Ifakara.Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu imeanza kutoa msaada wa kibinadamu kwa wananchi walioathirika na mafuriko katika Halmashauri ya Mji Ifakara, mkoani Morogoro, huku mamlaka zikiwataka wakazi kuchukua tahadhari zaidi kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.
Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Pilly Kitwana amekabidhi msaada wa chakula, magodoro, vyandarua na mablanketi kwa watendaji wa kata ili usambazwe kwa wananchi waliokumbwa na mafuriko katika kata za Kibaoni, Lipangalala, Michenga, Mbasa na Lumemo.
Akizungumza leo Jumatatu Machi 30, 2026, baada ya kufanya ziara katika maeneo yaliyoathirika, Kitwana amesema mafuriko hayo yalitokea Machi 24 kufuatia mvua kubwa iliyosababisha mito kujaa na kufurika katika makazi ya wananchi.
Askari wa jeshi la zimamoto na uokoaji wilaya ya Kilombero akimuokoa mtoto Kwa kumbeba mgongoni baada ya mvua kubwa kunyesha Machi 24 na kusababisha mafuriko katika najata mbalimbali kwenye Halmashauri ya mji Ifakara. Picha Hamida Shariff
Amesisitiza kuwa watendaji wa kata wanapaswa kusimamia kwa karibu ugawaji wa misaada hiyo ili kuhakikisha inawafikia walengwa wote waliokusudiwa.
“Ni muhimu kuhakikisha msaada huu unawafikia wananchi wote walioathirika. Serikali imefanya jitihada kubwa kuwasaidia, hivyo usimamizi madhubuti unahitajika ili haki itendeke,” amesema Kitwana.
Ameongeza kuwa msaada huo umetolewa na Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, akibainisha kuwa wananchi wengi wamepoteza makazi, mali pamoja na vyakula kutokana na mafuriko hayo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Dunstan Kyobya amewataka wakazi wanaoishi katika maeneo ya mabondeni kuchukua tahadhari za haraka, ikiwemo kuhama katika maeneo hatarishi na kuelekea kwenye makazi salama yaliyotengwa na Serikali.
Amesema mvua zinazoendelea kunyesha zinaweza kusababisha madhara zaidi iwapo wananchi hawatazingatia maelekezo ya mamlaka husika.
“Pamoja na tahadhari tunazotoa, nawaomba wananchi kufuata maelekezo ya mamlaka na kuelekea katika maeneo salama yaliyotengwa kwa ajili ya makazi ya muda. Serikali ipo bega kwa bega nanyi,” amesema Kyobya.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa kata ya Kibaoni, Diwani wa kata hiyo, Rashid Namtuka, ameishukuru Serikali kwa kutoa msaada huo, akieleza kuwa umeleta faraja kwa wananchi waliopoteza mali zao.
Amesema kata yake ni miongoni mwa maeneo yaliyoathirika zaidi, ambapo wananchi wengi wamepoteza makazi, vyakula na mazao mashambani.
Baadhi ya nyumba zilizokumbwa na mafuriko ya Machi 24 katika kata ya kibaoni Halmashauri ya mji Ifakara baada ya kunyesha mvua kubwa. Picha Hamida Shariff
“Msaada huu utakuwa faraja kubwa kwa wananchi wetu. Tumepokea mahindi, magodoro, mablanketi na vyandarua ambavyo vitasaidia kupunguza makali ya hali waliyopitia,” amesema Namtuka.
Ameongeza kuwa awali zaidi ya watu 200 waliathirika na mafuriko katika kata hiyo na kuhifadhiwa katika maeneo ya muda, lakini baadhi yao wameanza kurejea katika makazi yao kwa ajili ya kufanya ukarabati.
Hata hivyo, amewatahadharisha wananchi kuendelea kuwa makini licha ya hali ya hewa kuanza kuimarika, akisisitiza kuwa mvua za masika bado zinaendelea na zinaweza kusababisha mafuriko mengine.
Mamlaka za Serikali zimeendelea kusisitiza umuhimu wa tahadhari na ushirikiano wa wananchi ili kupunguza athari za mafuriko, huku zikihakikisha msaada unawafikia wahitaji kwa wakati.