Kupanda gharama za uwanja Arusha, Wadau wataka uwajibikaji

Wadau mbalimbali wameibua mjadala kuhusu ongezeko la gharama na changamoto za usimamizi katika miradi ya viwanja vya michezo, masuala ya uwajibikaji na uwazi yanapaswa kupewa kipaumbele ili kurejesha imani ya wananchi katika utekelezaji wa miradi ya umma.

Wanasisitiza umuhimu wa kufuata taratibu zilizowekwa katika mpango wa miradi kabla ya kuendelea na utekelezaji.

Hoja hizo zimetokana na Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere iliyoeleza makadirio yasiyosahihi ya gharama ya ujenzi wa Uwanja wa AFCON Arusha pamoja na udhaifu katika majadiliano ya zabuni ya ujenzi wa uwanja huo.

Kichere amebaini kiwango kidogo cha fedha kilichotarajiwa kutumika katika ujenzi wa uwanja huo ni kidogo kulinganisha na kile kilichosainiwa katika mkataba wa ujenzi.

Amebaini mapungufu katika ununuzi wa mradi wa ujenzi wa uwanja wa mpira wa Arusha wenye thamani ya Sh 338.54 bilioni hali inayoashiria kukosekana kwa tahamani halisi ya fedha katika matumizi ya rasilimali za umma.

Amesema kulikuwa na tofauti kubwa ya makadierio na thamani ya mkataba ambapo mradi ulikadiriwa kugharimu Sh 187 bilioni lakini ulisaikwa Sh 338.54 bbilioni sawa na ongezeko la asilimia 81.

Hata hivyo, wadau wanasema tofauti kati ya gharama za awali na zile za mwisho haziashirii ubadhirifu moja kwa moja, bali mara nyingi ni ishara ya ukiukwaji wa utaratibu au mabadiliko yasiyopitishwa rasmi.

Hivyo hili linaonyesha hitaji la uwajibikaji mkali na kufuata taratibu, ikiwa ni pamoja na kupata idhini mpya ya bajeti kabla ya kubadilisha mpango wa miradi na itasaidia kupunguza mianya ya matumizi mabaya ya fedha za umma.

Wakili, Fulgence Massawe alisema kisheria ongezeko la gharama katika miradi ya viwanja vya michezo ni suala la uadilifu na uwajibikaji wa wahusika.

Alisema tofauti kubwa kati ya makadirio ya awali na gharama halisi inaonyesha kuna tatizo lililokuwepo tangu mwanzo, kwani katika hali ya kawaida, mradi mkubwa hauwezi kufanikishwa bila kujua thamani halisi ya mradi.

Alisema makadirio yaliyotengenezwa bila msingi thabiti au uelewa wa gharama halisi yanatishia uadilifu wa mchakato mzima wa mradi.

Massawe alisema baadhi ya miradi, hasa inayohusiana na maandalizi ya michuano ya AFCON, imeendeshwa chini ya shinikizo la muda, hali inayofungua mwanya wa matumizi mabaya ya fedha.

“Presha ya muda inasababisha uamuzi kuundwa haraka bila kufuata taratibu zote ipasavyo, inaweza kuongeza hatari ya ubadhirifu kwa sababu watu hufanya maamuzi ya haraka ili kukamilisha mradi bila kufuata sheria.”

Pia, alisema mradi umebadilishwa kutoka viwango vya kawaida hadi viwango vya kimataifa umesababisha ongezeko kubwa la gharama bila kufuata upya taratibu za kibajeti.

Wakili huyo alisema iwapo gharama zimeongezeka kutoka kiwango cha awali hadi mara mbili au zaidi, taratibu za kibajeti lazima zifuatwe upya, ikiwemo kuomba idhini mpya kutoka mamlaka husika.

“Kuongeza matumizi kutoka kiwango cha awali hadi kiwango kikubwa namna hiyo bila kibali kipya ni kuvunja misingi ya usimamizi wa fedha za umma na hata katiba,” alisema Massawe.

Alisema hata kama mabadiliko ya mradi yalikuwa muhimu, wahusika walipaswa kurejea mamlaka husika na kuomba idhini mpya kabla ya kuendelea na utekelezaji, ili kuhakikisha kila hatua inafanywa kwa uwazi na kufuata sheria.

