Wanawake wabeba uchumi wa buluu, lakini wanabaki pembeni katika maamuzi

Tanga. Wanawake katika uchumi wa buluu bado wako nyuma katika ngazi za maamuzi licha ya mchango wao mkubwa, hali inayohitaji mabadiliko ya sera na mifumo.

Hoja hiyo iliibuliwa katika kongamano la maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani 2026, ambapo wadau walisisitiza umuhimu wa kuwapa wanawake nafasi zaidi katika maamuzi.

Mkurugenzi wa Mradi wa ReSea, Perpetua Angima, alisema wanawake wanashiriki kikamilifu katika shughuli za baharini kama kilimo cha mwani, uchakataji wa samaki na ufugaji wa viumbe wa baharini, lakini hawana ushawishi kwenye maamuzi.

Evansia Shirima kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais alisema Sera ya Taifa ya Uchumi wa Buluu ya 2024 inalenga kuongeza ushiriki wa wanawake, ingawa mabadiliko ya tabianchi bado yanawaathiri zaidi.

Kwa upande wa wanufaika, Jamila Ali alisema mafunzo yameongeza ujuzi na uzalishaji, lakini changamoto kama mitazamo hasi, ukosefu wa mitaji na miundombinu duni bado zipo.

Wadau walisisitiza kuwa bila kuwapa wanawake nafasi ya kushiriki kikamilifu katika maamuzi, maendeleo ya uchumi wa buluu hayatakuwa endelevu.