Mary Mugitu na ndoto ya biashara iliyogeuka tumaini kwa wanawake

Arusha. Katika nyakati hizi ambazo dunia ya biashara imejikita zaidi katika ushindani na faida, simulizi ya Mary Mugitu inabeba sura tofauti –huruma, maono na dhamira ya kuleta mabadiliko katika familia na Taifa kwa ujumla.

Mugitu akizungumza na Mwananchi hivi karibuni, amesema kwake biashara haikuwa njia ya kutafuta kipato pekee, bali ilikuwa jibu la changamoto alizoziona tangu utotoni.

Anasema changamoto hizo alizibaini hususan kwa wanawake waliokuwa wakifanya kazi kwa bidii kubwa, lakini matunda ya kazi zao hayakuwa yakionekana bayana.

Mugitu aliyekulia katika Kijiji cha Mafinga, mkoani Iringa, anasema huko alishuhudia maisha ya kila siku ya wanawake waliotengeneza bidhaa za mikono kwa ustadi mkubwa.

Anasema bidhaa hizo ni pamoja na vikapu, vyombo vya kuhifadhia nafaka na mapambo ya asili, ambavyo vilikuwa sehemu ya maisha ya kawaida kwao.

Hata hivyo, anasema nyuma ya uzuri na ubunifu wa bidhaa hizo, kulikuwa na simulizi kimya ya umasikini na kutotambuliwa kwa thamani ya kazi hizo.

“Nilikuwa naona kabisa akina mama wanajituma sana, wanatumia ubunifu mkubwa, lakini maisha yao hayabadiliki. Hapo ndipo wazo la biashara lilipoanza kuniijia, kwamba inawezekana kufanya kitu kitakachobadilisha maisha ya hawa wanawake,” anasema Mugitu.

Ndoto hiyo ilianza kama wazo la ndani, lakini baadaye ikawa dira ya maisha yake. Baada ya kuhitimu Shahada ya Utawala na Biashara, Mugitu alifanya kazi katika taasisi mbalimbali na alihitimisha safari yake ya kuajiriwa katika mfuko wa Serikali wa GEPF, ambako alifanya kazi kama Ofisa Masoko jijini Arusha.

Hata hivyo, anasema licha ya kuwa na kazi yenye uhakika, moyo wake uliendelea kuvutwa na ndoto yake ya kuleta mabadiliko kwa wanawake wa kipato cha chini.

“Nilijua nimeajiriwa, lakini sikujiona nitaendelea hivyo maisha yangu yote. Nilikuwa na ndoto ya kujiajiri na zaidi ya yote, nilitaka kuona wanawake wale niliokua nao wakibadilisha maisha yao,” anasema.

Hatimaye mwaka 2021, alichukua uamuzi mgumu wa kuacha ajira rasmi na kuanzisha biashara yake aliyoipatia jina la Almega Brands.

 “Huo ukawa mwanzo wa safari yangu mpya ya maisha ya biashara iliyohitaji uthubutu, uvumilivu na imani kubwa katika kile nilichokuwa ninakifanya,” anasema Mugitu.

Kupitia Almega Brands, Mugitu anasema ameanzisha biashara ya kijamii inayolenga kuwawezesha wanawake kiuchumi kwa kuwapatia soko la uhakika la bidhaa zao za mikono.

“Tofauti na biashara nyingi, Almega haitegemei malighafi kutoka viwandani au nje ya nchi, bali hununua moja kwa moja kutoka kwa wanawake wanaozalisha bidhaa hizo vijijini,” amesema.

Akifanya kazi kwa karibu na wanawake kutoka mikoa ya Iringa na Njombe, Mugitu amejenga mtandao wa wazalishaji wa bidhaa mbalimbali za asili, hususan vikapu vinavyotengenezwa kwa majani ya porini yaotayo kando ya mito. Kadiri muda unavyokwenda, mtandao huo unakua na kuhusisha pia vikundi vya wanawake wanaotengeneza bidhaa za udongo na wanaofuma vitambaa kwa kutumia mbinu za jadi.

Mugitu anasema hivi sasa zaidi ya wanawake 170 wanashirikiana na Almega Brands katika utengenezaji wa vikapu, huku wengine wakijihusisha na bidhaa za ufinyanzi wa udongo na vitambaa.