 “Ripoti ya CAG huelekezwa bungeni, na ni jukumu la wabunge kuhakikisha hoja zote zinajadiliwa na hatua za kuwawajibisha wahusika zinachukuliwa. Historia inaonyesha kuwa viongozi waliwahi kujiuzulu kutokana na shinikizo la Bunge.”

Pia alisema kutoa majibu nje ya mchakato rasmi wa ukaguzi kunapunguza uhalali wa ripoti na kuibua mashaka zaidi kwa umma. “Kila hoja lazima ijibiwe wakati wa ukaguzi, la sivyo, inaashiria kushindwa kwa wahusika na kudhoofisha imani ya umma kwa ripoti,” amesema.

Massawe alisema suluhisho la kudumu ni kuimarisha nidhamu ya matumizi ya fedha za umma, kuongeza uwazi na kuhakikisha kila mhusika anawajibika.

Amesema bila uwajibikaji halisi, miradi hiyo itaendelea kugubikwa na sintofahamu, na wananchi watapoteza imani na mifumo ya usimamizi wa rasilimali za taifa.

“Uwajibikaji, uwazi, na nidhamu ya kifedha ni msingi wa kuhakikisha miradi ya umma inafanikishwa kwa ufanisi, kwa haki, na kwa manufaa ya wananchi wote,” amesema Massawe.

Akizungumza na Mwananchi Machi 31, 2026 nyota wa zamani wa Simba, Zamoyoni Mogela alisema kuna changamoto ya uwajibikaji, akieleza kuwa mara nyingi hoja zinapoibuliwa hukumbana na utetezi kutoka kwa baadhi ya viongozi badala ya kufanyiwa kazi.

“Kinachotakiwa sasa ni hatua za vitendo bila kufanya hivyo, wananchi wataendelea kupoteza imani na kile kinachoendelea,” alisema Mogella.

Alisema imekuwa kama mazoea baadhi ya watu kupuuzia au kutetea mambo hata pale ambapo kuna viashiria vya ukiukwaji wa taratibu na sheria, jambo ambalo linaathiri taswira ya nchi. “Tunajenga utamaduni mbaya ambapo mtu akizungumza ukweli au kuonyesha kasoro, badala ya kufanyiwa kazi, kunakuwa na juhudi za kutetea hali hiyo, hii siyo afya kwa maendeleo ya taifa.”

Mogella alisema hatua madhubuti zikichukuliwa dhidi ya wahusika wa makosa au uzembe, itasaidia kurejesha imani kwa jamii na wadau wa michezo.

Naye Katibu Mkuu wa zamani wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Angetile Osiah alisema kuna umuhimu wa kusubiri majibu ya taasisi husika kwani ina wezekana ukaguzi ulifanyika muda mrefu.

Alisema inawezekana ukaguzi haukuzingatia muda ambao uwanja umejengwa hivyo hadi muda mkataba unasainia kunaweza kuwa na mabadiliko makubwa.

“Muda wa ujenzi pia unaweza kusababisha gharama kuwa kubwa kumekuwa na kipindi kifupi cha kujenga uwanja kutokana na muda uliowekwa na CAF,”Amesema.

Alisema muda wa kujenga uwanja kwa miaka miwili au mitatu ni tofauti kwa kuujengwa kwa mwaka mmoja na nusu hivyo gharama inaweza kuwa kubwa.

Osiah alisema cha msingi ni majibu ya wahusika kueleza kilitokea nini wakati wa ujenzi wa uwanja huo na endapo kulikuwa na ufisadi ndani ya mradi na wahusika hawajachukuliwa hatua basi imani itapotea kwa jamii.

Ni muhimu kwa wananchi wa kuelewa kwamba masuala yote yaliyoainishwa katika ripoti yatapata majibu rasmi kutoka serikalini. Baada ya kufahamika yale maeneo yaliyokuwa na amatatizo yatachuliwa hataua na yenye majawabu yatafutwa.

