Bahati. Katika kuhakikisha shoroba za wanyamapori zinatunzwa na mazingira yanaendelea kustawi, wadau wa mazingira wamepanda miti 5,000 katika eneo la Vilima vitatu ili kudhibiti uharibifu wa mazingira na kuunga mkono juhudi za Serikali za kupanda miti milioni 1.5 kwa kila halmashauri kwa mwaka.
Akizungumza leo Machi 31, 2026, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, Anna Mbogo, amesema upandaji huo utasaidia wanyama kupata chakula na maeneo ya kupumzika wakati wa jua kali.
Amesema eneo hilo linaunganisha Hifadhi ya Taifa Tarangire, Jumuiya ya Wanyamapori Burunge (WMA), Hifadhi ya Ziwa Manyara na Hifadhi ya Taifa Serengeti.
Mbogo amesema uwepo wa miti ni muhimu kwa wanyama, akitolea mfano twiga anayehitaji miti mirefu kwa ajili ya chakula. Ameongeza kuwa halmashauri inalinda miti kwa kufanya doria kwa kushirikiana na wadau wa uhifadhi na halmashauri, na yeyote anayeharibu huchukuliwa hatua za kisheria. Pia walinda mazingira si katika hifadhi pekee bali hadi kwenye misitu ya vijiji.
Amesema hatua hiyo ni endelevu kila mwaka kulingana na maelekezo ya Serikali ya upandaji miti kwa halmashauri zote.
Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Itracom Fertilizer Ltd Vilima vitatu, Nestor Nibitanga, amesema walichukua hatua ya kushirikiana na wadau kupanda miti baada ya kubaini ukataji uliokuwa unaendelea bila urejeshaji.
Amesema pia upandaji miti umesaidia kupunguza vumbi kutoka kiwandani ambalo lilikuwa linaathiri miundombinu ya umeme.
Mwakilishi wa mhifadhi misitu Wilaya ya Babati, Josephine Alphonce, amesema upandaji miti unasaidia kudhibiti mabadiliko ya tabianchi, kurejesha uoto wa asili na kutoa makazi kwa wanyamapori.
Mhandisi migodi wa ofisi ya madini mkoa wa Manyara, Ezekiel Izack, amesema juhudi za Itracom katika utunzaji wa mazingira ni chanya na shughuli hiyo ya upandaji miti itakuwa na manufaa ya muda mrefu.
Shughuli hiyo iliwashirikisha maofisa mazingira, viongozi wa vijiji na kata, ofisa madini mkazi, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) mkoa wa Manyara, wafanyakazi wa Itracom Fertilizer Ltd pamoja na wananchi.
