Katika kuadhimisha miaka 25 ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC), Kampasi ya Mbeya imefanya shughuli za kijamii, ikiwemo kutembelea na kutoa misaada kwa vituo viwili vya watoto yatima jijini Mbeya.
Katika ziara hiyo, TPSC Kampasi ya Mbeya imekabidhi mahitaji mbalimbali kwa ajili ya watoto hao, yakiwemo mchele, maharage, sabuni, juisi, mafuta ya kupikia, vitunguu, na mbuzi kwa ajili ya lishe na mahitaji ya kila siku.
“Chuo hiki kimeendelea kuwa chachu ya maendeleo kwa taifa letu kwa kutoa watumishi bora. Kila kinachofanywa hapa kinaonyesha dhamira ya kweli ya kuwahudumia wananchi na kujenga jamii yenye mshikamano,” alisema Mhe. Itanda.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kampasi ya Mbeya, Ndugu Saidy Nzagamba, alisema chuo hicho kimeamua kushiriki na kusaidia watoto yatima kama sehemu ya kuwajengea faraja na kuwahakikishia kuwa jamii inawajali.
“Tunatambua changamoto wanazokabiliana nazo watoto hawa, ndiyo maana tumeamua kuwa jirani nao na kuwagusa kwa upendo. Huu ni mwanzo wa dhamira yetu kuendelea kushiriki shughuli za kijamii katika siku zijazo,” alisema Nzagamba.




