UGUMU wanaopata viongozi wa Simba kuachana na kiungo Neo Maema ni kinga inayotoka kwa kocha wa timu hiyo, Steve Barker anayeangalia faida za staa huyo zaidi ya kile anachokionyesha uwanjani.
Katika kanuni ya 65 kifungu cha (5) kinasema kocha mkuu wa timu ndiye anawajibika kutangaza wachezaji wanaoachwa, wanaohamia na wanaohama pamoja na usajili kamili wa timu katika kipindi cha kukamilika kwa usajili wa timu, hilo linampa nguvu Barker kuamua nani asalie Simba na kuondoka.
Ikishindikana kuachana Maema itakuwa awamu ya pili ya kwanza ilikuwa achwe usajili wa dirisha kubwa, kipindi hicho kocha Barker alitoka kujiunga na timu, hivyo walimpa nafasi ya kuwaangalia wachezaji kupitia Kombe la Mapinduzi na staa alipona kukatwa.
Pia kanuni ya usajili ya 65 kifungu (4) kinasisitiza usajili wa wachezaji ni suala la kiufundi kama ilivyo kanuni ya 77:4. Kocha Mkuu wa timu atawajibika kutambua wachezaji wanaotakiwa kusajiliwa, endapo Barker hatakubaliana na maamuzi ya viongozi Maema ataendelea kusalia msimu 2026/27.
Simba inafanya mchakato wa usajili kimyakimya ili Ligi Kuu itakapofika mwisho wanatarajia wawe wamemaliza kila kitu, miongoni wa sababu zilizotolewa kwa nini Maema aachwe ipo ya umri (aliyezaliwa 01/12/1995 (30) nchini Afrika Kusini) na hawajaridhishwa na kiwango alichokionyesha.
Lakini mapendekezo hayo yalipofika kwa kocha, akawapa sababu kwa nini Maema asikatwe ikiwemo uzoefu, ni kiongozi mwenye ushawishi dhidi ya wenzake na anapenda umoja na hamasa. Chanzo hicho kilisema:”Kocha anaona Simba ina wachezaji wachache wazoefu ambao ni Shomari Kapombe, Clatous Chama na Maema lakini katoa plani B endapo Maema akiondoka atafutwe mgeni mwingine mzoefu na mwenye kiwango cha juu.”
Kiungo huyo aliyefunga bao moja hadi sasa inaelezwa nje ya uwanja ni mchezaji anayeweza akaelekeza wenzake na kukemea vitu visivyokuwa vya kinidhamu bila kuogopa, muumini wa kuhakikisha wanakuwa na morali kabla ya mechi na baada ya kuhakikisha hawatoki katika mstari wa kupambana pia ni mtu anayependa utani mwingi, hilo ni tofauti kidogo kwa Kapombe anayetajwa ana nidhamu ya hali ya juu, lakini ni mpole asiyependa mambo mengi.
“Kapombe hajavuliwa beji ya unahodha, lakini ni mpole akiongea neno moja kwa ustaarabu anaamini kila mtu anakuwa ameelewa, tofauti na Maema mchezaji akikosea anamfesi na kumwambia lakini ana ushawishi mkubwa sana kwenye vyumba, hivyo kocha anajikuta anatumia muda mchache kuwaelekeza wachezaji juu ya nidhamu ama vitu gani wanapaswa kuvifanya,” kilisema chanzo hicho.
Chanzo hicho kilisisitiza Kapombe ambaye msimu wa 2024/25, alimaliza na mabao matatu na asisti tatu ni mtu wa kazi zaidi uwanjani na asiyependa makelele wanapokuwa kambini, hivyo katika kuongeza wachezaji anakuwa anasaidiwa zaidi na Maema katika kukemea anapoona vitu haviendi sawa.
Alipotafutwa kocha Barker:”Huu siyo muda wa kuzungumzia usajili, kila mchezaji ni muhimu katika kuyatimiza malengo ya klabu Maema ni bora sana kwenye timu yangu, mwisho wa msimu ndipo inapokuwa inafanyika tathimini ya kipi kifanyike, ila kwa sasa tunaelekeza nguvu zetu kuwania ubingwa.”
