Mshery ampa kiburi Pedro | Mwanaspoti

YANGA ilianza mazoezi juzi kujiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara, na kocha Pedro Goncalves wala hana presha ya kumkosa kipa namba moja Djigui Diarra, huku akiridhishwa na mrithi wake.

Diarra hataichezea Yanga kwenye mechi tatu zijazo ikiwemo mbili za ligi na moja ya Kombe la Shirikisho la CRDB, kutokana na adhabu ya kusimamishwa na Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB) kwa kumfanyia vurugu mwamuzi wa mechi dhidi ya Mtibwa Sugar.

Kusimamishwa kwa Diarra hakuiumizi Yanga kwani inatamba na makipa wazuri ambao wanaweza kuziba nafasi ya Diarra wakiwemo Aboutwalib Mshery na Hussein Masalanga ambao wamekuwa wakicheza endapo kipa huyo wa Mali akikosekana.

Goncalves alisema Diarra ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa, lakini akiwa nje kwa kutumikia adhabu hiyo wala hawana presha kwa kuwa Mshery na Masalanga wanaweza kuziba nafasi yake.

Alisema msimu huu kuna mechi tatu ambazo Diarra alikosekana na bado Yanga ikaendeleza ubabe kwa kushinda zote bila ya kuruhusu bao lolote ambazo alidaka Mshery.

“Tumeanza maandalizi ya kuendelea na mechi za ligi, tulikuwa na wachezaji wote kasoro wale ambao wako timu za taifa na wale ambao ni majeruhi, lakini kila kitu kipo sawa, tunataka kuwa tayari ili turudi njia ya ushindi,” alisema.

“Tunafahamu kwamba hatutaweza kumtumia Diarra kwenye mechi zijazo kutokana na adhabu. Sidhani kama kuna haja ya kuzungumzia uwezo wa Diarra, nadhani kila timu kuna wakati zinatamani kuwa na kipa kama huyu.”

Msimu huu Mshery amesimama golini mechi tatu dhidi ya Fountain Gate, Mashujaa na Coastal Union ambazo hakuruhusu bao na Yanga ikishinda zote.

Yanga msimu huu imeruhusu mabao matatu pekee kwenye mechi zake 16 dhidi ya KMC (4-1), Dodoma Jiji (3-1) na Mtibwa Sugar (1-1) ambazo zote Diarra alikuwa langoni.