Wadau wataja sababu, suluhu kujirudia madudu ripoti ya CAG

Dar es Salaam. Haijawahi kupita ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) bila kuibua upotevu wa mabilioni ya fedha wala uzembe katika ufanisi wa usimamizi wa mashirika ya umma.

Hii inatoa picha ya kujirudia kwa changamoto; kila mwaka upungufu ukibainishwa, lakini utekelezaji wa ushauri kwa baadhi ya mambo unabaki kitendawili kisichoteguka.

Hali hiyo, inaelezwa na wachambuzi wa siasa na uchumi kuwa haitokani na tatizo la kiutendaji pekee, bali pia mifumo inayosababisha kusiwe na uwiano kati ya mamlaka za usimamizi, ushawishi wa kisiasa na uhuru wa kitaalamu.

Hayo yanakuja siku moja baada ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere kuwasilisha kwa Rais Samia Suluhu Hassan ripoti za ukaguzi kwa mwaka wa fedha 2024/2025, zinazoonyesha hasara na upotevu wa mabilioni ya fedha katika baadhi ya mashirika.

Miongoni mwa mashirika yaliyotajwa kupata hasara kwa mujibu wa ripoti hiyo ni Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), lililopata hasara ya Sh191.19 bilioni, ikiongezeka kwa asilimia 108 kutoka hasara ya mwaka wa fedha 2023/24.

Pia, Shirika la Reli Tanzania (TRC) lilipata hasara ya Sh3.06 bilioni, iliyotokana na ajali zilizosababisha uharibifu wa miundombinu ya reli ya zamani ya MGR.

Upotevu mwingine wa fedha umetajwa katika utekelezaji wa baadhi ya miradi, likiwemo Bwawa la Umeme la Julius Nyerere (JHPP) ambako kiasi cha Sh1.48 trilioni kimepotea.

Katika ripoti hiyo aliyoiwasilisha, Kichere ametaja sababu ya kukwama kwa utekelezaji wa mapendekezo yake kuwa ni kukosekana kwa mifumo madhubuti ya uwajibikaji katika taasisi za Serikali.

Alisema katika mapendekezo 38,181 yaliyotolewa na ofisi hiyo kuanzia miaka ya nyuma hadi sasa, asilimia 36.7 pekee ndiyo yametekelezwa, asilimia 43.5 yako katika utekelezaji na asilimia 7.5 hayajatekelezwa kabisa.

Kichere amekwenda mbali zaidi na kueleza kuwa kumekuwepo na mapendekezo yasiyotekelezwa kwa miaka saba hadi 20, jambo linaloonyesha changamoto ya kudumu katika ufuatiliaji wa utekelezaji na kushindwa kushughulikia vyanzo vya matatizo.

 “Hali hii inaendelea kuhatarisha upotevu wa rasilimali za umma na kudhoofisha ufanisi wa taasisi,” amesema.

Siasa inaingilia utaalamu
Kujirudia kwa hasara na dosari katika ripoti hizo kunachochewa na kuwepo kwa mgongano kati ya siasa na uendeshaji wa kitaalamu wa mashirika ya umma, kama inavyoelezwa na mchambuzi wa siasa, Said Majjid.

Kwa mtazamo wake, Majjid anasema mashirika hubeba ajenda za kisiasa badala ya kuendeshwa kwa misingi ya kibiashara na ufanisi, hali inayosababisha maamuzi yasiyozingatia faida au tija bali kulinda masilahi ya kisiasa.

Siasa pia, kwa mujibu wa Majjid, zinaingilia hadi uteuzi wa viongozi wa baadhi ya mashirika; badala ya kuzingatiwa weledi na uzoefu, uteuzi huathiriwa na ukaribu wa kisiasa.

“Hii inapunguza uwezo wa taasisi kufanya maamuzi magumu ya kibiashara, kama kupunguza gharama au kubadili mifumo isiyofanya kazi,” amesema.

Changamoto nyingine, mchambuzi huyo amesema, ni udhaifu wa bodi za wakurugenzi ambazo mara nyingi hushindwa kusimamia ipasavyo utendaji wa menejimenti.

Badala ya kuwa chombo cha kusahihisha mwelekeo, ameeleza bodi hujikuta zikiendeshwa na taarifa zinazochujwa au zisizokamilika.

Amesisitiza kuwa uwajibikaji unapokuwa dhaifu, hata ripoti kali za CAG zinaishia kuwa nyaraka za kumbukumbu badala ya nyenzo za mabadiliko.

“Kila mwaka tunasikia upungufu uleule kwa sababu wakosaji hawalipi gharama kwa dosari na hasara wanazozisababisha,” amesema.

Usimamizi tatizo
Kwa mtazamo wa Dk Lazaro Swai, aliyebobea katika taaluma ya usimamizi wa rasilimali watu na utawala, tatizo lipo kwenye mfumo mzima wa usimamizi wa fedha za umma, hususan udhibiti wa matumizi na ukusanyaji wa mapato.

Ameona katika mashirika mengi kuna mianya ya upotevu wa fedha inayotokana na mifumo ya kizamani au isiyounganishwa, yaani isiyosomana.

Yote hayo, amesema yanasababishwa na kukosekana kwa teknolojia madhubuti za kufuatilia mapato na matumizi, hivyo kufanya iwe rahisi kwa ubadhirifu kujificha ndani ya mifumo.

