ACT Wazalendo kugharimia mazishi ya Bwege

Dar es Salaam. Chama cha ACT Wazalendo kimeeleza kushtushwa na kuhuzunishwa na kifo cha aliyekuwa mwanachama wake, Seleman Bungara maarufu Bwege, huku kikiahidi kugharimia mazishi yake.

Bwege amefariki dunia ghafla leo asubuhi Machi 30, 2026, wakati akipatiwa matibabu ya kusafisha figo katika hospitali moja jijini Dar es Salaam.

Taarifa iliyotolewa na kiongozi wa chama hicho, Dorothy Semu, imeeleza kuwa kifo hicho ni pigo kubwa si tu kwa familia, bali pia kwa chama na wafuasi wa siasa za upinzani nchini.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Bungara alikuwa akipatiwa huduma ya kawaida ya matibabu kabla ya umauti kumkuta, hali iliyozua simanzi kwa wale waliomfahamu na kushirikiana naye katika harakati za kisiasa.

“Tumepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa za kifo cha ndugu Seleman Bungara. Alikuwa mwanachama wetu kabla ya hivi karibuni kutangaza kuhama chama,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Semu ametumia nafasi hiyo kutoa pole za dhati kwa mke wa marehemu, Mwanawetu Said Zarafi, ambaye pia ni mjumbe wa Bodi ya Wadhamini ya ACT Wazalendo, pamoja na familia nzima, ndugu, jamaa na marafiki walioguswa na msiba huo.

Amesema Bungara atakumbukwa kama mwanasiasa jasiri wa upinzani aliyesimama kidete kutetea haki, misingi ya demokrasia na mfumo wa vyama vingi nchini.

Katika hatua nyingine, chama hicho kimeahidi kushiriki kikamilifu katika msiba huo, ikiwemo kugharamia mazishi ya marehemu, sambamba na kutoa wito kwa wanachama wake, hususan wa jimbo la Kilwa Kusini, kuungana na familia katika kipindi hiki kigumu.

“Msiba huu si wa familia pekee, bali ni wa ACT Wazalendo kwa ujumla,” imeeleza taarifa hiyo.