Tope soko la Mabibo kero sugu, bila mabuti hutoboi

Dar es Salaam. Ikiwa imepita miaka mitatu tangu Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo kuchukua soko la Mabibo kutoka kwa wafanyabiashara, bado kero ya uwepo wa matope inaendelea sokoni hapo na watu kulazimika kukodi mabuti ili kuweza kuingia.

Soko hilo lilichukuliwa kutoka kwa wafanyabiashara ambao walikabidhiwa kwa tamko la Rais wa awamu ya tano, hayati John Magufuli mwaka 2020, hali iliyozua mvutano hadi kufika hatua ya waliokuwa viongozi wa soko kufukuzwa.

Amri ya kufukuzwa kwa viongozi hao ilitolewa na Mkuu wa Mkoa, Albert Chalamila mwaka 2023 na kulirudisha kwa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo ambao ndio wanaliendesha hadi sasa.

Hatua ya Chalamila kulirudisha soko hilo, ni kuwepo kwa tuhuma kuwa viongozi wa wafanyabiashara hao waliopewa dhamana ya kulisimamia soko hilo, kuwa kikwazo katika utoaji wa huduma bora na kufanya vitendo vya ubadhirifu wa fedha.

Baada ya mwezi mmoja tangu Halmashauri kukabidhiwa, Mwananchi ilitembelea sokoni hapo na kuzungumza na uongozi wa soko ambapo ulieleza mikakati mingi ya kuliboresha ikiwemo ujenzi wa mashedi ()mabanda makubwa na mrefu kwa ajili ya kukaa idadi kubwa ya wafanyabiashara na kupanga bidhaa zao, mitaro pamoja na barabara ambapo Sh600 milioni katika bajeti ya Manispaa ya mwaka 2023/2024 ilieleza kutengwa kwa kazi hiyo.

Hali ya matope ikiwa inaonekana katika soko la Mabibo upande wa wauza mbogamboga maarufu  geti la viazi.

Jana Jumapili, Machi 29, 2026,Mwananchi ilifika sokoni hapo na kushuhudia baadhi ya maeneo yakiwa yamefanyiwa ukarabati ikiwemo lile la wauza ndizi huku barabara ya kuingia sokoni hapo kwa upande wa bidhaa hizo ikiwa imewekwa zege.

Adha hiyo tope imegeuka fursa kwa baadhi ya watu ambao hukodisha mabuti kwa Sh1,000 na kuwanawisha miguu kwa Sh200 baada ya kutoka kufanya manunuzi.

Wakati kwa upande wa ndizi hali ikiwa inaridhisha , kwa upande wa mbogamboga maarufu geti la viazi hali bado ni mbaya kwani kumekuwepo na wingi wa matope hali inayosababisha si wateja wala wafanyabiashara kukodi mabuti ili kuweza kupita na  ambao hawana uwezo huo, walionekana wakivua viatu hali ambayo inahatarisha usalama wa afya zao.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wafanyabiashara, wamesema hali hiyo inawapa wakati mgumu hasa kipindi hiki cha mvua ambapo wateja wanapata taabu ya kuingia.

Mudy Ngoma amesema walifurahi walipoona ukarabati wa soko upande mwingine wa ndizi ulivyoanza muda mfupi tangu Halmashauri ilipokabidhiwa soko, lakini tangu mwaka jana ujenzi huo umesimama, huku wakiwa hawajui sababu ni nini.

Masoud Faham amesema hali hiyo ya matope imesababisha bidhaa nyingine zilizokuwa zikishushwa sokoni hapo, kwenda kushushwa masoko mengine na wao kuingia gharama ya kuzifuata.

“Kwa mfano karoti awali zilikuwa zikishushwa hapa sokoni, lakini sasa hivi zinashushiwa soko la Ilala, hivyo ukienda kuzichukua inakupasa kulipia ushuru wa soko la Ilala Sh1,000 na ukija hapa unalipia tena Sh500, bado hujawalipa waliokubebea na vifungashio gharama ambazo  mwisho wa siku zinaenda kumwangukia mwananchi wa kawaida,”amesema Fahamu.

Mmoja wa wateja aliyejitambulisha kwa jina moja la Hamza, amesema soko hilo huenda likachangia kueneza magonjwa ya mlipuko na kwa watu wastaarabu hawawezi kwenda, hivyo kuikosesha Serikali mapato na kuwapa hasara wafanyabiashara walioamua kujiajiri hapo.

Catherine Chale, mkazi wa Sinza, amesema ana imani halmashauri inapata mapato mengi kupitia hilo soko ambalo lipo eneo zuri la kibiashara na haoni kwa nini linakuwa chafu namna hiyo.

Wakati wafanyabiashara na wateja wakilalama hali hiyo ya matope, kwa upande wao wauza mabuti kwao ni neema ambapo wameleza wapo walioamua kuacha kuuza bidhaa nyingine katika kipindi hiki na kuhamia kwenye mabuti.

“Kama kwenye mabuti nina uwezo wa kupata hadi Sh60,000 kwa siku, wakati nikiuza mbogamboga sipati hiyo hela, kwa nini nisiitumie hii fursa, yaani kuna wakati unatamani mvua iendelee kunyesha hata mwaka mzima,”amesema Nusura Ally mmoja wa wauza mabuti.

Meneja wa soko hilo, Geoffrey Mbwama, amekiri kuwepo na hali hiyo ya matope sokoni hapo na kueleza kuwa kunachangiwa na maji yanayotoka mataa ya urafiki kupita sokoni hapo.

Hata hivyo, amesema mpango ni mitaro ya kuyaweza maji hayo kupita ni kujenga mashedi matano ambayo bajeti yake ya Sh500 milioni  inasubiriwa ipitishwe katika mwaka huu wa fedha huku malengo ikiwa ni kuanza ujenzi wake kuanzia Julai 2026.

‘Tayari Baraza la Madiwani limeshaidhinisha bajeti hiyo tunachosubiri ipitishwe  na Serikali kuu ili tuweze kuanza ujenzi ambapo sasa  hata mvua zikinyesha maji yatakuwa na mwelekeo wa kupita kuliko ilivyo sasa ikinyesha yanasambaa tu maeneo mbalimbali ya soko ,”amesema Mbwama.

Amesema ujenzi wa mashedi hayo utajumuisha moja la wafanyabiashara wa ndizi litakalounganika na mawili mengine ambayo yameshajengwa , na mojamoja ya wafanyabiashara wa  viazi, vitunguu, nyanya na mbogamboga huku kila moja likigharamu Sh100 milioni.

Kwa mujibu wa meneja huyo hadi sasa soko hilo maarufu kwa jina la Mahakama ya Ndizi, lina zaidi ya wafanyabiashara 5,000, huku wateja wanaofika kupata manunuzi kila siku wakiwa ni kati ya 10,000 hadi 12,000.