Wito shule binafsi kuchangamkia elimu ya amali

Dar es Salaam. Katika ulimwengu unaobadilika kwa kasi, ambako ajira rasmi zinazidi kuwa haba na ushindani wa soko la ajira unazidi kupanda, mfumo wa elimu hauwezi kubaki vilevile. 

Wazazi wanahitaji kuona watoto wao wakipata maarifa yatakayowasaidia kujitegemea, kuajirika au kujiajiri mara tu wanapohitimu masomo yao. 

Hili ndilo chimbuko la msukumo mpya wa kuimarisha elimu ya amali nchini Tanzania; mfumo unaolenga kuwapa wanafunzi ujuzi wa vitendo sambamba na maarifa ya kitaaluma.

Kwa miaka mingi, elimu yetu imejikita zaidi katika nadharia kuliko vitendo. Matokeo yake ni maelfu ya wahitimu wanaomaliza shule wakiwa na vyeti lakini bila ujuzi wa moja kwa moja wa kufanya kazi au kuanzisha miradi ya kujitegemea. 

Serikali imeliona pengo hili na kuanza kusisitiza utekelezaji wa elimu ya amali katika ngazi mbalimbali za masomo, ikilenga kuwajengea wanafunzi stadi za kazi, ubunifu na uwezo wa kuzalisha mali.

Hata hivyo, utekelezaji wa sera na maono haya unahitaji rasilimali, maandalizi na dhamira ya kweli. Ni katika muktadha huu ambapo shule binafsi zinapaswa kuchukua nafasi ya mbele na kuwa vinara wa mageuzi haya muhimu.

Elimu ya amali si dhana mpya. Tangu miaka ya mwanzo baada ya uhuru, kulikuwa na juhudi za kuifanya elimu iwe ya kujitegemea, kwa kuunganisha masomo ya darasani na shughuli za uzalishaji.

Lengo lilikuwa kuwafanya wanafunzi waelewe kuwa elimu si tu kwa ajili ya kuajiriwa ofisini, bali pia ni nyenzo ya kuunda ajira na kuchangia maendeleo ya jamii.

Katika awamu ya sasa, elimu ya amali imepewa msisitizo mpya ili kuendana na mahitaji ya karne ya 21.

Inahusisha masomo na mafunzo ya vitendo kama vile ufundi seremala, umeme, kilimo cha kisasa, ufugaji, Tehama, ushonaji, useremala, uchomeleaji na stadi nyingine za kazi. Haya ni maeneo yenye fursa kubwa za ajira na ujasiriamali.

Kwanza, elimu hii humjengea mwanafunzi uwezo wa kufanya kazi kwa mikono yake na kutatua matatizo kwa ubunifu. 

Pili, hupunguza utegemezi wa ajira rasmi, kwani mhitimu anaweza kuanzisha mradi wake mwenyewe. Tatu, huongeza tija katika jamii kwa kuzalisha wataalamu wa kati wanaohitajika katika sekta mbalimbali za uchumi.

Pamoja na nia njema ya Serikali, utekelezaji wake katika shule nyingi za umma umekumbana na changamoto kadhaa.

Idadi kubwa ya wanafunzi, uhaba wa walimu wa masomo ya amali na upungufu wa miundombinu kama karakana na maabara vimekuwa kikwazo kikubwa.

Shule nyingi zinahangaika hata kukidhi mahitaji ya msingi kama madarasa na walimu wa masomo ya kawaida, hali inayofanya utekelezaji wa elimu ya amali kuwa mgumu zaidi.Hapa ndipo nafasi ya shule binafsi inapojitokeza wazi.

Shule binafsi zina faida ya kuwa na mitaji na uhuru mkubwa wa kufanya uamuzi wa kiuwekezaji. Tofauti na shule za Serikali, ambazo zinategemea bajeti ya umma na kugawana rasilimali chache kwa shule nyingi, taasisi binafsi zina uwezo wa kupanga vipaumbele vyao kulingana na dira na mkakati wao wa muda mrefu. Hili linazipa nafasi ya kuwekeza katika miundombinu ya elimu ya amali bila kuchelewa.

Kwa mfano, shule binafsi zinaweza kujenga karakana za useremala, umeme au ufundi magari ndani ya muda mfupi, endapo zitatenga fedha na kupanga vizuri. 

Pia zinaweza kuanzisha mashamba darasa kwa ajili ya kilimo cha kisasa au mabanda ya mifugo kwa mafunzo ya ufugaji wa kibiashara. 

Uwekezaji huu, ingawa unahitaji mtaji wa awali, ni wa muda mrefu na unaweza hata kuongeza mvuto wa shule kwa wazazi wanaotafuta elimu yenye matokeo ya moja kwa moja kwa watoto wao.

Zaidi ya miundombinu, shule binafsi zina uwezo wa kuajiri walimu na wakufunzi wenye utaalamu maalumu katika fani za amali. Zinaweza kuvutia wataalamu kutoka viwandani au katika sekta binafsi na kuwapa mikataba maalumu ya kufundisha kwa muda au kudumu. 

Hii ni tofauti na mfumo wa Serikali unaokabiliwa na changamoto ya ajira na mgawanyo wa walimu, ambapo hata walimu wa masomo ya kawaida hawatoshi katika shule nyingi.

Ni ukweli usiopingika kuwa Serikali inaelemewa na mzigo wa kuendesha shule nyingi kote nchini. Kuanzia mishahara ya walimu, ujenzi wa miundombinu, hadi ununuzi wa vitabu na vifaa vya kufundishia, majukumu haya ni makubwa na yanahitaji fedha nyingi. Katika mazingira haya, ni vigumu kwa kila shule ya umma kuwa na karakana za kisasa au vifaa vya kutosha kwa mafunzo ya amali.

Hii haimaanishi kuwa Serikali haifanyi jitihada; bali inaonesha wazi kuwa sekta binafsi ina wajibu wa kushirikiana katika kuimarisha ubora wa elimu. Shule binafsi zinapochangamkia elimu ya amali, si tu zinasaidia wanafunzi wao bali pia zinachangia juhudi za kitaifa za kujenga nguvu kazi yenye ujuzi.

Aidha, kuwekeza katika elimu ya amali kunaweza kuwa fursa ya kiushindani kwa shule binafsi. Katika soko la elimu lililojaa ushindani, wazazi wengi wanatafuta thamani halisi ya ada wanazolipa.

Shule inayoweza kuonesha kuwa inatoa si tu ufaulu wa mitihani bali pia ujuzi wa vitendo, itakuwa na mvuto mkubwa zaidi. Hii inaweza kuongeza usajili na hata kuimarisha hadhi ya taasisi husika.

Ni wakati sasa kwa wamiliki na wasimamizi wa shule binafsi kutafakari kwa kina mustakabali wa elimu wanayoitoa. Je, wanawaandaa wanafunzi wao kwa mitihani pekee, au kwa maisha halisi baada ya shule? Je, wanachukua hatua za kuendana na mwelekeo wa taifa katika kuimarisha elimu ya amali?

Mageuzi ya kweli ya elimu hayawezi kuachwa mikononi mwa Serikali pekee. Yanahitaji ushirikiano wa wadau wote, wakiwamo watoa elimu binafsi. Kwa kutumia mitaji yao, uwezo wa kuajiri wataalamu na kujenga miundombinu, shule binafsi zina kila sababu na kila uwezo wa kuwa mstari wa mbele katika mapinduzi ya elimu ya amali.