Tatizo jingine, amesema analiona katika utegemezi wa ruzuku kutoka serikalini, ambao unapunguza nidhamu ya kifedha. Mashirika yanapojua kuwa yatasaidiwa hata yakipata hasara, motisha ya kuboresha ufanisi inapungua.

“Kuna changamoto ya mipango dhaifu ya biashara. Mashirika mengi yanaanzisha miradi bila tafiti za kina za soko au tathmini ya hatari, hivyo kujikuta yakizalisha hasara badala ya faida,” amesema Dk Swai.

Tatizo lingine bungeni
Denis Konga, mtaalamu wa utawala bora wa Chuo cha Diplomasia cha Dk Salim Ahmed Salim, anaona kiini cha tatizo ni kulegea kwa uimara wa Bunge, taasisi ambayo kimsingi ndiyo sauti ya wananchi na mhimili mkuu wa uwajibikaji wa Serikali.

Anasisitiza kuwa iwapo wananchi wangepata fursa ya kuchagua wawakilishi wao kwa uhuru na ufanisi zaidi, Bunge lingekuwa na nguvu ya kuisimamia Serikali ipasavyo.

Hata hivyo, anabainisha changamoto iliyopo ni baadhi ya wabunge kujiona sehemu ya Serikali badala ya kuwa wasimamizi wa Serikali, hali inayodhoofisha jukumu lao la msingi la kuhoji na kuwajibisha.

Kukosa uwajibikaji
Kwa upande mwingine, mchambuzi wa masuala ya utawala bora, Faraji Mangula amesema juhudi za kudhibiti upotevu wa fedha za umma haziwezi kuzaa matunda bila hatua madhubuti dhidi ya wahusika.

“CAG ameshaweka wazi kila kitu, sasa mamlaka husika zichukue hatua. Kukosekana kwa hatua kunazua taswira ya udhaifu au hata kuhusika kwa wanaopaswa kuwajibisha,” amesema.

Mangula ameonya kuwa bila uwajibikaji wa kweli, upotevu wa fedha za umma utaendelea na kudhoofisha imani ya wananchi, huku akipendekeza kuimarishwa kwa mifumo au kuundwa kwa chombo maalumu cha kusimamia uwajibikaji iwapo taasisi zilizopo zitashindwa kutekeleza wajibu wake.

Nini kifanyike
Ili kubadili hali hiyo, Majjid amependekeza kuwepo kwa mfumo wa wazi wa kuwawajibisha viongozi wa mashirika watakaokutwa wamesababisha hasara.

Amesema mikataba ya utendaji inapaswa kuwa na viashiria vinavyopimika na kuwe na adhabu iwapo utashindwa kuleta tija, pamoja na motisha iwapo utazalisha matokeo chanya.

Aidha, ameshauri Serikali ipunguze mwingiliano wa kisiasa katika uendeshaji wa mashirika, badala yake iweke mazingira ya ushindani na uhuru wa kitaalamu, huku ikibaki na jukumu la usimamizi wa sera na si uendeshaji wa kila siku.

Kwa upande wa Dk Swai, amependekeza uwekezaji katika mifumo ya kidijitali ya usimamizi wa fedha ili kuhakikisha fedha zinafuatiliwa, jambo litakalosaidia kupunguza mianya ya ubadhirifu na kuongeza uwazi.

Amesisitiza umuhimu wa mashirika kujitegemea kifedha kwa kupunguza utegemezi wa ruzuku, huku yakiboresha huduma na bidhaa zao ili zishindane sokoni na kuvutia mapato.

Kuhusu hilo, Konga anasema suluhisho la kudumu linahitaji Bunge lenye meno, linaloweza kusimama kidete kulinda masilahi ya umma.

Aidha, anaelekeza kuwa tayari kuna taasisi zenye mamlaka ya kisheria ya kuchukua hatua dhidi ya wanaojihusisha na rushwa na ukwepaji kodi, hivyo kinachokosekana si sheria bali utekelezaji wake.

Katika sekta ya afya, ripoti ya CAG imebainisha kuwepo kwa baadhi ya vifaatiba vyenye thamani ya Sh5.17 bilioni vilivyosambazwa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya katika halmashauri mbalimbali lakini havitumiki.

Kutotumika huko, Kichere amesema kunatokana na ukosefu wa wataalamu, miundombinu duni na kukosekana kwa umeme wa uhakika.

Akizungumzia hilo, Mtaalamu wa Afya ya Jamii, Dk Catherine Masawe amesema kuwepo kwa vifaatiba bila matumizi ni sawa na kuwa na rasilimali zilizokufa ndani ya mfumo wa afya.

Amesema vifaa kama mashine za uchunguzi, vipimo vya kisasa au vifaa vya upasuaji vinapokaa bila kazi, husababisha upotevu wa fedha za umma, pia huathiri ubora wa huduma na kuongeza muda wa wagonjwa kusubiri huduma muhimu.

Hali hiyo, amesema inahatarisha kupungua kwa imani ya wananchi kwa vituo vya afya vya umma; wagonjwa hulazimika kwenda kwenye huduma binafsi za gharama kubwa na wakati mwingine hata kuchelewa kupata matibabu sahihi.

“Hali hii inaonyesha changamoto si tu ya ununuzi wa vifaa, bali pia ya maandalizi ya mfumo wa kuhakikisha vifaa hivyo vinatumika kwa ufanisi na kuleta tija iliyokusudiwa,” amesema.