Dar es Salaam. Wadau wa elimu nchini wametaka kuandaliwa kwa sheria mpya itakayosimamia elimu nchini ambayo pamoja na mambo mengine, itaimarisha uwajibikaji, usimamizi, elimu jumuishi na mifumo ya tathmini ili kuendana na mabadiliko ya sera, mitaala na mahitaji ya soko la ajira.
Kwa sasa sekta hiyo inasimamiwa na Sheria ya Elimu ya mwaka 1978 ambayo inaelezwa kuwa imepitwa na wakati hivyo kunahitajika sheria mpya itakayoendana na hali ya sasa.
Mapendekezo hayo yaliwasilishwa hivi karibuni katika kikao cha mapitio ya Sheria ya Elimu, kilichowakutanisha wawakilishi wa Serikali na mashirika ya kiraia chini ya uratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET).
Mwenyekiti wa kamati ya mapitio ya sheria ya elimu, Profesa Saudin Mwakaje alisema kamati hiyo iliyafikia makundi mbalimbali ya wadau katika sekta ya elimu waliyotoa mapendekezo kadhaa ambayo yanaonesha kinachohitajika kufanyika sasa si maboresho bali kuandaliwa kwa sheria mpya.
Alisema kutokana na maboresho ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 toleo la 2023 ipo haja ya kuwa na sheria itakayoendana na yaliyomo kwenye sera hiyo na kufanikisha utekelezaji wa Dira ya 2050.
“Sheria ya sasa ina upungufu mwingi sasa wadau wamependekeza kutokana na upungufu huo sera tuliyonayo sasa na malengo ya shabaha za dira 2050 kuna haja ya kuwa na sheria mpya ya elimu na sio kuifanyia maboresho,” alisema Profesa Mwakaje.
Miongoni mwa maeneo yaliyopendekezwa ni uwajibikaji na usimamizi katika sekta ya elimu ambapo wadau hao wamebainisha kuwa sheria ya sasa, ina mianya inayosababisha ukosefu wa uwazi katika majukumu ya taasisi na mamlaka mbalimbali zinazosimamia elimu.
Eneo lingine lililopendekezwa na wadau kwenye kamati hiyo ni elimu jumuishi kupewa kipaumbele, ambapo msisitizo ni kuwekwa kwa misingi madhubuti ya elimu jumuishi ndani ya sheria.
“Pamoja na sera kuelekeza hakuna mtoto anayeachwa nyuma, bado utekelezaji unakabiliwa na changamoto kutokana na ukosefu wa vifungu vinavyolazimisha upatikanaji wa miundombinu rafiki kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu.
“Wadau wametaka sheria itamke bayana wajibu wa Serikali na wadau wengine katika kuhakikisha watoto wenye ulemavu, wanaotoka mazingira magumu na makundi mengine maalumu wanapata haki sawa ya elimu bora.
Aidha, walipendekeza kuwe na utaratibu wa kisheria wa kuhakikisha takwimu za watoto walio nje ya mfumo wa elimu zinakusanywa na kufanyiwa kazi kwa ufanisi.
Katika mazingira ya ufundishaji Mazingira ya ufundishaji walipendekeza maboresho ya sheria yanapaswa kuzingatia miundombinu ya shule, upatikanaji wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia, pamoja na rasilimali watu.
Eneo lingine lililopendekezwa kufanyiwa kazi kisheria ni kuanzishwa kwa mifumo bora ya tathmini na ufuatiliaji wa ubora wa elimu.
Wadau hawakuacha kugusia mabadiliko ya kijamii, kiuchumi na kiteknolojia yanayoendelea duniani ambapo mapendekezo ni sheria kutambua matumizi ya teknolojia katika ufundishaji, ikiwemo elimu kwa njia ya mtandao, ili kuweka msingi wa kisheria unaoendana na zama za kidijitali.
Akizungumza kwenye kikao hicho Mratibu wa Tenmet Martha Makala alisema mchakato huo umehusisha ukusanyaji wa maoni, mijadala ya kitaalamu, na uchambuzi wa kina wa changamoto zilizopo katika utekelezaji wa sheria ya sasa.
Alisema mapitio hayo yamelenga kuhakikisha kuwa Sheria ya Elimu inendana na mabadiliko ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, toleo la 2023, pamoja na maboresho ya mitalaa na nyaraka nyingine muhimu za elimu lengo likiwa ni kuweka uwiano kati ya sera, sheria na utekelezaji wake kwa vitendo.
