KIWANGO cha Yanga kimemuibua kiungo wa zamani wa klabu hiyo, Stephane Aziz Ki akiwatia nguvu mastaa kwamba watarejea kwenye ubora.
Yanga imekuwa haina matokeo mazuri katika mechi tatu mfululizo, ambako kote ilitoka na sare dhidi ya Azam FC, TRA United na Mtibwa Sugar.
Ukiachana na sare hizo timu hiyo imekuwa na bahati mbaya baada ya wachezaji wake kadhaa wakubwa kukumbwa na majeraha wengi wakiwa ni wale ambao walikuwa tegemeo kubwa kwenye safu ya ushambuliaji kama Clement Mzize ambaye hataweza kucheza tena msimu huu, lakini wamo Aurelio Depu na Prince Dube wengine ni Dickson Job, Ibrahim Hamad ‘Bacca’ na Chadrack Boka ambao wamekumbwa na majeraha kwa nyakati tofauti.
Akizungumza na Mwanaspoti, Aziz ambaye anaitumikia Al Ittihad ya Libya amesema anafahamu kuwa kikosi hicho kinapitia wakati mgumu, lakini anaamini kuwa mambo yatakuwa mazuri hivi karibuni.
Amesema bado anaamini kwamba Yanga itarudi kwenye ubora wake licha ya changamoto ambazo wamekumbana nazo msimu huu.
“Yanga ni timu kubwa na hiki ni kipindi cha mpito ambacho inapita, lakini naamini kikosi hicho kitarejea kwenye kiwango bora.
“Watu hawatakiwi kusahau kwamba hii ndiyo timu inayobeba ubingwa mara nne mfululizo, malengo ya Yanga bado hayajabadilika, kwani wanataka kumaliza msimu wakiwa kwenye nafasi ya juu na kutwaa ubingwa, hivyo lazima kila mmoja atapambana kuhakikisha anabadilisha hali hii iliyopo sasa.
“Kuna mshikamano mkubwa ndani ya kikosi na kila mmoja yuko tayari kujitoa kwa ajili ya mafanikio ya timu kwa ujumla, naamini hilo ni jambo ambalo litatimia bila shida yoyote.”
Ikumbukwe kuwa, Aziz aliitumikia Yanga kwa misimu mitatu kabla ya kwenda Wydad ya Morocco ambako aliichezea nusu msimu na kuuzwa Al Ittihad ya Libya. Akiwa na Yanga alifanikiwa kuwa mfungaji bora Ligi Kuu Bara 2023/2024 akifunga mabao 21 mawili mbele ya Feisal Salum Fei Toto aliyefunga mara 19.
