TAKUKURU YAOKOA MABILIONI YA FEDHA KUPITIA OPERESHENI ZAKE

Na Said Mwishehe,Michuzi TV

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU),imesema kupitia operesheni mbalimbali za uchunguzi ilifanikiwa kuokoa kiasi cha Sh. bilioni 14.5.

Kati ya fedha iliyookolewa, Sh. bilioni 10.1 ni fedha taslimu ambayo iliwekwa kwenye akaunti za Taasisi na Idara za Serikali na Sh. bilioni 4.4 ilidhibitiwa sambamba na kurejesha vifaa na mali zilizoelekezwa kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Hayo yameelezwa leo Machi 30,2026 Ikulu jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Chrispin Chalamila wakati wa kukabidhi taarifa ya utendaji kazi wa TAKUKURU kwa mwaka 2024/2025 kwa Rais Dk.Samia Suluhu Hassan.

Wakati akitoa taarifa hiyo pamoja na kuelezea hatua mbalimbali ambazo zimechukuliwa na TAKUKURU Kudhibiti rushwa nchini ,Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo amesema uokoaji huo wa Sh. bilioni 14.5 unahusisha maeneo mbalimbali.

Kupitia taarifa hiyo ametaja baadhi ya maeneo ni kama ifuatavyo Sh. bilioni 1.2 ni limbikizo la fedha ya ushuru wa huduma uliotakiwa kulipwa kwa halmashauri mbalimbali na kampuni za Mastermind Tobacco Ltd na Beijing Construction Engineering Group Company Ltd. Kutokana na Operesheni za TAKUKURU, fedha hii ililipwa kwenye halmashauri husika.

Pia Sh. milioni 770 ni fedha ya mikopo iliyotolewa na Benki ya NBC kwa vyama vya ushirika vinavyolima zao la tumbaku. Awali, vyama hivyo vilishindwa kurejesha fedha hiyo lakini baada ya TAKUKURU kufuatilia, vyamahivyo vilirejesha fedha hiyo benki ya NBC, Tawi la Kahama mkoani Shinyanga.

Amesema pia Sh. milioni 221 ni fedha iliyotokana na uuzwaji wa viwanja vya Halmashauri ya Manispaa ya Kahama eneo la Nyasubi.

“Awali, waliopewa hati za umiliki wa viwanja husika, hawakuwa wamelipia gharama za ununuzi wa viwanja hivyo kulingana na utaratibu lakini kupitia operesheni za TAKUKURU, kiasi hicho cha fedha kimelipwa na wamiliki wa maeneo hayo.”

Pia amesema taarifa hiyo ya operesheni ya uchunguzi aliyowasilisha leo ni kuanzia Julai 2024 hadi Juni 2025, lakini katika kipindi cha Julai 2025 hadi Februari 2026, kiasi cha Sh.bilioni 101.8 kimeokolewa kutokana na operesheni mbalimbali za uchunguzi zilizofanywa na TAKUKURU.

Wakati huo huo amesema wakirejea katika taarifa yao, katika kipindi cha Julai 2024 hadi Juni 2025, TAKUKURU ilikamilisha uchunguzi wa majalada 1,030. Kati ya majalada hayo, 22 ni ya rushwa kubwa yenye thamani ya jumla ya Sh.bilioni 210.5.

“Idadi hii ya majalada 1,030 ya uchunguzi yaliyokamilika, imeongezeka ikilinganishwa na majalada 728 yaliyokamilika kwa mwaka 2023/24yakiwamo majalada 17 ya rushwa kubwa kwa mwaka huo. Ongezeko hili linatokana na kasi ya ushughulikiwaji wa tuhuma zinazowasilishwa katika ofisi za TAKUKURU.

“Uchunguzi wa majalada yaliyokamilika Mwaka 2024/25 pamoja na mambo mengine unahusisha; ruhuma za kughushi kadi za benki zilizoibiwa taarifa zake na kupelekea kiasi cha Sh.bilioni 147.5 kutolewa hapa nchini Tanzania katika akaunti za wateja pasipo ridhaa yao,”amesema Chalamila.

Akifafanua zaidi amesema uchunguzi wao ulibaini kuwa fedha hiyo ilitolewa kupitia malipo ya huduma na bidhaa kwa kutumia kadi 1,551 za wateja wa mataifa 11, kupitia makampuni 162 na benki tano (5)za hapa nchini Tanzania.

Pia amesema uchunguzi ulibaini kadi zilizoghushiwa zilitumika kufanya malipo mbalimbali ya huduma za utalii, usafirishaji, malipo ya kodi na bima ya afya.

Amesema Watuhumiwa walifanya utakatishaji fedha na kusababisha hasara ya Sh. bilioni 2.6 kwa baadhi ya benki.

Aidha amesema kampuni 82 ya utalii yaliyopo katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Dar es Salaam na Mwanza, yalitumia kadi zilizoghushiwa kinyume na Sheria ya Kanuni ya Adhabu na Sheria ya Uhujumu Uchumi.

“Katika uchunguzi huu, hadi kufikia Juni, 2025,TAKUKURU ilikuwa imeokoa jumla ya Sh.milioni 678 zilizorejeshwa benki.

“Uchunguzi mwingine ni wa tuhuma za mkataba baina ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na Tourist & Hotels Limited wenye thamani ya Shilingi bilioni 23 unaohusu uboreshaji na uendeshaji wa SOPA LODGE.”

Vile vile, ameniambia Rais Dk.Samia TAKUKURU imefanya uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu wa Sh. bilioni 19.1 za benki ya NMB mkoani Shinyanga.

Amesema uchunguzi huo ulibaini kuwa ubadhirifu huo umefanywa na wakopaji 42 walioshirikiana na washika dhamana wa Brent Intertrade Co. Ltd kupitia mikopo ya stakabadhi ghalani, pamoja na watumishi wasiowaaminifu wa benki ya NMB wa matawi ya Kahama na kuiibia benki hiyo kiasi cha Sh.bilioni 19.1.

“Katika uchunguzi huu, majalada 10yamekamilika, kati ya hayo saba yamepata kibali cha mashtaka ambapo jumla ya kiasi cha Sh. bilioni 4.2 zimeokolewa na kurejeshwa benki ya NMB.

“Majalada mengine yaliyochunguzwa yanahusisha uchunguzi uliotokana na taarifa ya CAG ya mwaka 2023/24 ambapo jumla ya majalada 86 yenye thamani ya Sh. bilioni 9.6 yalifanyiwa kazi. Kati ya majalada yaliyochunguzwa.

“Majalada 13 watuhumiwa walichukuliwa hatua za kinidhamu;majalada 36 kesi zinaendelea Mahakamani; kesi saba zilitolewa uamuzi Mahakamani ambapo Jamhuri ilishinda kesi hizo; na majalada 30yalifungwa kutokana na kukosekana kwa ushahidi. Kupitia uchunguzi wa tuhuma hizi, kiasi cha Sh.milioni 259.2 kiliokolewa.