Akizungumza katika kikao hicho, Naibu Waziri wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Wanu Hafidh Ameir aliwashukuru wadau kwa ushiriki wao, akisema uwepo wa sauti mbalimbali ni ishara ya uongozi unaosikiliza na kuthamini maoni ya wananchi katika maboresho ya sekta ya elimu.
“Serikali ina dhamira ya dhati kuhakikisha mageuzi ya elimu yanatekelezwa kikamilifu kama ilivyokusudiwa, hivyo nawasihi muendelee kutoa ushirikiano kwa Serikali ili kwa pamoja tuweze kupata matokeo chanya ya mageuzi haya,” alisema Wanu.
Mtoto mwenye mahitaji maalumu. Wadau wanataka Sheria ya Elimu itakayotoa msukumo mkubwa kwa watoto wenye mahitaji maalumu.
Sheria yenye mtazamo mpana
Mbali na hoja za uwajibikaji, elimu jumuishi na mifumo ya tathmini, wadau wengine wa elimu wametaka sheria ya elimu iwe na mtazamo mpana unaogusa misingi ya maadili, mwelekeo wa taifa katika lugha ya kufundishia, ustawi wa walimu, ulinzi wa mtoto na nafasi ya elimu ya ufundi katika uchumi wa viwanda.
Mhadhiri wa sera za elimu, Dk Methodius Kamugisha, anasema sheria mpya inapaswa kurejesha mjadala wa malezi kama sehemu kuu ya mfumo wa elimu.
“Kwa miaka mingi tumepima mafanikio ya elimu kwa kuangalia alama za mitihani. Lakini taifa linahitaji vijana wenye maadili, wanaojitambua na wanaoheshimu misingi ya jamii yao. Sheria mpya iweke wajibu kwa shule kujenga maadili, uzalendo na uwajibikaji wa kijamii,” anasema.
Anasema ipo haja kwa shule kupewa mwongozo wa kisheria wa kuendesha programu za malezi, ushauri nasaha na uraia, badala ya kuziacha kama shughuli za hiari.
Eneo lingine lililoguswa ni matumizi ya lugha ambapo Dk Kamugisha anasema mjadala wa lugha ya kufundishia haupaswi kuachwa kwenye sera pekee, bali uwekwe wazi ndani ya sheria.
“Kumekuwa na mkanganyiko wa muda mrefu kuhusu lugha ya kufundishia kati ya Kiswahili na Kiingereza katika ngazi mbalimbali. Sheria mpya itoe mwelekeo thabiti, ili walimu, wanafunzi na wazazi wajue taifa linaelekea wapi,” anasema.
Anaongeza kuwa uwazi huo utasaidia kuandaa walimu, vitabu na miundombinu ya kujifunzia mapema badala ya kufanya mabadiliko ya ghafla.
Kwa upande wa usalama wa watoto, Mkurugenzi wa Shirika la Watoto na Elimu, Daniel Mushi, anasema sheria mpya inapaswa kuweka viwango vya lazima vya ulinzi wa mtoto katika kila shule.
“Matukio ya ukatili, unyanyasaji na hata ajali za miundombinu yamekuwa yakiripotiwa. Sheria itamke wazi kuwa kila shule iwe na sera ya ulinzi wa mtoto, mfumo wa kuripoti matukio na adhabu kali kwa watakaokiuka,” anaeleza.
Anasema ulinzi wa mtoto unapaswa kuwa sehemu ya leseni ya uendeshaji wa shule, iwe ni ya Serikali au binafsi.
Asha Kiwale ambaye ni mwalimu wa sekondari, anapendekeza sheria mpya ifafanue mamlaka ya mwalimu darasani na shuleni.
“Kuna sintofahamu kuhusu nidhamu. Wakati mwingine mwalimu akichukua hatua za kinidhamu anakumbana na lawama au vitisho. Sheria mpya iweke mizania kati ya haki za mwanafunzi na mamlaka ya mwalimu,” anasema.
Anaongeza kuwa bila nidhamu na heshima kwa taaluma ya ualimu, ubora wa elimu utabaki kuwa changamoto.
Kwa upande wake, Peter Lema ambaye ni mdau wa elimu ya ufundi anasema sheria mpya inapaswa kuipa kipaumbele elimu ya ufundi na ujuzi wa kazi.
“Elimu ya ufundi isiwe chaguo la mwisho kwa waliofeli. Sheria itambue rasmi usawa wa thamani kati ya elimu ya kitaaluma na ya ufundi, na iweke motisha za kodi au ruzuku kwa wawekezaji katika vyuo vya stadi,” anasema.
Anasema hilo litasaidia kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana na kuandaa nguvu kazi yenye ujuzi unaohitajika katika soko.