Ifakara yawa mfano kwa wataalamu wa Tarura kupitia mpango wa CBRM

Morogoro. Wataalamu wa wakala wa barabara za vijijini na mijini (Tarura) kutoka wilaya nane wametembelea Halmashauri ya mji Ifakara iliyopo wilaya ya Kilombero, kwa lengo la kujifunza utekelezaji wa mpango wa matengenezo ya barabara kwa kutumia vikundi vya kijamii (CBRM) unaotekelezwa kupitia mradi wa Rise.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, msimamizi wa mpango huo wa CBRM, Mhandisi Richard Missa amesema ziara hiyo ya mafunzo imelenga kuwajengea uwezo wataalamu hao ili waweze kutekeleza kwa ufanisi shughuli za matengenezo ya barabara kwenye halmashauri zao mara watakapopata mikataba ya utekelezaji.

Amezitaja halmashauri zilizofanya ziara hiyo ya mafunzo kuwa ni Mkuranga, Mvomero, Rufiji Lushoto, Pangani, Korogwe, Kongwa na Kilombero

Amesema mpango huo pia umelenga kuhakikisha barabara za vijijini zinapitika wakati wote lakini pia kuwapa vipato wananchi kupitia vikundi vyao vya kijamii ambavyo ndio vitakavyopewa kazi ya kufanya matengenezo ya barabara hizo.

Naye Meneja wa Tarura Wilaya ya Mkuranga, Mhandisi Silas Dilliwa ameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa kuendelea kuweka kipaumbele katika matengenezo ya barabara, pamoja na uongozi wa mamlaka hiyo  kwa kuruhusu utekelezaji wa mpango huo.

Aidha amesema uzoefu watakaoupata utasaidia kuboresha utekelezaji wa mpango huo katika maeneo yao mengine.

Akieleza manufaa ya mpango huo wa CBRM kwa jamii, Diliwa amesema ni pamoja kuwa na uhakika wa barabara zitakazopitika mwaka mzima kutokana na matengenezo ya mara kwa mara ikiwemo kuziba mashimo, kusafisha mitaro na makaravati hatua inayopunguza uharibifu hasa kipindi cha mvua.

Kwa upande wake Mratibu wa Programu ya CBRM kutoka Shirika la kazi dDuniani (ILO),  Dampu Ndenzako amesema taasisi hiyo inaendelea kushirikiana na Serikali kutoa utaalamu wa kitaifa na kimataifa ili kuhakikisha utekelezaji wa mpango huo unakuwa endelevu na wenye tija kwa wananchi, huku vikundi vya kijamii vikionekana kuwa wanufaika wakuu kupitia ajira na ongezeko la kipato.