Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra), Habibu Suluo amewataka waendeshaji wa vyombo vya moto kufuata taratibu zilizowekwa kabla ya kufanya mabadiliko yoyote ya nauli.
Amesena ongezeko lisiloidhinishwa linaweka mzigo usio wa haki kwa abiria.
Ametoa kauli hiyo ikiwa ni saa chache tangu kutangazwa kwa bei mpya za mafuta zilizoanza kutumika leo Jumatano, Aprili mosi 2026 ambazo zimeibua malalamiko katika maeneo tofauti ikiwemo mitandao ya kijamii.
Pia kutangazwa kwa bei hizo kumechochea kupandishwa kwa nauli katika baadhi ya maeneo jambo lililoongeza mzigo kwa wananchi.
Suluo amesema wanatambua bei za petroli na dizeli zimepanda Dar es Salaam na baadhi ya waendeshaji tayari wamepandisha nauli bila kibali licha ya kuwa mabadiliko yoyote lazima yazingatie kanuni,” amesema.
Kufuatia hali hiyo, amesema Latra itafanya kikao cha wadau Aprili 8, 2026 jijini Dar es Salaam, ambacho pia kitarushwa mtandaoni ili kuwashirikisha watu wengi zaidi.
Kutokana na hili, Suluo amewataka waendeshaji kuwa watulivu na kuwahakikishia abiria kuwa Latra inalenga kulinda usawa kati ya uendelevu wa huduma dhidi ya ongezeko la ghafla la nauli.
Matokeo ya kikao hicho yataamua kama nauli mpya zinaweza kupangwa nchi nzima iwapo shinikizo la bei ya mafuta litaendelea.
Latra wanatoa kauli hiyo wakati ambao wananchi wameanza kuugulia maumivu ya athari hiyo kutokana na kulipa nauli zaidi ya waliyokuwa wakilipa awali.
Nauli hizo zimeongezeka kwa wastani wa Sh500 katika kila safari ya bodaboda na bajaji na au Sh1,000 zaidi wakati ambao wamiliki wa mabasi wakitaka mamlaka ziangalie namna ya kupandisha nauli ili wasifirisike.
Kwa mujibu wa Suluo, Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), inayosimamia bei za mafuta ilitarajia mabadiliko lakini ongezeko limekuwa kubwa kuliko ilivyotarajiwa.
Kwa mujibu wa kanuni zilizopo, waendesha mabasi wanaotaka kuongeza nauli wanapaswa kuwasilisha ushahidi unaoonyesha kuwa faida yao imeshuka chini ya asilimia 10 katika kipindi fulani.
Latra itapitia maombi hayo pamoja na maoni ya abiria na wadau wengine kabla ya kuidhinisha mabadiliko yoyote.
Hata kama nauli mpya zitaidhinishwa, zitaanza kutumika tu baada ya kuchapishwa kwenye Gazeti la Serikali na baada ya kipindi cha siku 14 kupita.
Huko bungeni jijini Dodoma, Waziri Mkuu wa Tanzania, Dk Mwigulu Nchemba amesema Serikali itaketi ili kuangalia uwezekano wa kuleta unafuu kwa Watanzania.
Akiwasilisha makadirio ya bajeti ya ofisi yake kwa mwaka 2026/27, Dk Mwigulu amesema: “Tumeona bei zimeshaanza kupanda, tutakaa ndani ya Serikali kuhakikisha tunakabiliana nalo vipi suala hili ili wananchi waendelee kupata mafuta kwa bei nzuri na kudhibiti kupanda kwa gharama za maisha.”
Hata hivyo, Dk Mwigulu amesema licha ya changamoto zinazoendelea Mashariki ya Kati, Serikali itaendelea kusimamia upatikanaji wa petroli na dizeli ili kuhakikisha bei zinaendelea kuwa himilivu.
