Mtatiro atoa siku nne utatuzi tozo kwa wachimbaji Shinyanga

Shinyanga. Malalamiko ya wachimbaji wadogo wa madini katika mgodi wa Mwakitolyo yamechochea hatua za haraka kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro, ambaye ameitaka halmashauri ya wilaya hiyo kukutana na wadau hao ndani ya siku nne ili kutafuta suluhisho la mgogoro wa tozo.

Wachimbaji hao wamelalamikia kutozwa Sh200,000 kwa kila gari linalobeba mawe kutoka mgodini, wakisema kiwango hicho kinaongeza mzigo wa gharama katika shughuli zao.

Wakizungumza katika kikao cha kusikiliza kero zao Machi 31, 2026, wamesema tayari wanakabiliwa na gharama kubwa za uzalishaji, zikiwemo tozo za huduma, mrabaha, ukaguzi na michango mingine ya kijamii.

Mchimbaji mdogo, Alphonce Magesa, amesema wingi wa tozo unadhoofisha shughuli zao, akibainisha kuwa hata gharama za uendeshaji mgodi ni kubwa kutokana na ubora mdogo wa mawe.

Mchimbaji mdogo wa mgodi wa madini Mwakitolyo Alphonce Magesa akiwasilisha malalamiko ya wachimbaji juu ya tozo mpya iliyowekwa na Halmashauri Sh200,000 kwa kila gari linalotoka mgodini likiwa limebeba mawe

“Mazingira ya kazi ni magumu, tunatumia gharama kubwa kuendesha mgodi. Tozo hizi zinatukatisha tamaa na zinaweza kuathiri uzalishaji,” amesema.

Kwa nyakati tofauti, wachimbaji hao wameiomba halmashauri kupitia upya tozo hiyo ili kupunguza mzigo wa gharama na kuweka mazingira rafiki ya uzalishaji.

Mwenyekiti wa wachimbaji wadogo Wilaya ya Shinyanga, Elias Amos, amesema wamekuwa wakilalamikia suala hilo kwa muda bila mafanikio, hivyo kuomba mamlaka za juu kuingilia kati.

Kwa upande wake, mchimbaji Alice Kianila, aliyewakilisha wachimbaji wanawake, amesisitiza umuhimu wa kupata suluhisho la kudumu litakalopunguza malalamiko na kuboresha mazingira ya kazi.

Akijibu hoja hizo, Mtatiro amesema tozo hiyo ilianzishwa na Kamati ya Fedha na Mipango Septemba 22, 2022 na kuidhinishwa na Baraza la Madiwani, lakini utekelezaji wake umeibua changamoto kwa wadau.

Mchimbaji mdogo wa mgodi wa madini Mwakitolyo Alice Kianila   akiwasilisha malalamiko ya wachimbaji wanawake juu ya tozo mpya iliyowekwa na Halmashauri Sh200,000 kwa kila gari linalotoka mgodini likiwa limebeba mawe.

Ameagiza halmashauri kufanya majadiliano ya kina na wachimbaji hao ili kupitia upya tozo hiyo na kuhakikisha suluhisho linapatikana kwa haraka.

“Lazima kuwe na uwiano kati ya mapato ya halmashauri na uwezo wa wachimbaji. Ndani ya siku nne nataka suala hili liwe limejadiliwa na kufanyiwa kazi,” amesema Mtatiro.