Vita ndani ya ODM inavyochora ramani kuelekea uchaguzi 2027

Dar es Salaam. Siasa za Kenya zimeingia katika hatua mpya yenye misuguano mikali huku taifa hilo likiwa tayari limeianza safari ya kuelekea uchaguzi wake mkuu wa 2027, hali inayodhihirisha wazi mapambano ya ushawishi, mgawanyiko wa ndani ya vyama na mabadiliko ya ghafla ya muungano wa kisiasa.

Katika kipindi hiki, macho mengi yameelekezwa ndani ya chama kikuu cha upinzani, Orange Democratic Movement (ODM), ambacho kwa miaka mingi kimekuwa mhimili wa siasa mbadala nchini humo.

Hata hivyo, kwa sasa chama hicho kinakabiliwa na hali isiyo ya kawaida, ikiwa ni pamoja na mpasuko wa wazi wa kimtazamo unaotishia uimara wake kisiasa.

Mgawanyiko huo umejidhihirisha kupitia makundi mawili yenye mitazamo tofauti kuhusu mustakabali wa chama.

Kundi linaloongozwa na Katibu Mkuu wa chama, Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna, linaonyesha msimamo mkali wa kupinga aina yoyote ya ukaribu au ushirikiano na serikali ya Rais William Ruto.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara mwishoni mwa wiki, Sifuna alisisitiza kuwa yuko tayari kusimama imara kulinda misingi ya chama, akipinga kile alichodai ni juhudi za kukisogeza karibu na mamlaka ya serikali.

Kauli hiyo imeibua mjadala mkubwa ndani na nje ya ODM, ikiwagawa wanachama na wadau wa siasa kuhusu mwelekeo sahihi wa chama hicho.

Kwa upande mwingine, viongozi wanaomuunga mkono Mwenyekiti wa chama, Oburu Oginga, wanaonekana kuwa tayari kufungua milango ya mazungumzo ya kisiasa na serikali ya Ruto. Kambi hiyo inaamini kuwa ushirikiano wa kimkakati unaweza kuwa na manufaa ya kisiasa na hata kusaidia chama kujipanga upya kuelekea uchaguzi ujao.

Hatua ya makundi haya mawili kuandaa mikutano tofauti kwa wakati mmoja imeongeza taharuki ndani na nje ya chama hicho, huku wachambuzi wakitafsiri hali hiyo kama ishara ya mpasuko unaoweza kuathiri uwezo wa ODM kujipanga kwa ushindani wa 2027.

Kwa chama kilichojengwa juu ya mshikamano wa kisiasa kwa muda mrefu, hali hii ni ya kipekee na yenye uzito mkubwa katika mwelekeo wa siasa za Kenya.

Kauli kali za Sifuna zimezidisha mijadala kuhusu mustakabali wa ODM, wengi wakijiuliza iwapo chama hicho kitaendelea kubaki na utambulisho wake wa upinzani thabiti au kitaingia katika siasa za maridhiano zinazoweza kukipunguzia makali yake.

Wakati ODM ikikabiliwa na changamoto za ndani, upande wa serikali nako hali si shwari. Rais Ruto na aliyekuwa Naibu wake, Rigathi Gachagua, wameendelea kurushiana maneno hadharani, kila mmoja akijaribu kujijengea uhalali na kuimarisha kambi yake kisiasa kuelekea uchaguzi wa 2027.

Mvutano wao umechukua sura ya kampeni za mapema, ambapo majukwaa ya kisiasa yamegeuka kuwa uwanja wa kushambuliana kwa hoja na takwimu.

Ruto amekuwa akimlaumu Gachagua kwa kile anachodai ni kushindwa kuunga mkono kikamilifu utekelezaji wa ajenda za serikali wakati alipokuwa madarakani.

Kwa upande wake, Gachagua ameanza kujijenga kama sauti mbadala ya kisiasa, hasa kwa vijana, akishambulia sera za serikali kwa madai ya kushindwa kuboresha maisha ya wananchi wa kawaida.

