EUBG yaadhimisha miaka 10, ikiimarisha biashara Tanzania

Dar es Salaam. Umoja wa Wafanyabiashara kutoka Ulaya nchini Tanzania umeadhimisha miaka 10 tangu kuanzishwa kwake, ukithibitisha mchango wake katika kuboresha mazingira ya biashara, kukuza uendelevu wa biashara na kuandaa majadiliano ya kimkakati kati ya Ulaya na Tanzania.

Maadhimisho hayo yaliyofanyika Machi 30,2026 jijini Dar es Salaam, yamewakutanisha wanachama wa EUBG, wawakilishi wa Umoja wa Ulaya (EU), viongozi wa Serikali, sekta binafsi, washirika wa maendeleo na wanadiplomasia. Tangu kuanzishwa kwake, taasisi hiyo imekuwa jukwaa muhimu la ushirikiano kati ya wafanyabiashara wa Ulaya na Tanzania, ikiwajumuisha zaidi ya kampuni 120. Kupitia ushirikiano wa karibu na wanachama wake pamoja na ubalozi za Ulaya, EUBG imechangia kuboresha mazungumzo, kujenga imani na kuendeleza masilahi ya pamoja ya kiuchumi.

Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania, Christine Grau, alisema ushirikiano kati ya Umoja wa Ulaya na sekta binafsi, hususan kupitia mkakati wa Global Gateway, ni nguzo muhimu ya kuhamasisha uwekezaji bora, endelevu na wenye tija unaochangia ukuaji wa uchumi huku ukizingatia ajira, masuala ya kijamii na mazingira.

EUBG pia inasaidia kutoa zana za kifedha na kiufundi kupitia Mfuko wa Ulaya wa Maendeleo Endelevu Plus, unaolenga kupunguza hatari za uwekezaji na kuongeza upatikanaji wa fedha, na hivyo kufungua fursa kwa sekta binafsi, kuongeza ushindani na kuchochea ukuaji endelevu. Katika muktadha wa Tanzania, Umoja wa Ulaya unaendelea kuzingatia maeneo yenye masilahi ya pamoja kama mabadiliko ya kidijitali, kilimo, madini, nishati jadidifu na miundombinu endelevu.

Mwenyekiti wa Bodi ya EUBG, Dennis Ott, alisema Tanzania inaendelea kuwakaribisha wawekezaji kutoka sehemu mbalimbali duniani, huku kampuni za Ulaya zikizingatia ubora, huduma, ulinzi wa mazingira, uadilifu na kukuza vipaji vya Watanzania. Mkurugenzi Mtendaji wa EUBG, Marloes Hamelink, alisisitiza kuwa taasisi hiyo inaendelea kuandaa matukio na majukwaa yanayowaunganisha wanachama, kubadilishana maarifa na kukuza biashara endelevu.

Wanachama wa Umoja wa Wafanyabiashara kutoka Ulaya (EUBG) nchini Tanzania, wakifurahia hafla ya kutimiza miaka 10 kwa umoja huo kwa mafanikio makubwa. Hafla hiyo imefanyika jijini Dar es Salaam, Machi 30, 2026. Picha na Mpigapicha Wetu.

Taasisi hiyo imeahidi kuendeleza ushirikiano, kuongeza ushawishi wake katika masuala ya sera na kuchangia ukuaji wa uchumi jumuishi na endelevu nchini Tanzania, huku ikithibitisha nafasi yake kama jukwaa muhimu la biashara na uwekezaji.