MWANAMKE AKIPEWA USAWA NI NGUZO YA UCHUMI WA FAMILIA NA JAMII

………………………..

Na Mwajabu Mhando 

Wanawake wengi
nchini Tanzania wamekuwa wakijishughulisha na biashara ndogo ndogo ili
kujipatia kipato cha kujikimu na kuendesha familia zao. Miongoni mwa biashara
hizo ni uuzaji wa mboga mboga na matunda katika masoko na mitaa mbalimbali
wanayoishi. Biashara hii imekuwa chanzo muhimu cha kipato kwa wanawake wengi,
licha ya kukabiliwa na changamoto mbalimbali za kiuchumi na kijamii.

Katika kufanya
makala hii, nilifanya mahojiano na mwanamke muuza mboga mboga mkazi wa Tandale
jijini Dar es Salaam, anayeitwa Ester George, mama wa watoto watatu. Ester
anaendesha biashara yake ndogo ya kuuza mboga na matunda ili kusaidia mahitaji
ya familia yake. Anasema kuwa alianza biashara hiyo miaka kadhaa iliyopita
baada ya kuona kipato cha familia hakitoshi kukidhi mahitaji ya kila siku.
 

Katika
mahojiano hayo, Ester anaeleza kuwa biashara ya mboga mboga na matunda imekuwa
msaada mkubwa katika familia yake. “Kupitia biashara hii naweza kununua chakula
nyumbani, kusaidia ada za watoto na gharama nyingine za familia. Mume wangu
hana kazi yenye kipato kikubwa, hivyo biashara yangu imekuwa msaada mkubwa kwa
familia yetu,” anasema Ester.
 

Licha ya
mchango huo, wanawake wengi wanaofanya biashara ya mboga na matunda hukumbana
na changamoto mbalimbali. Miongoni mwa changamoto hizo ni mtaji mdogo,
ushindani mkubwa katika masoko, pamoja na uharibifu wa bidhaa hasa matunda na
mboga zinazoharibika haraka. Pia wateja wengine huchukua bidhaa kwa mkopo lakini
hushindwa kulipa kwa wakati, jambo linalopunguza mtaji wa wafanyabiashara hawa.

Mbali na
changamoto hizo za kiuchumi, wanawake hawa pia hukumbana na changamoto za
unyanyasaji wa kijinsia katika maeneo yao ya kazi. Baadhi yao hukumbana na
maneno ya kudhalilisha, vitisho au hata vishawishi visivyofaa kutoka kwa baadhi
ya wanaume wanaowazunguka katika maeneo ya biashara.

 Ester anaeleza kuwa hali hiyo wakati mwingine
huwafanya wanawake kufanya kazi katika mazingira yasiyo salama. Kwani yeye
amekuwa ni mmoja kati ya wahanga waliokumbana na changamoto hizo ikiwemo kuitwa
majina yasiyofaa na wakati mwingine baadhi ya watu kumdhania kwamba yeye si
mwanamke anayependa kutulia nyumbani kwake.

Kwa upande wa
serikali, juhudi mbalimbali zimekuwa zikifanyika kusaidia wanawake
wafanyabiashara wadogo. Afisa wa maendeleo ya jamii na ustawi wa jamii katika
halmashauri anasema wao hutoa elimu kuhusu haki za wanawake, mbinu za kujilinda
dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia, pamoja na kuwahamasisha wanawake kujiunga
katika vikundi vya kiuchumi ili waweze kupata mikopo ya riba nafuu. Pia
serikali imekuwa ikitoa mafunzo ya ujasiriamali ili kuwasaidia wanawake hawa
kuboresha biashara zao.
 