Taswira hii inaonyesha wazi kuwa mgawanyiko ndani ya serikali nao una mchango mkubwa katika kuchora ushindani wa kisiasa nchini humo.

Wachambuzi wanaona kuwa Gachagua anaweza kujijenga kama mpinzani mwenye nguvu kutokana na ushawishi wake katika eneo la Mlima Kenya, ambalo limekuwa na uzito mkubwa katika kuamua mwelekeo wa siasa za taifa hilo.

Aidha, uwepo wa Rais mstaafu wa Kenya, Uhuru Kenyatta katika mazingira haya unaongeza mvuto wa kisiasa katika kambi inayoweza kumpa nguvu Gachagua.

Ndani ya ODM, wachambuzi wanaeleza kuwa moja ya sababu kuu ya hali ya sasa ni kukosekana kwa kiongozi mwenye mvuto wa kitaifa kama ilivyokuwa hapo awali.

Kwa muda mrefu, chama hicho kilijengwa chini ya ushawishi wa Raila Odinga, ambaye alikuwa mhimili mkuu wa siasa za upinzani nchini Kenya.

Kutokuwepo kwake katika mstari wa mbele wa siasa za uchaguzi wa 2027 kumeacha pengo ambalo sasa linajazwa na makundi yenye mitazamo tofauti.

Hali hii kwa mujibu wa wachambuzi, ni ya kawaida kwa vyama vinavyotegemea umaarufu wa mtu mmoja, ambavyo hupitia misukosuko mara tu vinapokosa kiongozi wa kuunganisha pande zote.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Conrad Masabo anasema ODM ipo katika hatua ya mpito na kwamba, iwapo haitapata mwelekeo mpya wa pamoja, inaweza kupoteza mvuto wake kwa wapiga kura. Anaongeza kuwa vyama vingi duniani hupitia changamoto kama hizi, hasa vinapokabiliwa na mabadiliko ya uongozi.

Pamoja na changamoto hizo, mfumo wa kisiasa wa Kenya tangu kupitishwa kwa Katiba ya Kenya ya 2010, umeendelea kutoa nafasi pana ya ushindani.

Katiba hiyo imeimarisha taasisi muhimu kama mahakama na kuweka misingi ya uwajibikaji, hali inayoruhusu mijadala mikali ya kisiasa bila kuyumbisha misingi ya dola.

Hata hivyo, wachambuzi wanaonya kuwa migogoro ya ndani ya vyama isipopatiwa ufumbuzi wa kudumu inaweza kuathiri ubora wa ushindani wa kisiasa na hata kupunguza imani ya wananchi kwa vyama vya siasa.

Kwa mtazamo mpana, Kenya inaelekea katika uchaguzi ambao unaweza kuwa na ushindani mkali zaidi kuliko chaguzi zilizopita. Mchanganyiko wa mgawanyiko ndani ya vyama, mivutano ya viongozi wakuu na mabadiliko ya ghafla ya miungano ya kisiasa unaashiria kuwa wapiga kura watakuwa na chaguzi nyingi, lakini pia changamoto ya kuchambua nani anawakilisha nini.

Swali linalobaki ni iwapo siasa za Kenya zitaegemea zaidi kwenye hoja za msingi kama uchumi, ajira na maendeleo, au zitaendelea kutawaliwa na mihemko, misimamo binafsi na makundi ya kikabila ambayo kwa muda mrefu yamekuwa na ushawishi mkubwa.

Kadiri mwaka 2027 unavyokaribia, jambo moja linaonekana wazi; Kenya inaelekea katika uchaguzi ambao hautakuwa wa kawaida. Utakuwa mtihani wa uimara wa vyama vya siasa, nguvu ya viongozi binafsi na uwezo wa mfumo wa kisiasa kusimamia ushindani mkali bila kuyumbisha taifa, katika mazingira ambayo kwa mara ya kwanza baada ya miongo kadhaa, Raila Odinga hatakuwa mhusika mkuu katika kinyang’anyiro hicho.