SONGEA: MRADI WA MIJI 28 WAFIKIA ASILIMIA 6.5, WALENGA KUONDOA CHANGAMOTO YA MAJI.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na usafi wa Mazingira Songea SOUWASA, Mhandisi Patrick Kibasa, amesema kuwa mradi mkubwa wa maji unaotekelezwa katika Manispaa ya Songea unaendelea vizuri, licha ya changamoto chache zilizojitokeza.

Mradi huo ni sehemu ya mpango wa Serikali wa kuboresha huduma za majisafi na usafi wa mazingira katika miji 28 nchini, ukilenga kumaliza changamoto ya maji kwa wakazi wa Songea.

Ameyasema hayo  Machi 30, 2026, wakati wa ziara ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Mjumbe wa Kamati Kuu, Maganya Fadhili Rajabu, aliyefika kutembelea maendeleo ya mradi huo wa kimkakati mkoani Ruvuma.

Kibasa ameeleza kuwa mkataba wa utekelezaji wa mradi ulisainiwa Machi 10, 2022 kati ya Wizara ya Maji na kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC), huku ujenzi ukianza rasmi Januari 2, 2024 na hadi sasa mradi umefikia asilimia 6.5 ya utekelezaji. 

Amesema mradi huo una thamani ya shilingi bilioni 145.77 unahusisha ujenzi wa kidaka maji katika Mto Njuga, mtambo wa kisasa wa kuchuja na kutibu maji wenye uwezo wa kuzalisha lita milioni 16 kwa siku, pamoja na matanki matatu ya kuhifadhi maji yenye ujazo wa lita milioni 9 kwa jumla.

Aidha, zaidi ya kilomita 60 za mabomba ya kusafirisha na kusambaza maji zinajengwa sambamba na ukarabati wa mtambo wa Matogoro ili kuongeza ufanisi wa huduma. Hatua zilizofikiwa ni pamoja na usanifu wa miundombinu, ujenzi wa matanki mawili katika maeneo ya Maji Wilaya na Chandamali, pamoja na ujenzi wa tanki la Mahilo lenye ujazo wa lita milioni 5 ambalo limefikia asilimia 70 ya utekelezaji.

Hata hivyo, Kibasa ameainisha changamoto ya mabadiliko ya chanzo cha maji kutoka bwawa lililopangwa awali kwenda Mto Njuga kutokana na sababu za kiufundi, hali iliyopunguza kasi ya utekelezaji wa mradi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa CCM Taifa, Maganya Fadhili Rajabu amesisitiza wananchi kuwa na subira huku akiitaka jamii kushirikiana na Serikali ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa mafanikio. 

Amesema Serikali chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan inaendelea kuchukua hatua madhubuti za kuboresha huduma za maji nchini, ikilenga kufikia upatikanaji wa maji kwa asilimia 100 katika maeneo ya mijini.

Mradi huo unatarajiwa kuondoa changamoto ya maji safi na salama kwa wakazi wa Songea na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika eneo hilo.