HOSPITALI YA MKAPA YAWEKA HISTORIA MPYA KATIKA MATIBABU YA FIGO NA ULOTO

………..

Na Carlos Claudio, Dodoma

Hospitali ya Benjamin Mkapa imeanza rasmi maandalizi ya maadhimisho ya miaka 10 tangu kuanzishwa kwake, sambamba na uzinduzi wa harambee maalum ya kuchangisha fedha kwa ajili ya kuboresha huduma za matibabu ya upandikizaji uloto kwa watoto wenye ugonjwa wa seli mundu pamoja na upandikizaji wa figo.

Akizungumza leo Machi 31, 2026 jijini Dodoma, Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Profesa Abel Makubi, alisema hospitali hiyo imeendelea kuwa tegemeo kubwa kwa wananchi, ikihudumia takribani watu milioni 10 kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania pamoja na wagonjwa kutoka nje ya nchi. Alieleza kuwa hali hiyo imeifanya hospitali hiyo kuwa moja ya vituo muhimu vya tiba utalii nchini.

Profesa Makubi alifafanua kuwa kupitia harambee hiyo, hospitali inalenga kukusanya jumla ya shilingi bilioni 7 ndani ya kipindi cha miaka miwili, fedha zitakazosaidia kugharamia matibabu kwa wagonjwa 100. Kati yao, watoto 50 wanatarajiwa kufaidika na matibabu ya seli mundu kupitia upandikizaji uloto, huku wagonjwa wengine 50 wakipatiwa huduma ya upandikizaji figo.

Alisisitiza kuwa hatua ya kuimarisha huduma hizo ndani ya nchi imelenga kupunguza gharama kubwa ambazo wagonjwa wengi walilazimika kuzitumia kufuata matibabu nje ya Tanzania, na hivyo kuongeza upatikanaji wa huduma hizo kwa wananchi wa kipato cha kati na cha chini.

Kwa upande wake, mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa NHIF, Dkt. Devid Raymond, alisema mfuko huo unaendelea kuboresha huduma zake kwa kubuni vifurushi vipya vya bima vinavyolenga kuwafikia Watanzania wengi zaidi.

Aliongeza kuwa licha ya huduma za upandikizaji figo na uloto kutogharamiwa moja kwa moja na NHIF kwa sasa, serikali imeendelea kuchukua hatua za kusaidia huduma hizo ili kupunguza mzigo kwa wagonjwa na familia zao.

Harambee hiyo inatarajiwa kufanyika Mei 8, 2026 jijini Dodoma, ikiwa ni sehemu ya kilele cha maadhimisho hayo ya miaka 10 ya hospitali hiyo. Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Maadhimisho hayo yanatarajiwa kuwa chachu ya kuimarisha huduma za afya nchini, hasa katika matibabu ya magonjwa sugu yanayohitaji teknolojia ya hali ya juu, huku yakilenga kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora na za kisasa kwa gharama nafuu ndani ya nchi.