Tanga. Watumishi wawili wa halmashauri katika wilaya za Korogwe na Muheza mkoani Tanga wamenaswa kwa tuhuma za ubadhirifu wa fedha za umma Sh9.5 milioni.
Ni baada ya uchunguzi uliofanywa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kubaini walihusika na upotevu wa fedha hizo zilizokusanywa kupitia mashine za POS.
Kwa mujibu wa taarifa ya Takukuru, Mkoa wa Tanga, watumishi hao walifikishwa mahakamani na baadaye kukubali kurejesha sehemu ya fedha hizo kupitia utaratibu wa makubaliano ya kukiri kosa kwa hiari, hatua iliyowezesha kurejeshwa kwa jumla ya Sh5 milioni.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Machi 30, 2026, Kaimu Kamanda wa Takukuru, Mkoa wa Tanga, Mariam Mgaya, amesema hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za taasisi hiyo kudhibiti ubadhirifu na kulinda rasilimali za umma.
Hata hivyo, hakuwataja watumishi hao.
Mbali na hatua hiyo ya kisheria, Mgaya amesema Takukuru imefanikiwa pia kuzuia matumizi mabaya ya zaidi ya Sh12 milioni kufuatia ufuatiliaji wa kina wa miradi ya maendeleo uliofanyika kati ya Oktoba hadi Desemba 2025.
Amesema ufuatiliaji huo ulilenga kuhakikisha fedha zinazotolewa kwa ajili ya miradi ya maendeleo zinaendana na thamani halisi ya kazi inayotekelezwa ili kuwanufaisha wananchi.
Katika ukaguzi huo, dosari zilibainika katika mradi wa ujenzi wa madarasa matatu katika Shule ya Msingi Kwedihwahwala, kata ya Mgambo wilayani Handeni, ambapo halmashauri ilitoa Sh12.5 milioni kwa ajili ya kukamilisha darasa moja.
Mgaya amesema kazi za umaliziaji wa jengo hilo, zikiwemo upigaji wa rangi na uwekaji wa gypsum board, zilifanyika chini ya kiwango huku baadhi ya vifaa vilivyotumika vikiwa havikidhi ubora unaotakiwa.
“Tulibaini mapungufu katika hatua za umaliziaji wa jengo hilo, hivyo tuliagiza kazi irudiwe ili kuendana na thamani ya fedha iliyotumika,” amesema Mgaya.
Ameongeza baada ya maelekezo hayo, kazi ilirudiwa na kukamilika kwa kiwango kinachoridhisha, jambo lililothibitishwa na kamati ya shule pamoja na wananchi kupitia vikao vya maendeleo.
Katika kipindi hichohicho, Takukuru ilipokea jumla ya malalamiko 64, ambapo 42 kati ya hayo sawa na asilimia 65.6 yalihusu vitendo vya rushwa.
Amesema malalamiko yote yanayohusu rushwa yamefunguliwa majalada ya uchunguzi na yapo katika hatua mbalimbali, wakati yale yasiyohusu rushwa yameelekezwa katika mamlaka husika kwa hatua zaidi.
Kwa upande wa mashauri ya mahakamani, Mgaya amesema jamhuri imefanikiwa kushinda kesi mbili huku tano zikiendelea kusikilizwa katika mahakama mbalimbali.
Alisisitiza kuwa Takukuru itaendelea kusimamia kwa karibu matumizi ya fedha za umma ili kuhakikisha kunakuwa na uwajibikaji na thamani halisi ya fedha katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Katika kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2025, taasisi hiyo ilifuatilia jumla ya miradi 55 ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya Sh9.35 bilioni katika sekta mbalimbali zikiwemo afya, elimu, maji, miundombinu, usafirishaji, utawala na biashara.
