Dar es Salaam. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), imesema imeanzisha uchunguzi wa miradi 66 baada ya kubaini dosari walipofuatilia matumizi ya rasilimali za umma.
Miradi hiyo iliyoanzishiwa uchunguzi ni kati ya 913 iliyobainika kuwa na dosari, katika jumla ya miradi 1,864, ambayo taasisi hiyo iliifanyia uchunguzi wa matumizi ya rasilimali za umma kwa kipindi cha mwaka 2024/25.
Kwa mujibu wa Takukuru, miradi hiyo iliyofuatiliwa kwa ujumla wake ina thamani ya Sh14.3 trilioni. Hata hivyo idadi hiyo ni ongezeko kutoka miradi 1,773 yenye thamani ya Sh11.4 trilioni, iliyofuatiliwa mwaka 2023/24.
Hayo yameelezwa leo, Jumatatu Machi 30, 2026 na Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Chrispin Chalamila, alipowasilisha taarifa ya taasisi hiyo kwa kipindi cha mwaka 2024/25 mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Miradi hiyo iliyofuatiliwa, amesema ni Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT), Ujenzi wa miundombinu ya maji katika miradi 30 ya maji inayosimamiwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa) yenye thamani ya Sh187.1 bilioni katika mikoa kadhaa.
Mingine amesema ni 28 ya Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura), yenye thamani ya Sh43 bilioni na ufuatiliaji wa ulipaji fidia kwa waathirika wa mradi wa upanuzi wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti Bunda na ujenzi wa mabweni wa Sh4.3 bilioni Katavi na Rungwa, Mpanda mkoani Katavi.
Katika miradi hiyo 1,864 waliyofuatilia matumizi ya rasilimali za umma, amesema wamebaini kasoro katika miradi 913, kati ya hiyo 66 imeanzishiwa uchunguzi.
Ameeleza mwaka 2023/24 miradi 92 ilianzishiwa uchunguzi na hilo linadhihirisha kuwa miradi inayoanzishiwa uchunguzi inapungua kutokana na ufanisi wa ufuatiliaji wa Takukuru.
Chalamila, amesema wamebaini kuwepo kwa usimamizi dhaifu wa mikataba unaosababisha miradi kutekelezwa kinyume na matakwa ya mkataba husika na makandarasi kulipwa fedha kwa kazi ambazo hazikutekelezwa.
Kasoro nyingine, amesema kutokatwa kwa kodi ya zuia katika baadhi ya miradi, kutozingatiwa kwa sheria ya manunuzi ya umma, ubora wa kazi na vifaa usioridhisha na kufanyika kwa malipo zaidi ya matakwa ya mkataba.
Amesema dosari hizo zimekuwa zikijirudia na kwamba wasimamizi wa miradi waimarishe usimamizi ili kuepuka dosari zinazojirudia kila mwaka.
Mbali na kasoro hizo, amesema ufuatiliaji wa Takukuru umewezesha ukusanyaji wa mapato kuongezeka kwa zaidi ya Sh8.6 bilioni kwa mwaka katika halmashauri 40 zilizofanyiwa uchambuzi.
Makusanyo ya awali, amesema yalikuwa Sh97.8 bilioni na baada ya ufuatiliaji yameongezeka na kufikia Sh106.4 bilioni.
