Dodoma/Dar. Bunge kesho Jumanne, Machi 31, 2026 linaanza safari ya siku 87 za kujadili na hatimaye kupitisha Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2026/27 huku umma wa Watanzania ukitarajia mambo kadhaa kwa mustakabali wa Taifa.
Mambo hayo yameelezwa na makundi mbalimbali ya wananchi, kutokana na uhalisia wa hali ilivyo sasa nchini na duniani, yakiwataka wabunge wayazingatie katika mjadala huo.
Miongoni mwa mapendekezo hayo ni wabunge hao kujenga hoja zitakazowezesha kupatikana kwa bajeti itakayodhibiti kupanda kwa bei ya mafuta, hasa ukizingatia kuwa duniani kuna tishio la kupanda kwa bei ya nishati hiyo.
Mzigo mwingine waliowatwisha wabunge ni kuona namna ya kuifanya bajeti hiyo ijikite katika kujenga uchumi wa kujitegemea, kuondoa kodi zenye kero, kuimarisha usalama wa chakula na miundombinu.
Wadau wanakuja na mapendekezo hayo, Serikali ikiwa tayari imeshatangaza mwelekeo ya Bajeti hiyo, inayotazamiwa kuwa Sh62.33 trilioni, ambayo ni asilimia 10 zaidi ya ile ya mwaka wa fedha unaomalizika Juni 30, 2026, ambayo mkazo umewekwa katika makusanyo ili kujitegemea.
Akiwasilisha Mpango wa Serikali na Dira ya Taifa 2050, Waziri wa Fedha Hamisi Mussa Omary, aliwaeleza bayana wabunge kuwa katika bajeti ijayo, sekta binafsi itakuwa ndiyo injini kuu.
Udhibiti bei ya mafuta
Mchambuzi wa masuala ya siasa na utawala, Martine Lissu, amesema wabunge hao wanapaswa kufikiria mbinu za kupendekeza ili bajeti hiyo idhibiti bei za mafuta na kuhakikisha hazidi Sh3, 000.
Amesema kwa sababu kuna tishio la kufungwa kwa Mfereji wa Hormuz unaopitisha mafuta ambayo hata Afrika inanufaika nayo, bei za nishati hiyo zinaweza kupanda kupita kiasi, hivyo wabunge wahakikishe bajeti inalidhibiti hilo lisitokee.
Kinachopaswa kufanywa katika hatua ya sasa, Lissu amesema ni kuhakikisha nchi ina akiba ya mafuta ya kutosha katika hifadhi yake, huku ikiendelea kutengeneza mahusiano mazuri na mataifa yote ili kuendelea kupata nishati hiyo.
Usalama wa chakula
Mchambuzi huyo, amesema mvua zinazoendelea kunyesha zimesababisha athari katika uzalishaji wa baadhi ya mazao, ikiwemo vitunguu.
Mazao hayo, amesema yameharibika mashambani na kuna hatari ya mahindi nayo kuharibika kutokana na mvua hizo, hivyo uzalishaji katika mwaka huu huenda ukapungua.
“Ni muhimu kuangalia hifadhi ya chakula ili iwe kubwa, tusijikute tunakumbwa na janga la njaa litakalolazimu bajeti iliyopangwa kwa maeneo mengine itumike kuagiza chakula nje,” amesema.
Uboreshaji wa miundombinu ya usafiri na usafirishaji ni eneo lingine alilopendekeza lisimamiwe ili kurahisisha usafirishaji wa mizigo na bidhaa na hatimaye kukuza uchumi.
Pendekezo lake lingine ni kupunguzwa kwa bei ya umeme na maji, akisisitiza kuwa hizo ni huduma kwa wananchi na zinahitaji kurahisishwa ili kupunguza gharama za maisha.
“Kama umeme tayari tuna Bwawa la Mwalimu Nyerere na vyanzo vingine, ni jambo muhimu tuhakikishe tunapunguza bei ya uniti ya umeme na maji,” amesema.
Kulinda uchumi
Kwa upande wake Dk Nasibu Mramba, mchambuzi wa masuala ya bajeti na uchumi wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), amesema ni muhimu wabunge hao wahakikishe bajeti inajikita katika kuangalia viashiria vya kiuchumi zaidi kuliko mambo mengine.
