Namibia Yapunguza Ushuru wa Mafuta kwa Asilimia 50 Kudhibiti Bei

Global Publishers
April 1, 2026
0 Comments

Waziri wa Nishati Modestus Amutse

Katika kukabiliana na wimbi la kupanda kwa bei za mafuta duniani, Serikali mbalimbali barani Afrika zinaanza kuchukua hatua za moja kwa moja kulinda watumiaji na kudhibiti mfumuko wa bei.

Hatua hizi zinakuja wakati mvutano wa kisiasa unaoendelea Mashariki ya Kati, hasa katika eneo la Strait of Hormuz, ukiathiri kwa kiasi kikubwa upatikanaji na gharama za nishati duniani.

Mfano wa hivi karibuni ni Namibia, ambayo Machi 27, 2026 ilitangaza kupunguza kwa muda ushuru wa mafuta kwa asilimia 50 kwa kipindi cha angalau miezi mitatu hadi mwisho wa Juni.

Hatua hiyo inalenga kupunguza makali ya ongezeko la bei kwa watumiaji huku serikali ikijaribu kuweka uthabiti wa bei za ndani katika mazingira ya soko lisilotabirika.

Akizungumza mjini Windhoek, Waziri wa Nishati Modestus Amutse amesema serikali italazimika kutumia Mfuko wa Taifa wa Nishati kuanzia Aprili 1 hadi mwisho wa Juni kufidia gharama za ongezeko hilo.

Kwa mwezi Aprili pekee, serikali inatarajiwa kutumia takribani dola za Namibia milioni 500 kufidia tofauti ya bei, hatua inayolenga kupunguza mzigo kwa wananchi licha ya bei za mafuta kupanda kwa N$2.50 (6,444 Tanzanian Shillings (TZS) kwa petroli na N$4.00 kwa dizeli.

Katika hali ambayo Namibia bado inategemea kwa asilimia 100 uagizaji wa mafuta, Serikali pia imehakikisha kuwa akiba ya mafuta inatosha kwa mwezi mmoja hadi miwili na kuwataka Wananchi kuepuka ununuzi wa hofu, huku ikilenga kudhibiti athari za mfumuko wa bei katika uchumi wa ndani.