Bwege azikiwa Kilwa, viongozi walivyomzungumzia

Dar es Salaam. Baadhi ya viongozi na wanasiasa wamemzungua aliyekuwa mbunge wa Kilwa Kusini, Selemani Bungara, maarufu Bwege wakisema alikuwa kiongozi aliyekuwa na dhamira ya kweli katika kuwatumikia wananchi bila kujali itikadi za vyama.

Mbali na hilo wamesema Bwege alikuwa na ujuzi wa kujenga hoja zinazowakabili wananchi na kuzisimamia kuona utekelezaji unafanyika hasa pale alipokuwa akiwasilisha hoja bungeni.

Hayo yameelezwa leo Jumanne, Machi 31, 2026 kwenye mazishi ya Bwege, yaliyofanyika Kilwa Kivinje mkoani Lindi na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kiserikali, kisiasa na wadau wengine wa demokrasia.

Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Mohammed Nyundo, amemzungumzia Bwege akisema alikuwa mtu ambaye hakuamini katika vyama pale suala la maendeleo linapojitokeza.

“Bwege aliamini katika dhamira ya kuwatumikia watu kupitia vyama. Historia yake amewahi kuwa mwanachama wa TLP, TADEA, CUF, na ACT-Wazalendo; na mwisho tunasikia alikuwa anaelekea Chadema,” amesema.

Amesema aliamini katika dhamira, alipoona jukwaa alilokuwamo linaenda kinyume na alichokiamini, alikuwa akihama na kwenda jukwaa lingine ili kutimiza malengo yake.

“Nilipokuja kuanza kazi Kilwa, mtu wa kwanza kunipokea alikuwa Bwege. Nilimtafuta kwa kuwa nilijua umaarufu wake katika siasa za Kilwa. Wakati wote alikuwa akizungumza kwa masilahi ya wananchi,” amesema.

Amesema baada ya mazungumzo na kumkaribisha, alimshauri aendelee kufanya kazi ya kuwatumikia wananchi kama njia ya kuenzi na kuendeleza dhamira yake, kwani hakuwahi kubagua katika kushirikiana na watu.

“Msiba wa Bwege utuunganishe kama ilivyokuwa leo tulipokuwa tunamsindikiza. Msiba wake utumike kutupatanisha; alikuwa binadamu, inawezekana alikuwa na mapungufu na pia alikuwa na mema,” amesema.

Amesema Bwege hakuwa tajiri wala na elimu ya juu, lakini hekima na busara zake zilikuwa nguzo muhimu katika kuwatumikia wananchi na kuchochea maendeleo yao.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Bara, John Heche, amesema wakati wote, Bwege alikuwa anapigania haki na maslahi ya wakulima wa zao la korosho, na aliwapenda wananchi wake kwa dhati, akitaka wapige hatua za maendeleo.

“Tunachoamini na kuahidi sisi Chadema ni kupigania yale yote ambayo Bwege alitamani yapatikane. Tunataka rasilimali za nchi zitumike kuwanufaisha wananchi wote,” amesema.

Amesema wanahitaji mtoto wa kawaida apate matibabu katika hospitali zilezile wanazotibiwa viongozi wakubwa, na pia wanataka watoto wasome katika shule bora ili wapate elimu nzuri.

“Tunataka mtoto akimaliza shule apate ajira kwa kuzingatia uwezo wake, si kwa kufahamiana na mtu fulani. Bwege, wakati wote, aliamini katika hilo, na Chadema tutaendelea kupigania,” amesema.

Amesema Bwege alikuwa maarufu nchi nzima; kila mmoja alimfahamu si kwa sababu alikuwa fisadi, bali kwa sababu aliwapenda Watanzania na nchi kwa ujumla.

“Tunataka nchi hii ibadilike. Tanzania ni tajiri; ina kila kitu, tuna madini mengi, yakiwemo hata yale yanayotumika kutengeneza mabomu. Tunapopigania mageuzi hatuna ugomvi wa ngumi, bali ni wa mawazo,” amesema.

Kwa upande wake kiongozi mstaafu wa ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe amesema Bwege aliingia Bungeni mwaka 2010 wakati yeye akiwa kwenye kipindi cha pili na wakati huo kulikuwa na vuguvugu la rasilimali.

“Alinifuata kunielezea kuhusu suala la Lindi kuwa na gesi ya Songosongo lakini hawanufaiki na ushuru wa huduma, akitaka wasomi tuangalie nini hiki”amesema.

Amesema baada ya kumueleza hivyo na kwa kuwa alikuwa kwenye kamati inayoshughulika na masuala hayo waliwaita Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), kuwahoji na ikabainika hawalipi ushuru huo Lindi.

“Ikabainika ushuru unaliwa Ilala wakati gesi inazalishwa Songosongo mkoani Lindi, baada ya kupata usaidizi wa Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali kwa mara ya kwanza Lindi ilianza kunufaika na ushuru wa huduma,” amesema.

Amesema Bwege hakuwa mbunge wa kwanza wa Kilwa, lakini alijua namna ya kuwatetea na kupigania maslahi yao kuona mageuzi yanapatikana.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Mirambo Yusuf amesema Bwege alikuwa mbunge mwenye elimu ya darasa la saba lakini amefanya makubwa kuliko wasomi wakubwa.

“Bwege alikuwa anasema ukweli na kuusimamia hata baada ya kuhama niliongea naye kumshawishi arudi lakini alikataa sikuwa na namna …. Utamfanya nini sasa kishaamua,”amesema Mirambo.

Bwege aliyewakilisha wananchi wa Kilwa Kusini Bungeni kwa miaka 10 kuanzia mwaka 2010 hadi 2020 kupitia CUF, alifariki dunia jana Jumatatu, Machi 30, 2026 katika Hospitali ya EM iliyopo Mji Mwema, Kigamboni, jijini Dar es Salaam, alipokuwa akisubiri kupatiwa huduma ya matibabu.