrahim Molam akizungumzia mgogoro kati ya wakulima na wafugaji katika Kijiji cha Magungacheki katika wilaya Korogwe mkoani Tanga. Picha na Mbonea Herman

Kwa upande wa wakulima, baadhi yao wamesema walifika eneo hilo kulima baada ya kuona wenzao wameanza kujishughulisha na kilimo.

Mkulima Halid Juma amesema alikodishwa kulima katika eneo hilo na hakuwa na taarifa kuhusu mgogoro huo, akieleza kuwa alipofika alikuta tayari wakulima wengine wameshaanza shughuli za kilimo.

“Mimi ndiyo nimeanza kulima mpunga mwaka huu, lakini nilikuta tayari watu wengi wanalima hapa, ndiyo maana na mimi nikaja,” amesema.

Hata hivyo, ameiomba Serikali iwavumilie mpaka watakapovuna mazao yao (Mpunga) ndipo tathimini ifanyike upya.

Kwa upande wake, mkulima Baraka Issa amesema ni muhimu kila upande kuheshimu mipaka ili kuepusha migongano isiyo ya lazima.

“Wafugaji wanapaswa kudhibiti mifugo yao isiingie mashambani na Serikali isimamie sheria ili kila mtu afanye shughuli zake kwa utaratibu,” amesema.

Ameongeza kuwa ongezeko la watu na mifugo bila kuongezeka kwa rasilimali ardhi ni miongoni mwa sababu zinazochangia mvutano huo.