Alisema kuhusu mpango wa ujenzi wa viwanja vya michezo ulianza mwaka 2021 ambapo wa kiwanja cha Arusha makadirio yake yalikuwa Sh 187 

 “Tunapopanga ujenzi wa viwanja vikubwa, gharama zinaweza kuongezeka kulingana na vipimo na mahitaji ya kimataifa. Kwa mfano, uwanja unaojengwa kwa viwango vya mashindano ya AFCON unahitaji miundombinu ya kiwango cha juu,” alisema Msigwa.

Alisema Serikali iliamua kujenga viwanja vinavyoweza kupokea mashindano makubwa ya kimataifa, siyo tu kwa shindano la AFCON, inamaanisha viwanja vitajengwa kwa kiwango kikubwa, na gharama za ujenzi zitalingana na mahitaji hayo.

Alisema makadirio ya Serikali ya Sh 187 bilioni ilikuwa kabla ya kuthibitishwa na CAF kuwa wenyeji wa mashindano ya AFCON, hivyo Oktoba 2023 ndipo ilipothibitishwa hivyo ikabidi kubadilisha mpango ilikujenga kufikia vigezo wanavyovitaka.

Mtaalamu wa masuala ya uchumi Florianus Karugaba alisema dhana ya fedha kupotea kwenye ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) mara nyingi haimaanishi fedha zimeibiwa.

Alisema mara nyingi ni tatizo la ukosefu wa vielelezo vya matumizi, ambapo nyaraka kama risiti au mikataba hazipatikani kuthibitisha jinsi fedha zilivyotumika.

“Mkaguzi anaposema fedha hazionekani, anaweza kumaanisha kuwa hakuna nyaraka za kuthibitisha matumizi yake, si lazima kwamba zimeibwa, ushahidi wa malipo ni muhimu ili kuhakikisha matumizi ya fedha za umma yanafuata sheria  ” alisema Karugaba.

 Alisema kila mradi hupitia hatua muhimu ikiwemo kupanga mradi, kufuata kanuni za manunuzi na kisha utekelezaji ambapo hatua hizi ni muhimu kuhakikisha kila gharama inafanyiwa uthibitisho na uwazi.

“Katika hali ya kawaida, mradi unaanza na mpango ukibadilika njiani, ni lazima marekebisho yarudi kwenye mpango, yapitishwe tena, ndipo utekelezaji uendelee, huwezi kubadilisha tu njiani bila kufuata utaratibu.” alisema.

Mtaalamu huyo alisema mkaguzi anakagua kwa kuanzia kwenye mpango akikuta utekelezaji umeenda tofauti na mpango bila kufuata taratibu, anaona kuna mapungufu hata kama fedha hazijaibiwa ni muhimu kuhakikisha uadilifu na uwajibikaji katika miradi ya umma

Akitolea mfano, uwanja huop wa Arusha alisema mradi unaweza kuanza kwa ukubwa fulani lakini ukapanuliwa njiani kutokana na mahitaji mapya, jambo ambalo linaweza kuongeza gharama bila maana ya fedha kupotea.

“Hatari kubwa hutokea pale mabadiliko hayo yanapofanyika bila kufuata taratibu rasmi, kwani huacha mianya ya ubadhirifu na ukiukwaji wa kanuni. Kwa hivyo, mabadiliko yoyote katika mradi wa umma lazima yapitishwe kupitia utaratibu uliowekwa,” alisema.

Kutokana na hali hiyo, alisema umuhimu wa kuwawajibisha viongozi na watendaji wanaokiuka mipango ya miradi ya umma kwani tatizo i linakuja pale mpango unapobadilishwa bila kufuata utaratibu kwa sababu hawasimamii mali za umma kwa mujibu wa sheria.

Alisema uwajibikaji unasaidia kujenga nidhamu na kuhakikisha miradi ya baadaye inafuata taratibu.

Karugaba alisema suluhisho la changamoto hizi ni kuimarisha mifumo ya mipango, kufuata taratibu kikamilifu na kuhakikisha uwajibikaji kwa wanaokiuka sheria.

“Tusipowawajibisha wanaokiuka taratibu, tutazidi kujenga hofu kuwa fedha za umma zinapotea, uwajibikaji ndiyo suluhisho la kurejesha imani ya wananchi.”