Pendekezo lake hilo linatokana na kile alichofafanua kuwa tayari kumeanza kuonekana dalili mbaya za kiuchumi duniani; mataifa makubwa yamepunguza ufadhili, Mashariki ya Kati inakabiliwa na vita na Tanzania ilikumbwa na vurugu Oktoba 29, 2025.
“Inaweza kuwa bajeti nzuri kwa maneno lakini utekelezaji wake ukawa mgumu, tena huenda hata kabla ya kufikia miezi mitatu, hivyo Serikali ijipange kwa namna yoyote itakavyokuwa,” amesema Dk Mramba.
Katika mazingira kama hayo, amesema uelekezaji wa bajeti kubwa katika uimarishaji wa sekta ya kilimo, ili kisiathiriwe zaidi na mabadiliko ya tabianchi, utakuwa uamuzi sahihi kwa maslahi ya kiuchumi.
Hofu ya changamoto za kiuchumi wakati wa utekelezaji wa bajeti, imeibuliwa pia na Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Anna Henga, aliyesema hata nchi zilizokuwa zinaisaidia Tanzania, mataifa ya Ulaya, Marekani na wengine, sasa zimejikita kulinda uchumi wao wa ndani.
“Tutarajie kutakuwa na mfumuko mkubwa wa bei kwa sababu hata mataifa yanayozalisha mafuta yako kwenye migogoro mikubwa,” amesema.
Mwanaharakati huyo amesema mwaka 2026/27 ni miongoni mwa miaka ambayo Serikali inapaswa kuwa makini zaidi katika utekelezaji na usimamizi wa bajeti.
Soko la madini
Rais wa Shirikisho la Wachimbaji Madini Tanzania (Femata), John Bina ametahadharisha umuhimu wa kuwa makini katika kulinda rasilimali za umma kutokana na hali mbaya ya kiuchumi duniani.
Katika hilo, ametoa mapendekezo mawili akitaka Tanzania kujenga soko la madini la Afrika ili nchi zenye migogoro ziweze kununua na kuuza nchini, huku Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ikiendelea kuhifadhi madini kama inavyofanya sasa.
Uchumi jumuishi
Mkurugenzi wa Miradi wa Taasisi ya Sauti ya Wenye Ulemavu Tanzania, John Mlabu amesema matarajio ya kundi hilo ni kuona linashirikishwa kikamilifu katika uchumi.
Amesema suala la miundombinu limeanza kuboreshwa, lakini masharti ya upatikanaji wa mikopo kwa wenye ulemavu bado ni changamoto.
“Uwezeshaji usiwe wa jumla tu, sisi tuna changamoto nyingi. Unakwenda benki wanashindwa kuidhinisha Sh5 milioni eti kwa sababu unadaiwa Sh500 kwenye M-Pawa, hii siyo sawa,” amesema Mlabu.
Kujitegemea
Mwenyekiti wa Chama cha Sauti ya Umma Mkoa wa Dodoma, Emmanuel Ngobito ameomba Serikali kutumia kila njia kuhakikisha bajeti inakuwa ya kujitegemea zaidi badala ya kutegemea misaada ya nje.
Ili kufikia hapo, amependekeza iwaguse wananchi wa kipato cha chini, wakiwemo mamalishe, mafundi viatu na makundi mengine ambayo hayakuwa yakilipa kodi, kwa kuyapa viwango rafiki.
“Hapa kinachotakiwa ni elimu kwanza. Kila Mtanzania aone fahari kulipa kodi na isiwe kero. Wabunge wakemee tabia ya baadhi ya maofisa wa kodi kuwabughudhi wafanyabiashara badala ya kuzungumza nao,” amesema.
Mwenyekiti wa Wamachinga Mkoa wa Dodoma, Christian Msumari, amesema matarajio yao ni kuona bajeti inaleta mpango mkakati wa kupatikana maeneo rasmi ya kufanyia biashara.
Amesema katika kipindi cha miaka mitatu, wafanyabiashara ndogondogo wengi wamepoteza mitaji yao kutokana na operesheni za kuwaondoa maeneo ya biashara.
Ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano iliwahi kutoa ruhusa ya wafanyabiashara kufanya biashara maeneo mbalimbali bila kusababisha usumbufu kwa wengine.
“Wakati ule Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano alisema tufanye biashara popote ilimradi tusiwe kero kwa wengine. Hapo tulipata amani sana, lakini sasa tunafukuzwa na wengine wamepoteza kabisa mitaji yao,” amesema Msumari.
