Tanzania yaahidi kukabiliana ongezeko bei ya mafuta

Dar es Salaam. Wakati kukiwa na kilio cha bei za petroli na dizeli kuwa juu, Waziri Mkuu wa Tanzania, Dk Mwigulu Nchemba amesema Serikali itaketi ili kuangalia uwezekano wa kuleta unafuu kwa Watanzania.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), kwa sasa wanunuaji wa mafuta ya rejareja yanayopitia Bandari ya Dar es Salaam, watalazimika kuongeza Sh956 kwa kila lita moja ya petroli baada ya bei kufikia Sh3,820 kutoka sh2,864.

Wakati dizeli, watununua kwa Sh3,806 kwa lita moja kutoka Sh2,858 ikiwa ni ongezeko la Sh948. Huku mafuta ya taa yakinunuliwa kwa Sh3,684 kutoka Sh2,932 iliyokuwa ikitumika Machi mwaka huu.

Ongezeko hilo limetokana na athari za mapigano yanayoendelea Mashariki ya Kati ambapo visima, maghala ya kuhifadhia mafuta, viwanda vya kusafisha mafuta na Iran kufunga lango la Hormuzi linalopitisha takribani asilimia 20 ya mafuta inayosafirishwa katika masoko mbalimbali.

Leo Jumatano Aprili Mosi, 2026, akiwasilisha makadirio ya bajeti ya ofisi yake kwa mwaka 2026/27, Dk Mwigulu amesema: “Tumeona bei zimeshaanza kupanda, tutakaa ndani ya Serikali kuhakikisha tunakabiliana nalo vipi suala hili ili wananchi waendelee kupata mafuta kwa bei nzuri na kudhibiti kupanda kwa gharama za maisha.”

Hata hivyo, Dk Mwigulu amesema licha ya changamoto zinazoendelea Mashariki ya Kati, amewahakikishia Watanzania kuwa Serikali itaendelea kusimamia upatikanaji wa petroli na dizeli ili kuhakikisha zinaendelea kuwa himilivu.

Katika hatua nyingine, Dk Mwigulu Serikali amesema Serikali itaendelea kusimamia mifumo ya kuagiza, kuhifadhi na kusambaza mafuta pamoja na kuongeza uwezo wa kupokea na kuhifadhi mafuta katika Bandari za Dar es Salaam na Mtwara.

Kwa mujibu wa Dk Mwigulu, katika kufanikisha hilo, Serikali inaendelea kutekeleza mradi wa ujenzi wa ghala la kupokea na kuhifadhi mafuta lenye uwezo wa kupokea tani 308,110 katika Bandari ya Dar es Salaam ambao umefikia asilimia 30.