Mfumo wa NEST ulivyookoa fedha taasisi za umma

Dar es Salaam. Juhudi za Tanzania kuhamisha ununuzi wa umma kidijitali zimeanza kuonyesha matokeo baada ya taasisi kuokoa Sh13.3 bilioni ndani ya mwaka mmoja na Sh35 bilioni ndani ya miaka miwili.

Mafanikio hayo yanatokana na Mfumo wa Taifa wa Ununuzi wa Kielektroniki (NEST) ulioboresha zabuni, kuongeza ushindani na uwazi.

Kwa mujibu wa tathmini ya Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) ya Machi 11, 2026, zaidi ya zabuni 219,000 zilichakatwa kupitia NEST, zikiokoa zaidi ya Sh27.64 bilioni za karatasi na wino.

Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Denis Simba amesema utii wa sheria umeongezeka kutoka asilimia 76 hadi 79 mwaka 2024/25 kutokana na utekelezaji wa Sheria ya Ununuzi wa Umma ya 2023 na matumizi ya NEST.

Amesema pia zabuni ziliongezeka hadi karibu 100,000 kutoka 53,221 na wazabuni kuongezeka kutoka 11,564 hadi 22,913, ishara ya uwazi na ushiriki mpana.

Mtaalamu wa ununuzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Oliva Mwambafula alisema mifumo ya kidijitali inaongeza uwajibikaji na kupunguza mianya ya ubadhirifu.

Mhadhiri Msaidizi wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Alfred Assenga alisema ushirikishwaji wa taasisi za chini kama shule na vituo vya afya unaimarisha utii wa sheria katika ngazi zote.

Kwa sasa zaidi ya taasisi 6,900 zinatumia NEST, huku moduli za mikataba, malalamiko na ununuzi wa ndani zikiimarisha usimamizi.

Dk Isac Safari wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine alisema hatua hiyo inaongeza ufanisi wa bajeti na utoaji wa huduma.

Mchumi, Samson Rutashobya alisema NEST inatoa fursa kwa vijana na wanawake na kuchochea uzalishaji wa ndani.

Hata hivyo, PPRA imebaini taasisi 756 kati ya 943 hazikutenga asilimia 30 kwa makundi maalumu, huku malipo ya kazi zisizotekelezwa yakifikia Sh11.6 bilioni.

Dk Michael Mollel wa Sartify alisema teknolojia kama akili bandia na uchambuzi wa data inaweza kusaidia kugundua mapungufu mapema.

Mwaka 2024/25, kati ya Sh14.5 trilioni za ununuzi, Sh9.1 trilioni zilitolewa kwa makundi maalumu sawa na asilimia 62.

Ukaguzi wa PPRA kwa mikataba 481 ulionyesha asilimia 58 ilikidhi malengo, asilimia 34 haikukidhi kikamilifu na asilimia nane ilifanya vibaya.

“Marekebisho haya yanalenga kuimarisha uwazi, uwajibikaji na ufanisi wa matumizi ya fedha za umma kupitia NEST,” alisema Simba.