*Ni ujenzi uliogharimu Sh.bilioni 25,changamoto ya kukatika umeme imebaki historia
Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Ifakara
MRADI wa ujenzi wa Kituo cha kupoza umeme cha Ifakara ambacho kimejengwa na Serikali kupitia Wakala wa Umeme Vijijini(REA) kwa gharama ya Sh.bilioni 25 kimewezesha kumaliza changamoto ya kukatika umeme mara kwa mara katika Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro.
Kwa sasa kituo hicho kinazalisha umeme wa megawati 18 na kati hizo ambazo zinatimika ni megawati 7 na hivyo kuwa na ziada ya megawati 11 ambapo wananchi,taasisi za umma na binafsi zimeondokana kabisa na umeme wenye mashaka.
Umeme wa uhakika ambao REA wameufanikisha kupitia kituo hicho ambacho no moja ya kituo kikubwa cha kupoza na kuzalisha umeme kujengwa na wakala huo kimewafanya wananchi wa Wilaya hiyo wapato milioni moja kumshukuru Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kumaliza changamoto ya umeme katika Wilaya hiyo.
Akizungumza mbele ya Wahariri ambao ni Wanachama wa Jukwaa la Wahariri Tanzania(TEF) walioko katika ziara ya kutembelea miradi ya REA, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Dunstan Kyoba, amesema kituo hicho kimeondoa changamoto ya kukatika kwa umeme na kazi iloyobakia kwa sasa ni kuhamasisha watu kwenda kuwekeza kwani umeme ni wa uhakika.
Amesema kabla ya kujengwa kwa kituo hicho wananchi kwa muda mrefu walikuwa wakiteseka kwa umeme kuwa wa kukatikatikq lakini Rais Dk.Samia kwa maelekezo yake aliielekeza REA kujenga kituo hicho ambacho kimegharimu Sh.bilioni 25 hatua ambayo imewezesha kuwa na umeme wa uhakika.
“Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ilitoa takribani shilingi bilioni 25 kugharamia ujenzi wa kituo hicho, hatua iliyoongeza upatikanaji wa umeme kutoka megawati 3 hadi megawati 7 pamoja na sasa kuwepo kwa ziada ya megawati 11.
“Upatikanaji wa umeme wa uhakika umefungua fursa za uwekezaji katika sekta mbalimbali ikiwemo viwanda, kilimo, hoteli na huduma za afya,” amesema na kusisitiza kwa kazi nzuri ya REA katika Wilaya hiyo hivi sasa wametoa ombi kituo hicho kiitwe kituo cha kupoza umeme cha Samia kama sehemu ya kutambua jitihada zake katika kuhakikisha wananchi wanakuwa na umeme wa uhakika.
Hata hivyo ametoa rai kwa wawekezaji kuwekeza katika Wilaya ya Kilombero na ukanda wa Morogoro Kusini unaojumuisha wilaya za Kilombero, Ulanga na Malinyi huku akiweka wazi Wilaya hiyo imebarikiwa kuwa na kila aina ya fursa ikiongozwa na kilimo pamoja na utalii.
Awali Meneja wa Usimamizi wa Miradi kutoka REA, Mhandisi Deogratius Nagu, amesema mradi huo umegharimu takribani Sh. bilioni 25, ukihusisha pia ujenzi wa njia za kusafirisha umeme za msongo wa kilovolti 33 zenye urefu wa kilometa 70 pamoja na huduma za ushauri elekezi.
“Ujenzi wa Kituo hiki umetumia teknolojia ya kosasa kutoka mataifa matatu ikiwemo transfoma kutoka Bulgaria, mifumo ya udhibiti na ulinzi kutoka Hispania pamoja na mifumo ya switching kutoka Ujerumani,”amesema Mhandisi Nagu alipokuwa akitoa taarifa ya kituo hicho kwa wahariri hao wakiongozwa na Mwenyekiti wa TEF Deodatus Balile.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa TEF, Balile ametoa pongezi kwa REA kwa kazi kubwa wanayofanya nchini ya kuhakikisha nchi inakuwa na umeme wa uhakika na Kamba kituo hicho cha kupoza umeme Ifakara unaonesha matumizi sahihi ya rasilimali za umma na mchango wa REA katika kusambaza umeme vijijini.
Balile ameongeza kwamba ongezeko la matumizi ya umeme hadi kufikia megawati saba ni ishara ya ukuaji wa shughuli za kiuchumi na maendeleo ya taifa kwa ujumla.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Kilimo Ifakara, Setina Ngailo, amesema shule yao ni moja ya wanafuika wa umeme wa REA na awali walikumbwa na changamoto ya kukatika kwa umeme hasa kipindi cha masika, hali iliyokuwa ikiathiri upatikanaji wa maji na mwanga shuleni.
“Kwa sasa changamoto hiyo imeondoka kabisa na tunapata huduma ya umeme muda wote.Umeme wa uhakika umewezesha wanafunzi kusoma bila kupata usumbufu ya kukosa umeme
Wakati huo huo Msimamizi wa Hospitali ya Kansa ya Good Samaritan, Father Charles Masawe, amesema hapo awali walilazimika kutumia jenereta kutokana na umeme mdogo, hali iliyokuwa inaongeza gharama za uendeshaji.“Kwa sasa tunaendesha vifaa tiba kwa ufanisi zaidi kutokana na upatikanaji wa umeme wa uhakika,” alisema.
Kwa upande wake Meneja wa Kiwanda cha Kukoboa Mpunga cha Bezelengule, Enos Machumu, amesema uzalishaji umeongezeka kutoka tani 3 hadi tani 22 kwa siku kufuatia kuimarika kwa huduma ya umeme, huku pia wateja waliokuwa wameondoka wakirejea.
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)

