UCHAMBUZI WA MALOTO: Ripoti ya CAG ni mtihani namba moja kwa Spika Zungu

Mjadala mezani ni ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), mwaka wa fedha 2024/2025. Kama ilivyozoeleka katika miaka iliyotangulia, madudu yameendelea kuwemo. Rais Samia Suluhu Hassan, ametaka ripori zijazo, wahusika watajwe ili waone soni.

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ibara ya 143, inaeleza uwepo wa CAG, wajibu wake na nguzo zake kikazi. Ukisoma Sheria ya Ukaguzi wa Hesabu za Umma, kifungu cha kumi kuhusu majukumu ya CAG, inaelekeza kuwa CAG anafanya kazi kwa niaba ya Bunge. Kwa hiyo, lile jukumu la ukaguzi ambalo CAG hulifanya ni la Bunge.

Hiyo ndiyo sababu CAG akishamaliza ukaguzi wake, ripoti yake huikabidhi kwa Rais ambaye huagiza ipelekwe bungeni. Na jukumu la Bunge ni kuisoma ripoti na kuichambua kisha kuifanyia kazi. CAG hukagua hesabu zote za Serikali na Bunge ndilo lenye wajibu wa kuisimamia sekta ya umma.

Hivyo, CAG amewekwa kikatiba na kisheria ili kulisaidia Bunge kuisimamia Serikali kimahesabu. Kwamba badala ya Bunge lenyewe kupitia kamati zake, kufanya kazi ya kukagua matumizi ya fedha za Serikali, kuchambua na kuhoji palipo na ubadhirifu, CAG anakuwepo ili kulisaidia Bunge kukamilisha kazi ya ukaguzi wa mahesabu, jukumu la Bunge linabaki kusoma ripoti ya CAG, kuichambua na kuihoji Serikali.

Kifungu cha 11 cha Sheria ya Ukaguzi wa Hesabu za Umma 2008, kinachambua mamlaka ya CAG, kwamba anaweza kumwita ofisa yeyote wa Serikali na kumhoji kuhusu matumizi ya fedha. Mamlaka hayo ni kuonesha kuwa CAG akitimiza wajibu wake, kisha Bunge likisimama imara, basi ubadhirifu hautakuwepo na mwenye kujaribu basi atakamatwa na kushughulikiwa.

Ofisi ya CAG ina bajeti. Bunge lina bajeti. Shabaha ni kuzipa ofisi zote ufanisi. Ukitazama mamlaka ya Bunge kikatiba, ungedhani Bunge ndilo lingekuwa linamlaumu CAG kwa kutofanya kazi yake sawasawa. Matokeo ni kinyume. CAG anafanya kazi. Bunge linaonekana halitimizi wajibu wake sawasawa.

Muhula wa pili wa Rais Jakaya Kikwete, ripoti za CAG zilikuwa na nguvu mno. Bila shaka ni baada ya kuanza kutumika Sheria ya Ukaguzi wa Hesabu za Umma 2008. Kamati za Bunge zilisoma ripoti na kuamua kuiwajibisha Serikali. Kuna mawaziri walipoteza kazi baada ya madudu kuonekana. Bunge la 11 na 12, hayakuochomoa meno ya kibunge. Vipi Bunge la 13?

Mwaka 2012, mawaziri Mustafa Mkulo (Fedha), Cyril Chami (Viwanda na Biashara), Haji Mponda (Afya), Omar Nundu (Uchukuzi), William Ngeleja (Nishati na Madini), waling’oka kufuatia ripoti ya CAG kutokana na msimamo wa Bunge.

Naibu mawaziri wawili nao waling’oka, Lucy Nkya (Afya) na Athuman Mfutakamba (Uchukuzi). Hicho ni kipimo kuwa Bunge lilikuwa imara, lilipokea ripoti kutoka kwa CAG, kamati zake za hesabu, PAC (Serikali Kuu), Laac (Serikali za Mitaa) na Poac (Serikali za Mitaa), zilichambua ripoti kwa umakini na kutoa mapendekezo.

