Moshi. Vilio na simanzi vimetawala katika mazishi ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Kitongoji cha Masaera, Kata ya Kilema Kusini, Wilaya ya Moshi, Ezekiel Temu (54), aliyeuawa kikatili kwa kukatwa shingo na mtuhumiwa anayedaiwa kuondoka na kichwa chake baada ya tukio hilo.
Mazishi hayo yamefanyika leo Aprili 1, 2026 kijijini Masaera, yakihudhuriwa na mamia ya waombolezaji, wakiwemo viongozi wa dini na Serikali, ambao wamelaani tukio hilo wakilitaja kuwa la kinyama na lisilokubalika katika jamii.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Machi 24, 2026 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa, chanzo cha tukio hilo kinadaiwa kuhusishwa na matatizo ya afya ya akili kwa mtuhumiwa.
Kamanda Maigwa amesema mtuhumiwa alimkimbiza marehemu kabla ya kumshambulia kwa kitu chenye ncha kali, kumkata shingo na kutenganisha kichwa na kiwiliwili, kisha kuondoka nacho.
Baadaye, mtuhumiwa alikamatwa na kuonyesha alipoficha kichwa hicho.
Akihubiri katika ibada ya mazishi iliyofanyika nyumbani kwa marehemu, Padre Kalist Shayo wa Jimbo Katoliki la Moshi ameitaka jamii kumrudia Mungu na kudumisha upendo, akisisitiza umuhimu wa kuwa na imani katika nyakati za majonzi.
“Matukio kama haya yanapaswa kutufundisha kumtegemea Mungu na kuishi kwa upendo. Tuwe na subira na tumwombee marehemu, huku tukikubali ni mapenzi ya Mungu,” amesema.
Kwa upande wake, Mtendaji wa Kijiji hicho, Florencea Kong’oa, amelaani tukio hilo na kuitaka jamii kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa mapema pale wanapobaini viashiria vya uhalifu.
“Ni wajibu wa kila mwananchi kuhakikisha anatoa taarifa za uhalifu ili kuzuia matukio kama haya. Tusisubiri hadi madhara yatokee,” amesema.
Akisoma historia ya marehemu, ndugu yake Dismas Temu amedai aliuawa Machi 24, 2026 alipokuwa njiani kuelekea shambani kupanda maharage, baada ya kukutana na mtu aliyemshambulia kwa panga hadi kupoteza maisha.
