Hizi hapa fursa 300 za ajira Saudi Arabia, mshahara Sh7 milioni

Dodoma. Serikali ya Tanzania imetangaza fursa mpya za ajira 300 kwa wauguzi nchini Saudi Arabia, ambapo wanawake wa Kitanzania wenye sifa wakihimizwa kujitokeza kuwania nafasi hizo.

Tangazo hilo limetolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, ikieleza kuwa nafasi hizo zinalenga kupanua ajira za Watanzania nje ya nchi na kutoa fursa ya kipato pamoja na uzoefu wa kimataifa kwa wataalamu wa afya.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ajira hizo zimetolewa na Wizara ya Afya ya Saudi Arabia kwa kushirikiana na kampuni ya Dalba Consulting Group, ambapo watakaofanikiwa watasaini mikataba ya miaka miwili ikiwa na kipengele cha kuongezwa kulingana na utendaji kazi.

Waombaji wanatakiwa kuwa wanawake wenye umri wa miaka 23 hadi 45, wenye shahada ya uuguzi au zaidi, pamoja na leseni halali ya taaluma kutoka Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania (TNMC). Pia, awe na uzoefu wa kazi usiopungua miaka miwili.

Mbali na ajira hizo, tangazo linaonyesha vivutio vinavyolenga kuwavutia waombaji, ikiwamo mshahara wa kati ya Sh3 milioni hadi Sh7 milioni kwa mwezi.

Aidha, mwajiri atagharamia huduma za matibabu, malazi, chakula pamoja na tiketi za safari ya kwenda na kurudi.

Waombaji wametakiwa kuwasilisha maombi yao kwa njia ya barua pepe na baadaye kujisajili katika mfumo wa ajira wa Serikali kupitia Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma.

Mwisho wa kutuma maombi ni Aprili 12, 2026.

Serikali imesema kuwa hatua hiyo ni kupunguza changamoto ya ajira nchini kwa kufungua milango ya ajira nje, sambamba na kuwajengea Watanzania uwezo wa kushindana katika soko la ajira la kimataifa.