Serikali yaahidi kutimiza ndoto za Lukuvi Ismani

Iringa. Ndoto za maendeleo alizoziacha aliyekuwa mbunge wa Ismani kwa zaidi ya miongo mitatu, William Lukuvi, zimeibuka tena wakati wa mazishi yake, ambapo   Serikali imeahidi kuendeleza miradi aliyokuwa akiipigania kwa manufaa ya wananchi wa jimbo hilo.

Ahadi hiyo imetolewa leo Machi 31, 2026 na Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, katika mazishi ya kiongozi huyo yaliyofanyika katika kijiji cha Idodi, mkoani Iringa, kufuatia wito uliotolewa na viongozi na wananchi wa Ismani kutaka miradi ya maendeleo aliyokuwa akiisimamia itekelezwe.

Mapema, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Iringa Vijijini, Costantino Kihwelo, ameitaka Serikali kuhakikisha maono ya marehemu yanageuzwa kuwa matokeo halisi kwa wananchi, akitaja miradi ya ujenzi wa barabara ya Pawaga, miundombinu ya umwagiliaji katika eneo la Idodi na uanzishwaji wa mabwawa ya kufugia samaki kuwa miongoni mwa vipaumbele muhimu.

Viongozi mbalimbali nchini wakiwa na familia pamoja na wananchi katika shughuli ya mazishi ya aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), na Mbunge wa Jimbo la Isimani, William Lukuvi, iliyofanyika leo Machi 31, 2026 nyumbani kwake Idodi mkoani Iringa.

Amesema miradi hiyo ni sehemu ya ndoto za maendeleo ambazo Lukuvi alikuwa akizisukuma kwa nguvu kwa ajili ya kuinua uchumi wa wananchi wa maeneo ya Pawaga, Ismani na Idodi.

“Tunapozungumza hapa hatuzungumzi ndoto mpya, tunazungumzia maono ambayo tayari yalikuwa yameanza kupewa mwelekeo na Mzee Lukuvi. Serikali isimamie utekelezaji wake hadi mwisho,” amesema Kihwelo.

Kauli hiyo imeungwa mkono na wananchi waliohudhuria mazishi hayo ambao wameonyesha matumaini makubwa kuwa miradi hiyo itatekelezwa kama sehemu ya kuenzi mchango wa kiongozi huyo.

Akijibu wito huo, Dk Mwigulu amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wananchi wa Ismani kuhakikisha maendeleo yaliyokuwa yakipiganiwa na Lukuvi yanafika kwa wananchi.

Viongozi mbalimbali nchini wakiwa na familia pamoja na wananchi katika shughuli ya mazishi ya aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), na Mbunge wa Jimbo la Isimani, William Lukuvi, iliyofanyika leo Machi 31, 2026 nyumbani kwake Idodi mkoani Iringa.

“Nimeagizwa niseme wazi kuwa Serikali haitaacha yale yote aliyokuwa akiyapigania Lukuvi. Tutaendelea kushirikiana nanyi kuhakikisha maendeleo yanafika kwa wananchi wote wa eneo hili,” amesema.

Katika hotuba yake, Mwigulu amemtaja marehemu Lukuvi kuwa kiongozi aliyekuwa na nidhamu ya hali ya juu na aliyekuwa akijituma kutekeleza majukumu yake bila kusubiri kusukumwa.

Amesema marehemu alikuwa mshauri wa viongozi wengi ndani na nje ya Serikali, akiwemo wabunge, mawaziri, manaibu mawaziri na makatibu wakuu.

“Alikuwa mtu wa kazi. Hakusubiri kuambiwa afanye nini, alijua wajibu wake na aliutekeleza kwa moyo wote,” amesema.

Ameongeza kuwa hata katika maeneo ambayo hayakuwa chini ya wizara yake, Lukuvi alikuwa na tabia ya kujifunza kwa kusoma hotuba na nyaraka mbalimbali ili kuongeza uelewa wake katika utendaji wa Serikali.

Wakizungumza na Mwananchi Digital, baadhi ya wananchi wa Jimbo la Ismani wamesema miradi hiyo imekuwa ikitajwa kwa muda mrefu bila kukamilika, hali inayochangia changamoto za kiuchumi katika maeneo yao.

Mkazi wa Ismani, Mashaka Nduva, amesema barabara ya Pawaga ni muhimu kwa maisha ya wananchi kwa kuwa inasaidia usafirishaji wa mazao na upatikanaji wa huduma muhimu.

Viongozi mbalimbali nchini wakiwa na familia pamoja na wananchi katika shughuli ya mazishi ya aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), na Mbunge wa Jimbo la Isimani, William Lukuvi, iliyofanyika leo Machi 31, 2026 nyumbani kwake Idodi mkoani Iringa.

“Barabara hii ni uhai wetu, lakini imekuwa changamoto kubwa hasa wakati wa mvua. Tunaamini sasa ni wakati wake kukamilika,” amesema.

Ameongeza kuwa mabwawa ya kufugia samaki yanaweza kuwa chanzo kikubwa cha ajira kwa vijana wa eneo hilo.

Kwa upande wake, mkazi wa Idodi, Ally Chuya, amesema wananchi wa eneo hilo wana matumaini makubwa kuhusu miradi ya umwagiliaji kwa kuwa itawasaidia kuondokana na utegemezi wa mvua.

“Tukipata umwagiliaji tutalima mwaka mzima na kuongeza uzalishaji pamoja na kipato chetu,” amesema.