Wadau wengine
ambao wamekuwa wakitetea haki na usawa wa wanawake nchini ikiwemo Chama cha Wanawake
Wanahabari Tanzania (TAMWA),
kupitia Mkurugenzi
mtendaji wa taasisi hiyo Dr. Rose Reuben katika kilele hicho cha siku ya
wanawake amesema licha ya uwepo wa changamoto nyingi kwa wanawake wauzaji wa
mboga mboga  ikiwemo upungufu wa usalama
, kukosekana kwa soko la uhakika na hata upatikanaji hafifu wa bidhaa lakini
bado wanaendelea kuwapa elimu wakishirikiana na benki ya CRDB kwani wanawake
wengi wajasiriamali wameahidi kupokea elimu hiyo na kuendelea kuitumia huku
kipaumbele cha mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia kikizingatiwa ili kufikia
usawa katika Nyanja zote za kijamii.

Aidha, taasisi
mbalimbali za kifedha ikiwemo Benki ya CRDB imeendelea kuwa mstari wa mbele
katika kuwawezesha wanawake wajasiriamali kupitia huduma za kifedha jumuishi,
mikopo nafuu, pamoja na mafunzo ya ujasiriamali ikiwemo kupitia programu zake
mbalimbali.
 

CRDB katika siku maalumu ya wanawake
duniani ambayo waliungana na wanawake wajasiriamali kwa kushirikiana na TAMWA
kupitia Meneja usimamizi wa mafunzo ambaye ni Joshua Mwakalobo amesema
wataendelea kutoa elimu ya fedha na ujasiriamali ili kuwainua vijana na wanake
wajasiriamali pamoja na kuwawezesha kifedha ili kuijua thamani ya pesa na
mafanikio.
 

Kwaujumla benki hiyo imefanikiwa kuwainua wanawake hawa kwa kuwapatia
mitaji na ujuzi unaowawezesha kukuza biashara zao, kuongeza kipato, na
kuboresha maisha yao na jamii inayowazunguka kwa ujumla.

Wanawake
wanaouza mboga mboga na matunda pia wana mchango mkubwa katika jamii na uchumi.
Wanachangia upatikanaji wa chakula kwa urahisi katika maeneo ya mijini na
vijijini, wanazalisha ajira binafsi, na kusaidia familia zao kupata mahitaji
muhimu kama chakula, elimu na huduma za afya. Biashara hizi ndogo ndogo pia
huchangia mzunguko wa fedha katika jamii.
 

Katika
mafanikio hayo, mchango wa wanaume nao ni muhimu. Wanaume wanaweza kuwasaidia
wake zao kwa kuwapa ushirikiano, kuwaheshimu katika kazi zao, pamoja na
kuwasaidia katika majukumu ya familia ili wanawake waweze kuendesha biashara
zao kwa utulivu. Ushirikiano wa wanandoa katika shughuli za kiuchumi unaweza
kuimarisha ustawi wa familia kwa ujumla.
 

Kutokana na
hali hiyo, jamii inapaswa kuthamini na kuheshimu kazi zinazofanywa na wanawake
hawa, huku ikiendelea kupinga vitendo vyote vya unyanyasaji wa kijinsia.
Wanawake nao wanahimizwa kuendelea kufanya kazi kwa bidii, kujiunga katika
vikundi vya maendeleo na kutumia fursa za mafunzo na mikopo zinazotolewa na
serikali na taasisi mbalimbali.
 

Kwani takwimu
mbalimbali za kiuchumi ikiwemo Global Enterpreneurship kwa mwaka 2024 inaonesha
kuna ongezeko la wanawake katika umiliki wa biashara ndogo ndogo ambazo zimekua
ni sehemu mojawapo inayochangia kukua kwa uchumi wa mtu mmoja mmoja, familia na
hata Taifa kwa ujumla.

Kwa ujumla,
wanawake wauzaji wa mboga mboga na matunda ni sehemu muhimu ya maendeleo ya
familia na jamii. Kwa kupewa mazingira salama ya kufanya biashara pamoja na
msaada kutoka kwa jamii na serikali, wanaweza kuendelea kuchangia kwa kiwango
kikubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi, wakati nchi ikikua ni vyema
kuhakikisha usalama wa wanawake na jamii nzima kwa ujumla. Kwa pamoja TUMLINDE
MWANAMKE ILI TUILINDE JAMII YETU SOTE.