Kwenye hadithi za Khalifa Harun Rashid wa Baghdad, tunasoma jinsi alivyoifanya dola yake kuwa bora kuliko dola nyingi za wakati huo. Ilijaaliwa kuwa na ukwasi, elimu, ustaarabu na nguvukazi bora.
Enzi zile hakukuwa na mfumo wa kidemokrasia, ni kama tujuavyo, hadi leo mifumo ya tawala za Kiarabu ni ya kifalme na kisultani. Hivyo hakukuwa na Serikali ya Taifa, Mkoa wala Mtaa.
Miongoni mwa ratiba zake, ilikuwepo ya kukutana na wananchi barazani kwake kila siku. Baraza lilikuwa kama Bunge lenye Spika na naibu wake, yaani Khalifa na Waziri Mkuu ambaye alikuwa ndiye msaidizi wake wa pekee. Pia liliendeshwa kama Mahakama na kituo cha usuluhishi. Hapo walipokea mashtaka ya kawaida kama “huyu kawatuma kazi wanangu bila kuwalipa!” Lakini iliwalazimu kuyafanyia maamuzi katika mfumo waliojiwekea.
Pia Khalifa kila mara alifanya matembezi ya kushtukiza kwenye mji wake. Huko alikutana na kesi za wafanyabiashara dhidi ya wateja wao (kwamba walipunjana kibaba cha mchele), kesi za ardhi (hasa za matajiri kuwadhulumu masikini, yatima na wajane), lakini pia zile za kugombea mipaka ya mashamba. Kwa kusaidiana na Waziri Mkuu walifanya maamuzi ya kutoa haki kwa aliyestahili.
Unaweza ukashangaa kwa nini asiteue Mawaziri, Wabunge na Watendaji katika vijiji, kata hadi mitaa. Hayo pale mwanzoni yalishafanywa, lakini tatizo kubwa la tawala za Kifalme na Kisultani ni ubaguzi.
Ukimuamini mfanyabiashara kuamua kesi ya kapuku dhidi ya tajiri, jua wazi kuwa kapuku atadhulumiwa. Unategemea nini kesi ni ya ngedere dhidi ya nyoka inapoamuliwa na hakimu nyani?
Hivyo kwa kuwa koo za matajiri ndizo zilizomiliki kila kitu pamoja na haki, masikini walikuwa sawa na watumwa. Ndio maana baadhi ya watawala walitengeneza mfumo kama wa Khalifa. Yeye ndiye aliyekuwa tajiri mkuu, lakini alikuwa na jukumu la kuongoza watu wote masikini na matajiri.
Ilimpasa kuzingatia haki, kwa sababu angewatendea vibaya masikini angebaki na matajiri tu. Wapagazi wote wangehama mjini.
Tanzania nayo imekuwa kama inayolazimishwa kufuata mfumo wa Khalifa. Sisi tuna viongozi kutoka Serikali kuu mpaka Serikali ya Mtaa. Lakini kila mahala Rais atakapotembelea, atakutana na kero za maji, miundombinu na kadhalika.
Fikiria Mheshimiwa anapokwenda kukagua miradi mipya ya maendeleo, wananchi wanajitokeza kulalamikia ukosefu wa matundu ya vyoo katika Zahanati au Shule iliyozinduliwa juzi.
Mambo haya yanatufanya tufikirie vibaya. Aidha tumekosa viongozi makini, au tunapigwa mchana kweupe. Haiwezekani usanifu ufanywe kikamilifu hadi bajeti itolewe, halafu mkandarasi ajenge nyumba bila choo.
Tunavyoelewa ni kwamba hata kama ni ujenzi wa soko, ni lazima ieleweke ni wafanyabiashara na wateja wangapi watalitumia soko hilo kila siku. Habari za upungufu wa matundu ya vyoo haiwezi kuwepo.
Katika nchi zetu masikini, ni jambo la kawaida kabisa kuona mtu aliyekubali kubeba dhamana ya kulinda mali ya umma, akigeuza mali hiyo kuwa mali yake binafsi. Rushwa, uzembe na ubadhilifu vimetawala kila kona. Wakati mwingine kunakuwa na ushahidi kamili kuwa kiongozi fulani anahusika moja kwa moja. Lakini hata akithibitika Mahakamani, adhabu yake itakuwa ni kuhamishwa kituo.
Ieleweke kuwa kunguru hafugiki. Mtu huyo akipelekwa katika kituo kingine ataendelea na uharibifu. Adhabu hii ni ya kuoneana aibu kati ya wawajibishaji na wawajibishwaji. Inajulikana wazi kuwa mfanyakazi huyu ni sawa na gurudumu lililopasuka, halifai kutumika na gari nyinginezo. Matokeo ya kulazimisha kisichowezekana ni ajali, watumishi wanaohamishwa huhamia na ubovu wao kwenye vituo vingine.
Tunaweza kuwafananisha watu hawa na wale wanaoogopwa na Khalifa. Ndio wale wabinafsi, makaburu na walafi wakubwa. Kinachofanyika na wakubwa kumpeleka kwa wasiomjua, ni sawa na mbuni anayeficha kichwa mchangani akiacha mwili wazi. Ingelikuwa afadhali mtu huyu akarekebishwe kwanza gerezani, kisha aletwe na kuangaliwa iwapo amerekebika. Lakini sijui tunawaweka wapi wahitimu waadilifu wanaohitimu kila mwaka.
Tatizo hili si geni. Mara nyingi tunaona kila kiongozi huja na safu yake. Kila kiongozi kuwa na kasi yake ya utekelezaji wa mipango, hivyo huunda timu itakayoweza kwenda naye sawa katika mfumo wake. Atakachobakiza ni wachache walioaminika tangu mwanzo ili waongeze chachu katika safu yake mpya. Lakini kumbe kuna viongozi wanafiki wenye uwezo wa kujibadili mithili ya kinyonga.
Tazama mfano huu: Tiba ya haraka ya kutibu maji yasiyo salama ni kuyachemsha maji kabla ya matumizi. Wadudu watakufa wakiyaacha maji yakiwa tayari kwa matumizi.
Lakini miongoni mwa wadudu wa majini, yupo mmoja anayejulikana kama “amoeba”. Yeye anapogundua maji yakipanda joto (kwa maana yanapochemshwa), hujifunika kwa koti lake linalohimili zaidi ya nyuzijoto 100!
Hivi ndivyo baadhi ya viongozi wenye kashfa wanavyotoboa awamu kwa awamu. Wanaweza kudumu kwenye joto na baridi bila kuungua wala kuganda.
Ndio maana kiongozi mkuu Kaisari aliweka utaratibu wa kumuwajibisha hata msaidizi wake aliyetuhumiwa. Alisema: “Mke wa Kaisari hapaswi kuwa na tuhuma”.
