Waziri Mkuu: William Lukuvi Ataendelea Kukumbukwa Milele – Video


WAZIRI MKUU, Mwigulu Nchemba, amesema aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) na Mbunge wa Isimani, William Lukuvi, ataendelea kukumbukwa na Watanzania kwa mchango wake mkubwa na utumishi uliotukuka katika nafasi mbalimbali alizowahi kushika.

Akizungumza katika ibada ya mazishi iliyofanyika nyumbani kwa marehemu katika kijiji cha Idodi, wilayani Iringa mkoani Iringa leo Jumanne, Machi 31, 2026, Waziri Mkuu alisema kuwa Lukuvi alikuwa nguzo muhimu katika kuleta maendeleo kupitia nafasi zake serikalini, bungeni na ndani ya chama.

“Mheshimiwa Lukuvi atakumbukwa kwa mengi na Watanzania kutokana na utumishi wake uliotukuka katika nafasi mbalimbali. Mchango wake kwa jamii na Watanzania kwa ujumla umekuwa chachu ya maendeleo,” alisema.

Waziri Mkuu ambaye aliongoza mazishi hayo kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, aliwahakikishia wananchi kuwa ndoto na maono ya marehemu yataendelea kutekelezwa.

“Kwa niaba ya Mheshimiwa Rais, niwahakikishie kwamba yale aliyoyasimamia na kuyaota yataendelea kutimizwa,” alisisitiza.

Aidha, aliwataka wananchi wa Isimani kuendelea kumuenzi marehemu kwa kudumisha umoja na kuepuka migawanyiko isiyo na tija.

“Na kwa wana-Isimani, ninawasihi tuendelee kumuenzi, tusianze mashindano, tulinde heshima ya Mzee wetu kwa kuwa na staha,” aliongeza.

Akimzungumzia zaidi marehemu, Waziri Mkuu alisema kuwa Lukuvi alikuwa kiongozi aliyegusa maisha ya watu moja kwa moja, jambo lililomuwezesha kudumu madarakani kwa zaidi ya miaka 31 akiwa Mbunge wa Isimani.

“Si kazi rahisi kuongoza kwa muda wote huo, lakini yeye aliweza kwa sababu aliweka kipaumbele kwenye maisha ya wananchi wake,” alisema.

Katika hatua nyingine, Serikali imeahidi kuendeleza miradi aliyokuwa akiisimamia marehemu, ikiwemo ujenzi wa barabara za lami katika maeneo ya Pawaga na Isimani.

“Miradi yote aliyoiacha itaendelea kutekelezwa kama sehemu ya Ilani ya CCM, lakini pia kama njia ya kumuenzi Mheshimiwa Lukuvi,” alihitimisha.

Mazishi hayo yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, chama na wananchi, wakimuenzi kiongozi huyo aliyetoa mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa.