Same. Hofu, sintofahamu na taharuki vimetanda katika Kitongoji cha Makandeni, Kijiji cha Marieni, Kata ya Chome wilayani Same, Mkoa wa Kilimanjaro baada ya ardhi kuanza kutitia na kujipasua kuzalisha nyufa hadi kwenye makazi ya watu.
Kutokana na hali hiyo, kaya 10 zimeyakimbia makazi katika kitongoji hicho, huku moja ya nyumba za ibada ikishindwa kutumika, baada ya kutengeneza nyufa zilizosababishwa na hali hiyo.
Mmoja wa wananchi wa Kijiji cha Marieni, kata ya Chome, akionyesha moja ya eneo ambalo limeathiriwa na mpasuko wa ardhi ambao umepelekea baadhi ya maeneo kutitia.
Katika tukio hilo lisilo la kawaida, wananchi wanaoishi pembezoni mwa Milima ya Chome, wameingiwa hofu, wakishuhudia ardhi ikisogea, maeneo mengine yakididimia, jambo linalotia mashaka juu ya usalama wa maisha yao.
Kufuatia hali hiyo, baadhi ya wananchi ambao maeneo yao yameathiriwa wamehamisha familia zao na mali zao na kwenda kuhifadhi walikopata hifadhi ya muda wakisubiri muafaka wa Serikali.
Baadhi ya wananchi wakionyesha eneo karibu na kanisa la Wasabato Kungwini ambalo limepata mpasuko mkubwa kutokana na baadhi ya vipande vya aradhi kupishana.
Mwananchi ilipotembelea eneo hilo, leo Aprili Mosi, 2026, imeshuhudia moja ya makanisa likiwa limeachwa wazi baada ya kuta zake kupasuka kwa nyufa kubwa, huku sakafu yake ikionyesha dalili za kutitia.
Waumini wake, wamelazimika kusitisha ibada na kutafuta hifadhi katika makanisa jirani wakati wakisubiri suluhisho la kudumu.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, amesema tayari Serikali imeanza kuchukua hatua kwa kuagiza wataalamu kwenda eneo hilo kufanya uchunguzi wa kina.
“Nimeshapokea taarifa na nimeshaelekeza wataalamu waende haraka ili kubaini chanzo cha tatizo na hatua stahiki za kuchukua,” amesema.
Moja ya eneo la kanisa la Wasabato, ambalo lipo katika Kitongoji cha Makandeni, Kijiji cha Marieni, ambalo limeachana kutokana na ufa mkubwa ambao umepita katika eneo hilo la kanisa.
Kinachotokea sasa, kilitokea mwaka 2009, katika Kitongoji cha Manja, kata ya Mamba Myamba wilayani humo ambapo watu 24 walifariki dunia baada ya kuangukiwa na maporomoko ya udongo na magema, hali ambayo ilisababisha baadhi ya wananchi hao kuhama.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wakazi wa eneo hilo, wamesema hali hiyo inaongezeka, huku mipasuko ya ardhi ikisambaa kutoka eneo moja hadi jingine na kuongeza hofu miongoni mwao.
Mmoja wa wananchi wa Kijiji cha Marieni, kata ya Chome, akionyesha moja ya eneo ambalo limeathiriwa na mpasuko wa ardhi ambao umepelekea baadhi ya maeneo kutitia.
Mzee wa Kanisa la Wasabato Kungwini lililoathirika, Msafiri Mkodo, amesema changamoto hiyo imewalazimu kuhama mara mbili kutoka eneo moja la ibada kwenda jingine na hata walipojaribu kujenga kanisa jipya, nalo limekumbwa na tatizo hilo.
“Awali tuliona nyufa ndogo, lakini zilikuja kuwa kubwa na kuhatarisha maisha yetu. Tulihama tukajenga kanisa jingine pembeni, lakini nako hali ikawa ileile. Kwa sasa tumelazimika kuondoka kabisa,” amesema.
Kutokana na hali hiyo, waumini wa kanisa hilo wamekosa mahali pa kuabudia na kulazimika kutawanyika katika makanisa mengine huku wakijipanga kujenga banda la muda katika eneo salama.
Mkazi mwingine wa eneo hilo, Amani Elia, amesema wao na familia zao wamelazimika kuhama baada ya nyumba zao kupasuka vibaya na kukosa usalama wa kulala usiku.
Mmoja wa wananchi wa Kijiji cha Marieni, kata ya Chome, akionyesha moja ya eneo ambalo limeathiriwa na mpasuko wa ardhi ambao umepelekea baadhi ya maeneo kutitia.
“Kwa sasa tunaishi kwa ndugu, hatuwezi kulala kwenye nyumba yenye nyufa kubwa. Tunaogopa inaweza kuanguka muda wowote,” amesema.
Kwa upande wake, John Chambua, amesema hali hiyo imewalazimu wakazi wengi kuondoka kwa hiari ili kuokoa maisha yao, wakisubiri wataalamu wa Serikali waje kubaini chanzo cha tatizo hilo.
“Hii si hali ya kawaida. Nyufa zinazidi kutanuka kila siku. Tumeamua kuondoka kwanza, tusubiri majibu ya wataalamu,” amesema.
Naye, Elisa Mtera, amesema kinachowaongezea hofu ni kasi ya ardhi kusogea, akidai kuwa katika baadhi ya maeneo imeonekana kusogea hadi mita moja.
“Tunajiuliza hii ardhi imeenda wapi inapohama? Ina maana kuna nguvu kubwa chini yake. Hii inatisha sana,” amesema.
Mmoja wa wananchi wa Kijiji cha Marieni, kata ya Chome, akionyesha moja ya eneo ambalo limeathiriwa na mpasuko wa ardhi ambao umepelekea baadhi ya maeneo kutitia.
Mwenyekiti wa kitongoji cha Makandeni, Marry Godfrey, amesema tayari kaya 10 zimekimbia makazi yao, akiwemo yeye, huku akibainisha athari zimegusa vitongoji vitatu.
“Watu hawana pa kukaa, nyumba zimepasuka, hata mashamba yameathirika. Tunaomba msaada wa haraka wa Serikali,” amesema.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Marieni, Andrea Mndeme, amesema tatizo hilo lilianza mwishoni mwa mwaka jana na limekuwa likiongezeka kwa kasi siku hadi siku.
“Kadiri muda unavyokwenda, ndivyo hali inavyozidi kuwa mbaya. Tunahitaji wataalamu waje watueleze ukweli na hatua za kuchukua,” amesema.