Anasema kupitia ushirikiano huo, wanawake hao wamepata fursa ya kupata kipato cha uhakika na kuboresha maisha yao kwa kiwango kikubwa.

Hata hivyo, anasema mafanikio ya Almega Brands hayakuja kwa kuuza bidhaa hizo kama zilivyo. Mugitu anasema hatua muhimu zaidi ilikuwa kuongeza thamani ya bidhaa hizo ili ziweze kushindana katika soko la kisasa.

“Tunachofanya ni kuboresha bidhaa hizi kwa ubunifu wa kisasa bila kupoteza asili yake. Tunatumia malighafi kama ngozi, shanga, vitenge, batiki na hata magamba ya konokono kuzibadilisha kuwa bidhaa zinazokidhi mahitaji ya soko la ndani na kimataifa,” anasema.

Ansema matokeo ya juhudi hizo yameonekana wazi. Hivi sasa bidhaa za Almega zinapatikana katika masoko ya kimataifa, ikiwemo nchi za Uingereza, Marekani na Ujerumani.

Aidha, bidhaa hizo zinauzwa katika maduka ya zawadi pamoja na maeneo ya utalii, ambapo huvutia wageni wanaotafuta bidhaa zenye utambulisho wa Kiafrika.

Kwa mujibu wa Mugitu, sekta ya utalii imekuwa mhimili mkubwa wa mafanikio ya biashara yake, ikichangia takribani asilimia 85 ya mauzo yote. Bidhaa zake zinapatikana katika hoteli na nyumba za kulala wageni zilizopo katika maeneo ya kitalii kama Ngorongoro, Serengeti, Manyara na Arusha.

Watalii wanapenda sana bidhaa za mikono, lakini zaidi wanavutwa na hadithi iliyo nyuma ya bidhaa hiyo, anasema.

“Ukimweleza kuwa kikapu kimetengenezwa kwa siku kadhaa na mama anayelea familia peke yake, wanaguswa na wengi hununua si kwa matumizi tu bali kwa nia ya ‘kuwaungusha’,” anasema.

Mbali na soko la utalii, Mugitu pia ametumia kwa ustadi mkubwa mitandao ya kijamii kupanua biashara yake. Kupitia jukwaa la Instagram, ameweza kuwafikia wateja kutoka sehemu mbalimbali duniani.

“Asilimia karibu 98 ya wateja wangu wa nje nimewapata kupitia mitandao ya kijamii. Lakini mafanikio haya hayaji bila mkakati, lazima ujue unataka nini na unataka kufahamika vipi,” anasisitiza.

Anabainisha kuwa pamoja na uuzaji wa bidhaa, Almega Brabds pia hujikita katika kuhakikisha biadhaa zina ubora wa kimataifa katika ufungashaji, utambulisho wa bidhaa, pamoja na kutoa mafunzo na uwezeshaji kwa wanawake wanaoshirikiana nao.

Kwa upande wa mazingira, Mugitu anasema matumizi ya malighafi za asili yana mchango mkubwa katika kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi, kwa sababu bidhaa nyingi hutengenezwa kwa rasilimali zinazoweza kurejelewa na hivyo kupunguza uzalishaji wa taka.

Licha ya mafanikio hayo, Mugitu bado ana ndoto kubwa zaidi. Anapanga kuanzisha kiwanda kitakachozalisha bidhaa mbalimbali kwa kutumia mchanganyiko wa teknolojia za jadi na za kisasa.

Bidhaa hizo zitajumuisha mashuka, napkins, robs na table mats, huku lengo likiwa ni kupanua wigo wa soko na kuwafikia wanawake wengi zaidi.

“Natamani kuona wanawake wengi zaidi wakinufaika na fursa hii. Hii si biashara tu, ni maisha ya watu. Tunapoboresha bidhaa, tunaboresha maisha yao,” anasema.

Kwa wanawake wanaotamani kuingia katika ujasiriamali, Mugitu anashauri wanawake wanapaswa kujitambua, waweke malengo na wasimamie ndoto zao kwa uthubutu na uvumilivu.