Teknolojia mpya kukabili wahalifu wa misitu

Morogoro. Tanzania ikiwa na zaidi ya hekta milioni 48.1 za misitu, sawa na asilimia 55 ya eneo lote la nchi, Serikali imeanza kuimarisha mapambano dhidi ya uhalifu wa misitu kwa kutumia mbinu za kisasa za intelijensia na teknolojia, hatua inayolenga kulinda rasilimali hiyo muhimu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Hii imejidhihirisha kupitia mafunzo maalumu ya siku saba ya ufuatiliaji wa uhalifu, uchunguzi na operesheni yaliyoandaliwa kwa ushirikiano kati ya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), yakihusisha maofisa 45 wa TFS.

Profesa Agness Sirima wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) amesema uwekezaji katika mafunzo ya kiintelijensia ni hatua muhimu katika kuimarisha ulinzi wa misitu na kuhakikisha usimamizi wake unakuwa endelevu na wenye tija.

Baadhi ya maafisa wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wakifuatilia jambo katika mafunzo maalum ya siku saba ya ufuatiliaji wa uhalifu, uchunguzi na operesheni yaliyoandaliwa na FAO na TFS  yaliyofanyika Manispaa ya Morogoro. Picha na Juma Mtanda.

Takwimu zinaonyesha takribani nusu ya misitu ipo kwenye ardhi za vijiji na halmashauri, huku maeneo ya hifadhi yakifikia asilimia 40, jambo linalohitaji usimamizi makini na shirikishi.

Tanzania inapoteza takribani hekta 469,000 za misitu kila mwaka, huku asilimia 92 ya wananchi wakitegemea kuni na mkaa kama nishati ya kupikia, hali inayoongeza uharibifu.

Mkuu wa operesheni wa TFS, Charles Mwafute, amesema wakala unasimamia hifadhi 465 za Serikali kuu, mashamba 25 ya miti na hifadhi 26 za misitu ya asili, huku ukubwa na mtawanyiko wake ukiongeza changamoto za usimamizi.

TFS imeanza kutumia teknolojia ikiwemo ndege nyuki (drone), mifumo ya kijiografia (GIS) na picha za satelaiti ili kubaini haraka maeneo yenye uhalifu na kuchukua hatua.

Mhifadhi Mwandamizi Rosemay Sabida amesema teknolojia hiyo imeongeza ufanisi, kupunguza gharama na muda wa kufuatilia matukio ya uhalifu, ingawa bado kuna uhitaji wa vifaa na wataalamu zaidi.

Mkuu wa Ndaki ya Misitu, Wanyamapori na Utalii wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Profesa Agness Sirima akimkabidhi cheti, Rosemari Chuwa baada ya kumalizika kwa mafunzo maalum ya siku saba ya ufuatiliaji wa uhalifu, uchunguzi na operesheni yaliyoandaliwa na FAO na TFS yaliyofanyika Manispaa ya Morogoro. Picha na Juma Mtanda.

FAO kupitia Mratibu wake,  Diomedis Kalisa inashirikiana na Serikali katika maboresho ya sera, sheria na matumizi ya teknolojia, huku ikihamasisha matumizi ya nishati mbadala kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa.

Wahitimu wa mafunzo wametakiwa kutumia maarifa waliyopata kuimarisha ukusanyaji wa taarifa, kuboresha operesheni na kushirikiana na vyombo vya dola kudhibiti uhalifu.

Serikali itaendelea kuwekeza katika teknolojia, kuongeza vitendea kazi na kuimarisha ushirikiano na wadau kuhakikisha misitu inalindwa kwa ufanisi, kwa manufaa ya Taifa na vizazi vijavyo