Bunge zima lilipokea mapendekezo na kushughulikia Serikali. Matokeo yalionekana. Tangu Bunge la 11, hakuna wakati wowote, ripoti za CAG zimepata kufanyiwa kazi.

Desemba 2018, aliyekuwa CAG, Prof Mussa Assad, alifanya mahojiano na idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa, akaeleza masikitiko yake kuwa Bunge la Tanzania lilikuwa dhaifu, ndiyo maana alitoa ripoti zenye kasoro nyingi za Serikali, lakini hatua hazikuchukuliwa.

Chambilecho Waingereza “business as usual”. Mambo hayajabadilika tangu Assad aliposema Bunge ni dhaifu mpaka sasa. Ripoti ya mwaka wa fedha 2016-2017, ilibaini Sh1.5 trilioni ilipotea na haikuwa na maelezo.

Spika wa Bunge la Tanzania, Mussa Zungu, anayo nafasi ya kuhakikisha ripoti ya CAG inafanyiwa kazi ipasavyo bungeni. Zungu amekuwa mbunge tangu mwaka 2005. Huu ni muhula wake wa tano. Alikuwepo nyakati za Bunge lenye kuibana mbavu serikali. Bunge na kashfa ya Richmond mwaka 2007 – 2008. Bunge na Oparesheni Tokomeza Ujangili mwaka 2013, na Bunge dhidi ya kashfa ya Tegeta Escrow mwaka 2014.

Zungu amekuwa na uzoefu wa uendeshaji wa vikai vya Bunge kwa muhula wa nne sasa. Mwenyekiti wa vikao vya Bunge mwaka 2010 – 2015 na 2015 – 2020. Naibu Spika 2021 – 2025, na sasa Spika. Anayo nafasi ya kuhakikisha hadhi ya Bunge inarejea mahali pake.

Haya mambo, uwanja uwanja wa wa michezo wa Arusha, upembuzi yakanifu kuonesha gharama za matengenezo yangekuwa Sh187 bilioni, hadi kukamilika kwake, lakini mkataba uliosainiwa kuwa Sh338 bilioni, majibu yake na hatua stahiki, ni kazi ambayo inatakiwa kufanywa na Bunge. Wananchi watafurahi hatua zikichukuliwa.

Upande wa CCM, wana nafasi kubwa ya kuamua majibu yapatikane na hatua zichukuliwe. Asilimia 98 ya wabunge ni CCM. Hivyo ni sahihi kuliita Bunge la CCM. Uchaguzi unapofanyika, chama ndicho kuwaangukia wananchi kuomba ridhaa ya kuongoza, kwa Ilani na ahadi kemkemu.

Baada ya uchaguzi, chama kwa kutambua kuwa chenyewe ndicho kiliomba ridhaa kwa wananchi, hupaswa kuisimamia Serikali, ihakikishe inatimiza ahadi zote, vilevile kuendesha nchi kwa namna ambayo itakidhi maagano na mapatano ya kipindi cha kampeni.

Kwa kuwa chama kinatakiwa kuwa juu ya Serikali yake, CCM kupitia sekretarieti, au Kamati Kuu, ikiwezekana hata Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec), wanapaswa kuwabana mbavu wabunge ili waende bungeni wakaitende kazi. Vinginevyo, kwa ripoti za CAG kutofanyiwa kazi, ni masizi kwenye joho jeupe kwa chama hicho.

Rais Samia, kwa nafasi yake ya uenyekiti CCM, hapaswi kusubiri ufike mwakani ndiyo CAG awataje majina wahusika. Hata ripoti ya mwaka huu, anaweza kuitisha mkutano wa Nec, kisha watoe maazimio ya kuwashinikiza wabunge wajadili ripoti bila woga, na kuwataja waziwazi wezi wa mali za umma. Hakuna haja ya kusubiri.