Morogoro. Katika juhudi za kuinua kiwango cha elimu ya sayansi na teknolojia, taasisi ya African Olympiad Academy (AOA) imeanzisha kambi maalumu ya mafunzo ya hisabati, ikilenga kuibua na kukuza vipaji vya wanafunzi wenye uwezo mkubwa katika masomo ya sayansi.
Kambi hiyo imewaleta pamoja zaidi ya wanafunzi 40 kutoka sehemu mbalimbali za Tanzania, wakipatiwa mafunzo ya kina, kushindanishwa, na kuandaliwa kushiriki mashindano ya kimataifa ya hisabati. Lengo ni kuwajengea wanafunzi uwezo wa kufikiri kwa kina, ubunifu na ustadi wa kutatua changamoto ngumu za kihisabati.
Akizungumza wakati wa kufunga kambi hiyo leo Aprili 1, 2026, Mwanzilishi Mwenza na Mkuu wa Shule wa AOA, Gaidi Faraj, amesema wanafunzi bora watashiriki Pan-African Math Olympiad nchini Ivory Coast Juni mwaka huu, na International Math Olympiad nchini China Julai. “Dhamira yetu ni kuandaa kizazi kipya cha vijana wa Afrika wenye uwezo wa kushindana katika sayansi, teknolojia, na akili bandia (AI),” amesema Faraj.
Mkurugenzi wa Ufuatiliaji na Tathmini kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Makuru Petro akisikiliza jambo kutoka kwa Mwenyekiti wa Chama cha Hisabati Tanzania, Dk Said Sima wakati kufunga kambi hiyo mkoani Morogoro. Picha na Juma Mtanda
Aidha, Chama cha Hisabati Tanzania (MAT/Chahita) kimeandaa kambi ya wanafunzi 34 bora kutoka shule mbalimbali za sekondari, ikilenga kuandaa washiriki wa mashindano ya kikanda na kimataifa. Mwenyekiti wa chama hicho, Dk Said Sima, amesema Tanzania imeanza kuonyesha mafanikio makubwa, ikiwemo nafasi ya tatu katika mashindano yaliyofanyika Afrika Kusini mwaka 2024 na kuingia katika orodha ya nchi 10 bora mwaka jana.
Baadhi ya wanafunzi walioshiriki wamesema wamejipanga kufanya vizuri katika mashindano hayo. Nyanduhu Theophil (18) kutoka Shule ya Sekondari Kibaha alieleza ndoto yake ya kuiletea Tanzania medali ya dhahabu, huku Buthayna Mohammed (16) kutoka Feza Zanzibar akihimiza wasichana kujitokeza katika masomo ya sayansi.
Hata hivyo, ufinyu wa bajeti umebainika kama changamoto, kwani mashindano ya kimataifa mara nyingi yanategemea ufadhili wa nje. Dk Sylvester Ruguihyamu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ameomba Serikali kuongeza bajeti ili wanafunzi wote waweze kushiriki kikamilifu.
Mkurugenzi wa Ufuatiliaji na Tathmini kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Makuru Petro, amesema Serikali ina mkakati wa kuongeza ufaulu wa hisabati kutoka asilimia 25 hadi viwango vinavyokidhi ushindani wa kimataifa, huku akisisitiza umuhimu wa vijana kujitokeza na kuonyesha umahiri wao.
