Dar es Salaam. Viongozi mbalimbali wamemtaja aliyekuwa Mbunge wa Ismani na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Bunge na Uratibu , William Lukuvi (70), kama kiongozi aliyependa kufanya kazi kwa vitendo, aliyedumisha ukaribu na wananchi na kuacha mfano wa uongozi unaopaswa kuigwa na vizazi vijavyo.
Lukuvi alifariki dunia Machi 25, 2026 katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dodoma alikokuwa akipatiwa matibabu ya mshtuko wa moyo, anatarajiwa kuzikwa leo Jumanne, Machi 31, 2026 katika kijiji cha Idodi baada ya kufanyika kwa adhimisho la misa takatifu iliyoongozwa na Naibu Askofu Jimbo Katoliki Iringa, Paul Msombe.
Wakizungumza baada ya azimisho la misa hiyo, viongozi hao wamesema Lukuvi alijijengea heshima kubwa ndani ya chama na kwa wananchi kutokana na unyenyekevu, kujituma na uwezo wake wa kudumisha uhusiano wa karibu na wapiga kura wake kwa zaidi ya miongo mitatu.
Waziri Mkuu. Mwigulu Nchemba akiwa na mke wake waliweka shada wakati wa mazishi ya aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), na Mbunge wa Jimbo la Isimani, William Lukuvi, iliyofanyika leo Machi 31, 2026 nyumbani kwake Idodi mkoani Iringa.
Spika mstaafu wa Bunge, Anne Makinda amesema Lukuvi alikuwa mtu wa vitendo zaidi kuliko maneno, akisisitiza kizazi cha sasa kinapaswa kuiga utamaduni huo wa kufanya kazi kwa bidii.
“Lukuvi hakuwa mtu wa maneno bali vitendo zaidi. Tukiwa Umoja wa Vijana wakati ule tulikuwa timu ya mwisho pamoja na kina Jakaya Kikwete na Abdulrahman Kinana. Tulipoondoka ndipo kikaingia kikosi cha akina Lukuvi,” amesema Makinda.
Amesema Lukuvi aliwafundisha wananchi wa Ismani kujitegemea na kufanya kazi kwa bidii bila kunung’unika wala kusubiri kusaidiwa kila wakati.
“Naomba muendeleze mtindo aliowafundisha wa kujitegemea, kufanya kazi bila kunung’unika wala kutegea. Watanzania tumezidi maneno, lakini maneno pekee hayaijengi nchi, tunapaswa kufanya kazi,” amesema Makinda.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda amesema alimfahamu Lukuvi kwa karibu katika vipindi mbalimbali vya utumishi wake serikalini na kisiasa, akimtaja kama kiongozi aliyeelewa vizuri nafasi ya mbunge na umuhimu wa kuwa karibu na wapiga kura.
Pinda amesema Lukuvi alikuwa na uwezo mkubwa wa kujenga mahusiano na jamii, jambo lililomfanya kudumu kwa muda mrefu katika Jimbo la Ismani.
Viongozi mbalimbali nchini wakiwa na familia pamoja na wananchi katika shughuli ya mazishi ya aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), na Mbunge wa Jimbo la Isimani, William Lukuvi, iliyofanyika leo Machi 31, 2026 nyumbani kwake Idodi mkoani Iringa.
“Alikuwa anaelewa vizuri nafasi ya ubunge na uhusiano wake na wapiga kura. Pia alikuwa mzuri sana kuzungumza lugha ya Kihehe, jambo lililomsaidia kujenga ukaribu mkubwa na wananchi,” amesema Pinda.
Ameongeza pamoja na nafasi kubwa alizowahi kushika serikalini, Lukuvi alibaki kuwa mtu mnyenyekevu na wa kawaida.
“Hakuwa mtu wa makuu. Sio wale wanaotaka hata koti lishikiliwe wanapotembea. Ukikutana naye ni mtu wa kawaida kabisa,” amesema Pinda.
Viongozi mbalimbali nchini wakiwa na familia pamoja na wananchi katika shughuli ya mazishi ya aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), na Mbunge wa Jimbo la Isimani, William Lukuvi, iliyofanyika leo Machi 31, 2026 nyumbani kwake Idodi mkoani Iringa.
Naye Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasira amesema safari ya kisiasa ya Lukuvi ni somo kwa vijana ndani ya CCM, akisisitiza kuwa alipanda ngazi za uongozi hatua kwa hatua kuanzia ngazi za chini.
Amesema Lukuvi alijiunga na Tanu mwaka 1974, miaka mitatu kabla ya kuanzishwa kwa Chama cha Mapinduzi, na baadaye akapanda ngazi mbalimbali hadi kufikia nafasi ya Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana.
Wasira amesema tofauti na baadhi ya viongozi, Lukuvi aliendelea kulilea jimbo lake hata baada ya kushika nyadhifa kubwa serikalini.
“Sio wengi sana wanaoweza kuwa wabunge, wakawa mawaziri na bado wakaendelea kulilea jimbo lao. Wengi wakishapata nafasi hizo wanasahau majimbo yao na kuyakumbuka wakati wa uchaguzi,” amesema.
Ameongeza kwa zaidi ya miaka 31 aliyokuwa Mbunge wa Ismani na kuhudumu kama waziri katika awamu nne za Serikali, Lukuvi aliendelea kudumisha uhusiano wake na wananchi na shughuli za chama.
Familia ya aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), na Mbunge wa Jimbo la Isimani, marehemu William Lukuvi, katika mazishi iliyofanyika leo Machi 31, 2026 nyumbani kwake Idodi mkoani Iringa.
“Chama chetu kimepoteza mwanachama mahususi. Itakapofika wakati wa kuchagua mrithi wake, ni muhimu kuhakikisha anapatikana mtu atakayeendeleza kazi nzuri aliyoifanya Lukuvi,” amesema Wasira.
