Mwanamke Atoroka Kwenye Gari la Polisi Kupitia Dirisha Akiwa na Pingu

Tukio la kushangaza limewaacha wengi midomo wazi baada ya mwanamke mmoja aliyekuwa amefungwa pingu kufanikiwa kutoroka ndani ya gari la polisi kwa njia ya dirisha, kisha kutimua mbio bila askari kugundua mara moja.

Katika video inayosambaa mtandaoni, mwanamke huyo mwenye nywele za rangi ya dhahabu anaonekana akichungulia nje kupitia dirisha la nyuma lililokuwa limefunguliwa nusu, kana kwamba anahakikisha hakuna anayemwangalia. Kwa ustadi wa ajabu, anajikamua na kupenyeza mwili wake kupitia uwazi mdogo wa dirisha hilo licha ya mikono yake kuwa imefungwa nyuma kwa pingu.

Baada ya kufanikiwa kutoka, anashuka kwa ustadi bila kuanguka na kuanza kukimbia kwa kasi barabarani. Wakati huo, maafisa wa polisi waliokuwa karibu wanaonekana kuwa bize wakikagua gari lingine jeupe lililokuwa limeegeshwa jirani.

Ni baada ya muda mfupi ndipo askari mmoja alipogonga dirisha la nyuma la gari la polisi na kugundua mtuhumiwa ametoweka, hali iliyosababisha msako mkali kuanza mara moja.

Kwa mujibu wa taarifa, mwanamke huyo alikamatwa siku ya Jumamosi mchana katika eneo la biashara lililotelekezwa huko Muskegon Heights. Polisi walipofika eneo hilo walimtambua dereva wa gari lililokuwa na shaka, lakini walishindwa kumtambua abiria mwanamke hadi walipotumia kifaa cha alama za vidole na kugundua alikuwa na kosa la kukiuka masharti ya parole.

Baada ya hapo, alifungwa pingu na kuwekwa ndani ya gari la doria hatua iliyosababisha tukio hilo la kutoroka muda mfupi baadaye.

Taarifa zinaeleza kuwa hadi kufikia Jumatatu jioni, bado alikuwa hajakamatwa tena. Polisi pia wanahisi huenda anahusishwa na jaribio la uvamizi wa nyumba lililoripotiwa chini ya saa moja baada ya kutoroka kwake.

Kwa sasa, anakabiliwa na makosa mapya ikiwemo kutoroka chini ya ulinzi wa polisi, uvamizi wa nyumba (felony), pamoja na makosa mengine kama wizi na kuvunja na kuingia.

Video hiyo imeibua hisia kali mtandaoni, huku wengi wakishangazwa na ustadi wake. Baadhi walieleza kuwa kitendo hicho kinafanana na “uchawi,” huku wengine wakidai huenda si mara yake ya kwanza kufanya jambo la aina hiyo.