Mwizi wa Mtoto Ahukumiwa Jela Mwaka Mmoja, AJitetea Hawezi Kubeba Ujauzito

Bakari Mahundu
March 31, 2026
0 Comments

Mahakama ya Wilaya ya Sengerema, mkoani Mwanza, imemhukumu Novina Yoel Kuboja (23), mkulima na mkazi wa Buchosa, kutumikia kifungo cha mwaka mmoja jela baada ya kupatikana na hatia ya kumuiba mtoto wa kiume mwenye umri wa miezi mitatu (jina limehifadhiwa kwa sababu za kisheria).
Hukumu hiyo imetolewa leo Machi 30, 2026, na Hakimu Mfawidhi, Mhe. Evod Kisoka, baada ya mshtakiwa kukiri      kosa hilo na hivyo kutaka kutoisumbua mahakama. Alipatikana na hatia ya kosa la kuiba mtoto kinyume na kifungu cha 169(1)(a) cha Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, marejeo ya mwaka 2023.
Awali, Wakili wa Serikali, Rivana Kasinisala, alisoma shtaka hilo katika kesi ya jinai namba 6895/2026, akieleza kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Machi 11, 2026, katika kijiji cha Nyamatemele, kata ya Nyehunge, wilayani Sengerema.                                                                                                                                                                                        Katika utetezi wake, mshtakiwa aliiomba mahakama impunguzie adhabu akidai kuwa alichukua mtoto huyo kwa lengo la kumlea kutokana na kushindwa kupata mtoto wake mwenyewe.
Hata hivyo, upande wa mashtaka ulipinga maelezo hayo ukisisitiza kuwa kitendo hicho ni cha kikatili na kinyume cha sheria, na kuiomba mahakama kutoa adhabu kali ili kukomesha vitendo vya wizi wa watoto.
Akitoa hukumu, Mhe. Kisoka alisema mahakama haina mbadala wa adhabu hiyo kwa mujibu wa sheria husika, hivyo akaamuru mshtakiwa kutumikia kifungo cha mwaka mmoja gerezani.