Dar es Salaam. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesitisha kwa muda mpango wake wa kuuza akiba ya dhahabu kufuatia kushuka kwa bei katika soko la dunia, hatua inayoashiria mabadiliko ya tahadhari kadri hali ya soko inavyozidi kuwa tete.
Mapema Machi 2026, BoT ilisema inazo takribani tani 19.6 za dhahabu, ikikaribia lengo lake la tani 20.
Benki hiyo imekuwa ikiongeza kwa kasi akiba ya dhahabu tangu Oktoba 2024 ili kuimarisha akiba ya fedha za kigeni na kupanua aina ya mali zake, huku ikiwa na mpango wa kuuza sehemu ya dhahabu hiyo ili kuweka usawa katika uwekezaji wake.
Uamuzi huo unakuja wakati bei za dhahabu kimataifa imeanza kushuka baada ya kupanda kwa kasi mwanzoni mwa mwaka huu. Kufikia Machi 31, 2026, bei ya dhahabu ilikuwa takribani dola 4,555 za Marekani kwa wakia, kwa mujibu wa tovuti ya Trading Economics.
Ingawa bei hiyo ni juu kidogo kutoka dola 4,426 hadi 4,430 kwa wakia zilizorekodiwa Machi 24, 2026; bado iko chini ya kiwango ambacho BoT ilikuwa imepanga kuuza sehemu ya akiba yake.
Kabla ya kuanza kushuka bei hiyo ilikuwa imepanda hadi kufikia zaidi ya dola 5,000 kwa wakia ndani ya muda mfupi, kutokana na ongezeko la mvutano wa kisiasa duniani na mahitaji makubwa ya dhahabu kama sehemu salama ya uwekezaji.
Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba ameliambia gazeti dada la The Citizen kuwa benki hiyo ilikuwa imepanga kuuza sehemu ya dhahabu bei ilipofikia karibu dola 5,500 kwa wakia lakini sasa imeamua kusubiri.
“Bei zimeshuka kidogo, hivyo huu si wakati mzuri wa kuuza,” alisema. “Wakati soko linashuka, huwa ni wakati mzuri wa kununua, kwa hiyo tunaendelea kufuatilia hali ya soko.”
Aliongeza kuwa ingawa bei za sasa bado ni kubwa kuliko dola 2,400 hadi 2,500 kwa wakia ambazo benki ilinunulia dhahabu hapo awali, BoT itasubiri kuona kama bei zitapanda tena kabla ya kufanya uamuzi.
Wachambuzi wanasema kushuka kwa bei kunatokana na mabadiliko ya mtazamo wa wawekezaji duniani badala ya kupungua kwa umuhimu wa dhahabu kwa muda mrefu.
Mambo kama kupungua kwa mvutano wa kisiasa, viwango vya juu vya riba na wawekezaji kuchukua faida yamepunguza mahitaji ya dhahabu.
Kupanda kwa bei hapo awali kulichochewa na hofu ya migogoro ya Mashariki ya Kati, iliyowasukuma wawekezaji kuelekea dhahabu kama sehemu salama ya kuhifadhi thamani. Hata hivyo, dalili za kupungua kwa mvutano huo zimepunguza mahitaji na kusababisha bei kushuka kidogo.
Wakati huohuo, viwango vya juu vya riba vinavyotolewa kwenye uwekezani kama hatifungani duniani vinaendelea kuathiri bei dhahabu kwa kuwa vinavutia zaidi ya madini hayo.
Katibu Mtendaji wa Chama cha Wachimbaji Madini Tanzania, Benjamin Mchwampaka, alisema maamuzi ya uwekezaji kati ya dhahabu na dola ya Marekani yanaathiriwa na mabadiliko ya soko.
“Mambo mengi huamua kama mtu awekeze kwenye dhahabu au dola, lakini hatimaye huangalia mwenendo wa soko,” alisema.
Mchambuzi huru wa masuala ya fedha, Oscar Mkude alisema dhahabu bado ni hifadhi ya thamani ambayo huimarika pale uwekezaji mwingine unapodhoofika.
“Dhahabu hutazamwa kama sehemu salama ya uwekezaji, na mara nyingi hupanda wakati uwekezaji mwingine hauendi vizuri. Dola inapodhoofika, wawekezaji huhamia kwenye dhahabu,” alisema.
Aliongeza kuwa hali hiyo hubadilika pia pale dola inapokuwa imara, ambapo husababisha watu kuuza dhahabu.
“Kwa sasa dola imeanza kuimarika. Dhahabu haitoi riba, na kutokana na kuongezeka kwa mapato ya hati fungani Marekani, wawekezaji wengi wanahamisha fedha zao huko. Hata hivyo, hali hii inaweza kuwa ya muda mfupi,” alisema.
Mkude alibainisha kuwa dhahabu imekuwa ikipanda tangu mapema 2025 lakini sasa inaonyesha dalili za kushuka kadri wawekezaji wanavyokusanya faida.
“Baada ya kufikia kilele, bei zimeanza kushuka na hivyo wawekezaji wanauza kabla hazijashuka zaidi,” alisema.
Aliongeza kuwa hali ya kutokuwa na uhakika katika masoko ya dunia pia inawafanya wawekezaji wengi kutunza fedha taslimu ili kubaki na ukwasi.
“Watu wengi wanapouza, ugavi unaongezeka sokoni na kusababisha bei kushuka,” alieleza.
Mkude alisema uamuzi wa Benki Kuu ya Tanzania ni wa busara na umefanyika kwa wakati muafaka.