Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba ameiagiza Wizara ya Kilimo kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara ili kuweka mpango mahsusi wa usimamizi wa katazo la utaratibu wa lumbesa.
Kwa mujibu wa Dk Mwigulu, mpango huo mahsusi utaleta tija inayotarajiwa katika sekta ya kilimo nchini, huku akisisitiza mazao yote yanayofungashwa kwenye vifungashio yauzwe kwa kuzingatia vipimo.
Dk Mwigulu ameeleza hayo leo Jumatano Aprili Mosi, 2026 wakati akiwasilisha makadirio ya bajeti ya ofisi yake kwa mwaka 2026/27 bungeni jijini Dodoma, akiomba kuidhinishiwa Sh12.5 trilioni.
“Suala hili litekelezwe sambamba na halmashauri zote kusitisha mara moja ushuru holela unaotozwa kwa mazao ya kilimo. Vilevile, kusitisha utaratibu wa wakulima kukopwa mazao na AMCOS,” amesema Dk Mwigulu.
Aidha, Dk Mwigulu amesema kwa mwaka 2026/2027, Serikali itaendelea kuimarisha upatikanaji wa pembejeo, huduma za ugani, afya ya udongo, hifadhi ya chakula na masoko ya mazao.
Amefafanua lengo kuu ni kuongeza uzalishaji, kuimarisha usalama wa chakula na lishe, kukuza kilimo biashara na kuongeza mchango wa sekta ya kilimo katika ukuaji wa uchumi.
Kuhusu sekta ya mifugo, Dk Mwigulu amesema Serikali imeendelea kuiimarisha kwa kuboresha mazingira ya ufugaji na biashara ya mifugo.
Jitihada zilizochukuliwa ni pamoja na kuendelea na utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa karantini ya Kwala mkoani Pwani yenye thamani ya Sh997.99 milioni ambapo umefikia asilimia 45.”
“Kukamilika kwa karantini hiyo kutaongeza idadi ya mifugo itakayokidhi vigezo vya kusafirishwa nje ya nchi,” ameeleza Dk Mwigulu.
Endelea kufuatilia Mwananchi
