Tanzania yanyakua ubingwa Ghana | Mwanaspoti

TIMU ya Taifa ya Wanaume ya Kriketi imetawazwa kuwa mabingwa wa mashindano ya kufuzu Kombe la Dunia la T20, Kanda ya Afrika B, ICC Men’s T20 World Cup Sub Regional Africa Qualifier B.

Mashindano hayo yaliyofanyika jijini Accra, Ghana, yalianza Machi 22 na kutamatika leo Machi 30, 2026, Tanzania iling’ara mbele ya mataifa mengine sita yaliyoshiriki, ambayo ni wenyeji Ghana, Malawi, Saint Helena, Eswatini, na Seychelles.

Ushindi huo umeifanya Tanzania na wenyeji Ghana kufuzu hatua inayofuata ya kufuzu Kombe la Dunia litakalofanyika mwaka 2028, Wabongo hao wakichukua wiketi 39 kati ya 40 za mashindano yote.

Timu hizo tayari zilikuwa zimehakikisha nafasi mbili za juu kabla ya mechi yao ya mwisho, lakini mvua ilisababisha mchezo wao kufutwa. Tanzania ilimaliza kileleni kwa tofauti ya net run rate dhidi ya Ghana.

Tanzania ilionyesha ilianza kwa kuifunga Malawi kwa wiketi nane, wakapata ushindi wa tofauti ya runi 158 kisha waliifunga Seychelles na Saint Helena na kuweka rekodi ya kutopoteza mechi hata moja.

KRI 01

Kwenye mashindano hayo timu hiyo pia ilinyakua tuzo binafsi za wachezaji, Ivan Selemani alichukua tuzo ya Mchezaji Bora wa Mashindano, Ajith Augustin aliondoka na Mfungaji Bora (Best Batsman) huku Laksh Bakrania akitwaa tuzo ya Mtupaji Bora wa Mpira (Best Bowler).

Wachezaji chipukizi Khalidy Juma na Laksh Bakrania walionyesha ushindani mkubwa kwa upande wa kupiga mipira (bowling), kila mmoja akichukua wiketi nane.

Mafanikio haya yanaonyesha kuwa Tanzania kwa upande wa kriketi ina hazina kubwa ya vipaji na inaendelea kuitangaza vyema nchi katika mashindano ya kimataifa.

KRI 02

Nahodha wa Tanzania, Kassim Nassoro Chete alisema walikwenda Ghana kwa dhamira ya kucheza kwa mipango na kuonyesha kiwango bora.

“Ni hisia isiyoelezeka kufuzu kwenda hatua inayofuata. Tulikuja hapa na mpango maalum wa kucheza kwa kushambulia tangu mwanzo, na wachezaji walitekeleza hilo kikamilifu katika kila eneo,” aliongeza kuwa

“Kumaliza mashindano bila kupoteza hasa kwa namna washambuliaji wetu walivyojitokeza inaonyesha tulichonacho sasa tunaiangalia Fainali za Kanda kwa kujiamini sana.”