BMH Kuadhimisha Miaka 10 kwa Harambee ya Bilioni 7 Kuboresha Huduma za Upandikizaji Uloto na Figo

Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) iliyopo jijini Dodoma, inatarajia kuhitimisha rasmi maadhimisho ya miaka 10 tangu kuanzishwa kwake kwa kufanya harambee maalum ya kuchangisha fedha kwa ajili ya matibabu ya upandikizaji uloto na figo kwa wananchi wenye uhitaji.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Profesa Abel Makubi, amesema kuwa maadhimisho hayo yalianza Oktoba 13, 2025, na yatahitimishwa Mei 8, 2026, baada ya kudumu kwa takribani miezi saba.

Prof. Makubi amesema kuwa lengo kuu la maadhimisho hayo ni kuhamasisha wadau kushiriki katika harambee itakayolenga kukusanya shilingi bilioni 7 ndani ya kipindi cha miaka miwili. Fedha hizo zitatumika kusaidia matibabu ya wagonjwa 100, ambapo 50 ni watoto wenye ugonjwa wa selimundu wanaohitaji upandikizaji wa uloto, na wengine 50 ni wagonjwa wa figo.

Ameeleza kuwa gharama za matibabu hayo ni kubwa, hivyo hospitali imeona umuhimu wa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) pamoja na taasisi nyingine ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma hizo muhimu.

Kwa mujibu wa Prof. Makubi, hospitali hiyo kwa sasa inahudumia takribani wananchi milioni 10 kutoka mikoa nane ya Tanzania, na imeanza pia kupokea wagonjwa kutoka nje ya nchi kama sehemu ya kukuza utalii wa matibabu.

Ameongeza kuwa hospitali hiyo ina jumla ya watumishi 1,173, wakiwemo madaktari bingwa zaidi ya 100, na kwa sasa inatoa huduma 20 za kibingwa pamoja na huduma 18 za ubingwa bobezi.

Katika hatua nyingine, Prof. Makubi amesema BMH ina mipango ya kuanzisha miradi ya kimkakati ikiwemo vituo vya umahiri katika matibabu ya saratani, upanuzi wa huduma za upandikizaji uloto, pamoja na kuanzisha taasisi maalum za macho, moyo, na upasuaji wa ubongo na mifupa ndani ya miaka mitano ijayo.

Amesema lengo ni kuifanya hospitali hiyo kuwa kitovu cha utalii wa matibabu nchini na barani Afrika.

Katika kilele cha maadhimisho hayo, mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Sambamba na hilo, hospitali imepanga kufanya kongamano la kisayansi Mei 6, 2026, litakalowakutanisha wataalam wa afya, hususan katika masuala ya upandikizaji wa viungo.

Prof. Makubi ametoa wito kwa taasisi za afya, wadau wa maendeleo na wafadhili kujitokeza kwa wingi kuunga mkono juhudi hizo ili kusaidia kuokoa maisha ya wananchi wenye uhitaji wa matibabu hayo ghali.