Dodoma. Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Benjamini Mkapa (BMH) imepanga kufanya harambee ya kusaidia wagonjwa 100 wanaohitaji upandikizaji wa uloto kwa watoto wenye ugonjwa wa seli mundu na upandikizaji wa figo kwa watu wazima.
Akizungumza na waandishi wa habari Jumanne, Machi 31, 2026, Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, Profesa Abel Makubi, amesema harambee hiyo itafanyika Mei 8, 2026 jijini Dodoma, ikishirikisha wadau mbalimbali ikiwemo taasisi za umma, sekta binafsi, wadau wa kimataifa na wananchi binafsi.
Hafla hiyo pia itaambatana na maadhimisho ya miaka 10 ya kuanzishwa kwa hospitali hiyo, ambayo kwa miaka saba imekuwa kitovu cha matibabu ya kibingwa nchini. Mgeni rasmi katika hafla hiyo anatarajiwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan.
Profesa Makubi amesema kuwa matatizo ya seli mundu na figo ni makubwa nchini, akibainisha kuwa takribani watoto 12,000 huzaliwa kila mwaka na ugonjwa wa seli mundu, huku wagonjwa wapatao 100 wakihitaji upandikizaji wa figo. Ili watoto hao waweze kupona, wanahitaji upandikizaji wa uloto, ambao gharama yake ni kubwa mno. “Upandikizaji wa uloto kwa mtoto mmoja ni Sh75 milioni nchini na kati ya Sh120 hadi Sh150 milioni nje ya nchi. Kwa mgonjwa wa figo, gharama ya upandikizaji ni Sh40 milioni kwa mtu mmoja,” amesema Profesa Makubi.
Ameongeza kuwa Rais Samia amewahi kugharamia matibabu ya watoto wenye seli mundu na hata kuwatazama wagonjwa hao hospitalini, jambo lilichochea juhudi za kuendelea kusaidia wagonjwa wengine. “Harambee hii itasaidia kuwatibu ndugu zetu wenye matatizo ya figo na seli mundu ambao hawana uwezo wa kugharamia matibabu,” ameongeza.
Hospitali hiyo tayari imefanikiwa kufanya upandikizaji wa figo kwa wagonjwa 55, ambapo wote wamepona isipokuwa mmoja aliyekumbana na changamoto nyingine zisizohusiana na upandikizaji. Aidha, watoto 28 kutoka ndani na nje ya nchi wamefanyiwa upandikizaji wa uloto na kupona ugonjwa wa seli mundu kwa gharama ya jumla ya Sh1.9 bilioni.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Dk David Mwenisano, amesema tatizo la figo nchini ni kubwa huku wagonjwa wengi wakiendelea na uchujaji wa damu licha ya kuhitaji upandikizaji wa figo ambao ndiyo tiba kamili.
Amesema gharama za uchujaji wa damu ni kubwa, akitoa mfano wa mtoto anayelipia bima ya afya Sh50,400 kwa mwaka, lakini akipata tatizo la figo hulazimika kutumia hadi Sh28 milioni kwa mwaka, sawa na michango ya watoto 571.
“Serikali imeanzisha mpango wa bima ya afya kwa wote, huku kaya maskini takribani milioni 3.9 wakigharamia bima ya afya kupitia Serikali. Hadi sasa, kaya 276,004 zimeshasajiliwa kwa awamu ya kwanza kwa gharama ya Sh41 bilioni kwa mwaka,” amesema Dk Mwenisano.
